TROPEA - Mji wa wafu
SEHEMU YA 03
ILIPOISHIA.......
Alisafa akigugumia maumivu, punde si punde akadondoka chini akapoteza fahamu. Akiwa katika hali hiyo, alistaajabu yupo katika ulimwengu mwingine wakati huo kwa mbali zilisikika sauti za nafsi zikilalama.
ENDELEA NAYO.....
Sauti hizo za ajabu zilimshtua Seya, wakati huo punde si punde ulitokea mwanga mkali, mwanga ambao haukudumu sana ukatoweka kisha ikatokea barabara ndefu ambayo pembeni ilipambwa mafuvu. Seya alipigwa na taharuki ya kujikuta yupo katika ulimwengu mwingine, hofu zaidi ikamjaa baada kusikia sauti za nyimbo zikiimba kwa kumkaribisha Tropea. Ni sauti ambayo ilipenya vyema masikioni mwake.
"Seya..Seya karibu katika himaya ya mizimu ya Abdi. Amini tatizo lako limekwisha endapo kama utakubaliana na matakwa yetu" Wakati hofu ikiendelea kumtanda Seya, ghafla alisikia sauti ikimwambia maneno hayo, sauti hiyo ilikuwa ya Sultan wa mji ule wa Tropea, mji ambao wakazi wake ni wafu japo binadamu wa kawaida hufika huko kwa shida zao mbali mbali mfano mwenye shida kama ya Seya aidha utajiri.
"Matakwa? Matakwa gani hayo na wewe ni nani?.." Aliuliza Seya kwa sauti ya woga kwa sababu sauti hiyo aliyoisikia ilimuogopesha sana kulingana na namna ilivyokuwa ikisikika.
"Ahahahahah Hahahahaha. Seyaa?.." Ilisema sauti hiyo huku ikijirudia mara mbili mbili. Punde nguvu ya ajabu ikamvaa, nguvu hiyo ikamuongoza Seya kwenye hiyo barabara iliyopambwa mafuvu. Kitendo hicho kilimfanya Seya kupiga mayowe ya kuogopa, lakini mayowe yake hayakuweza kufua dafu zaidi muda mchache baadaye alijikuta yupo chumbani, chumba ambacho kilionekana cha ajabu kikipambwa mapambo mbali mbali sambamba na kunukia marashi kuwahi kutokea Duniani.
Seