Simulizi : Siku 100 Za Mateso Ya Kuzimu
Sehemu Ya Kwanza (1)
IMEANDIKWA NA : ALLY KATALAMBULA
KISIWA cha Guam kilichopo katika bahari ya Pasific ndio kisiwa kikubwa kuliko kisiwa kingine chochote katika bahari hiyo, kisiwa hicho kiko umbali wa kilometa zaidi ya 800 kutoka nchini Marekani ambapo huchukua masaa zaidi ya 18 kusafiri kwa ndege kutoka mji wa New York hadi kufika katika kisiwa hicho.
Kama ungepata bahati ya kuona mandhali ya Msitu mkubwa unaopatikana kwenye kisiwa cha Guam ungeona miti mirefu yenye matawi mapana, sanjari na nyasi fupi zenye ukijani kibichi wenye kuvutia.
Jioni moja katika msitu wa Guam zilisikika sauti za mbwa zilizokwenda sambamba na sauti za milunzi ya ndege waliokuwa wakishangilia na kuimba nyimbo zisizo na maana yoyote kwenye masikio ya binadamu.
Hali ye hewa ilikuwa shwari, jua la jioni lilikuwa linazama taratibu huku likiacha mwanga wenye rangi ya njano na mionzi yenye joto hafifu.
Kadiri muda ulivyokuwa unayoyoma ndivyo mwangwi wa sauti za mbwa na ndege zilivyokuwa zikiyeyuka taratibu, mambo yale yakawa yanatendeka taratibu, yanii mwanga wa jua ukawa unazidi kufifia, giza likawa linachukua hatamu na sauti za mibweko ya mbwa ikawa inaishilizia.
Hatimaye giza lilingia, na muda mfupi badaye, kila kitu kikawa kimya!
Wakati mabadiliko hayo ya kidunia yakiendelea kutendeka katikati ya msitu ule, kulikuwa na mwanaume mmoja aliyekuwa taabani, alikuwa amelala chini, damu nyingi zilikuwa zimetapakaa mwilini mwake.
Alikuwa na majeraha makubwa mwilini.
Mtu huyo ambaye umri wake ungeweza kuukisia kati ya miaka thelathini ama thelathini na tano, alikuwa amevaa suti nyeusi ambayo ilionekana kuwa ghari kabla ya kutapakaa damu na vumbi.
Hali ilivyoonyesha ni kama alipoteza fahamu kwa muda mrefu sana kutokana na maswahibu yaliyomkuta, alikuwa akihema kwa tabu.
Wakati huo giza lilikwisha ingia na kumeza nuru yote ya nchi. Wingu jeusi la mvua lilionekana kwa mbali, kukawa na ngurumo ndogo za radi zilizokwenda sambamba na mvumo wa upepo, kiasi cha lisaa limoja tangu nuru imezwe na giza zito, matone ya mvua yakanza kushuka kidogo kidogo kwenye msitu ule wa Guem. .
Matone ya mvua yalipomdondokea mtu yule, fahamu zikamtwaa! akafumbua macho, akakunja sura alipogundua anamaumivu makali sana mwilini mwake.
“Aaagh!” alitoa mguno. Maumivu makali yalimwathibu alipojaribu kusimama.
Alijikaza, akajikaza na kujikaza, hatimaye akanyanyuka na kukaa kitako huku mgongo wake akiwa ameuegemeza kwenye mti, akawa anahema kwa nguvu kama katoka kwenye mbio ndefu, alitumia dakika moja kufikiri ni jambo gani limemfanya awe pale.
Alionyesha taharuki kubwa baada ya kukumbuka kila kitu kilichotokea hadi kupelekea kuwa katika hali ile.
Alitizama juu kama mtu aliyetegemea kuona kitu fulani, lakini baada ya kuona hakuna alichotegemea akajawa na woga.
Alijinyanyua kwa tabu na kusimama wima, akapiga hatua moja, akaona anaweza kutembea. Akawa anachechemea huku akitizama huku na kule kama mwenye kutafuta kitu fulani, bado hakuweza kuona kile alichotarajia.
Giza lilikuwa nene ndani ya msitu huo, mvua ndogo ikawa inanyesha na kukatika huku upepo ukivuma kwa kasi.
Yule mtu alipuyanga katika ule msitu kwa muda wa kama nusu saa, kwa mbali akawa anasikia sauti ya kitu kama mawimbi. Naam!...Yalikuwa ni mawimbi ya bahari yaliyokuwa yakijisukuma kwa nguvu katika pwani na kurudi baharini.
Akaongeza mwendo kuelekea uelekeo ambao sauti ya mawimbi ya bahari yalisikika, alipita kwenye madimbwi na matope, akakatiza vichakani na hatimaye alitokea kwenye fukwe.
Giza lilikuwa limezagaa eneo lote la fukwe wa bahari, yule mtu alibaki akimangamanga macho huku na kule
“Any one here?” alisema kwa lugha ya Kingereza akimaanisha kama kuna mtu yoyote pale. hakuna kilichosikika zaidi ya mawimbi ya habari yaliyokuwa yakijisukuma kwa nguvu ukingoni mwa bahari.
Mvua ilipungua kidogo, na haikuchukua muda mrefu zaidi ikakatika.
Mtu yule aliketi chini kwenye mchanga akionekana kukata tamaa, bado maumivu ya majeraha mwilini mwake yalizidi kumsurubu, akiwa chini alingiiza mkono mfukoni mwake kisha akatoa simu ndogo ya mkononi.
Simu ile ilikuwa imezimwa, akaiwasha... Nuru ya mwanga ikaonekana, uso wake ukaonekana kuwa na faraja, lakini faraja yake ilidumu kwa dakika chache baada ya ile simu kuwaka.
Kwenye kioo cha simu ilionesha kutokuwepo na mtandao, lilitokea neno lilisomeka ‘network error’ alizima simu na kuiwasha tena, bado simu ile iliendelea kuwa na tatizo la mtandao. Network ilikuwa haipo.
Alisimama akawa anatangatanga mwelekeo mmoja hadi mwingine, mkono alioshika simu ukiwa juu, akijaribu kuona kama atabahatisha mtandao lakini bado neno ‘network error’ liliendelea kutokea kwenye kioo cha simu yake.
Alikata tamaa, kwa msaada wa mwanga wa simu yake saa yake ya mkononi ikamwonesha ilikuwa ni saaa tatu usiku.
“Kwa nini niwe hapa? Na kwanini niwe peke yangu? Kitu gani kilitokea” mtu Yule alinong’ona, maswali aliyokuwa akijiuliza hapakuwa na wa kumpa majibu.
Alibaki njia panda!!
Giza zito lililokuwa limezagaa kwenye kisiwa cha Guem lilizidi kumchanganya mtu yule, akawa anapuyanga ukingoni mwa ufukwe akiwa hajui ni wapi anakwenda!
Kijiupepo kilichotokea baharini kilifanya maungo ya mwanaume yule kutetemeka, baridi ikawa ni kitu kingine kilichochochea maumivu ya jeraha baya lilikokuwa ubavuni mwake.
Sauti moja akilini ikamweleza:
“Endelea kusonga mbele, huko ndiko kuna msaada,” aliitii sauti ile kwa moyo mmoja, akazidi kuzipiga hatua kwenda asikokujua.
Kadiri muda ulivyokuwa ukiyoyoma ndivyo giza zito lilivyokuwa likitanda katika anga na kufanya usiku huo kuwa na weusi wa kutisha, kelele ya mawimbi ya maji yaliyokuwa yakijibamiza kwenye ufukwe na kurudi baharini, ndicho kitu kipee kilichosikika. Eneo lote lilikuwa kimya.!!
Akiwa ametembea umbali wa kama nusu kilometa, ghafla!!! kishindo kikubwa kikasikika umbali wa kilomita kama mbili ama tatu.
“Boooooom!”
ilikuwa ni sauti ya kitu kama bomu. Ndani ya muda huohuo mwale mkali wa moto ukaonekana angani na kutawanyika katika anga, giza nene lililokuwa limetanda likang’aa.
Mtu yule alibaki ameduwaa kwa kile alichokiona, akili yake ikahamanika kwa tukio lile. Akakimbia kwa kuchechemea kuelekea kule moto ule ilipokuwa ukiwaka.
Alipokuwa akikaribia kwenye tukio lile, sauti za watu waliokuwa wakilia na kuomba msaada zilisikika. Akazidi kusogea. Sauti zile zikazidi kulindima masikioni mwake, hatimaye akafika eneo lile na kujionea tukio lililokuwa likiendelea.
Ndege kubwa ya abiria ya Panasonic Airline ilikuwa ikiungua vibaya mno, ndani kulikuwa na watu alishuhudia tukio baya sana, abiria waliokuwa wakiungulia ndani ya ndege hiyo hapakuwa na hata mtu mmoja aliyejishugulisha kutoa msaada kwa watu wale. kila mtu alikuwa bize kukoa roho yake.
Kulikuwa na pilikapilika eneo lile, huyu alienda kule huyu alirudi huku, zilisikika sauti za akina mama zikiwaita watoto wao.
Wengine walikuwa wakiomba msaada wa kimatibabu kutokana na kuvunjika na kupata majeraha milini mwao, hakuna aliyemjali mwenzake wakati ule. Kila mtu aliangalia uhai wake.
Yote hayo yalishuhudiwa na yule mtu akiwa hatua chache kutoka eneo lile lenye patashika.
Kwa mara nyingine tena akatupa macho kwenye kioo cha simu yake, bado mtandao ulikuwa haupo.
“Please help me....help to move out from fire,” sauti ya mtu mmoja alisikika ikiomba msaada kuondolewa karibu na moto.
ITAENDELEA...
SHEA NA WENZIO ILI TUZIDI KUSONGA MBELE...
Tags
simulizi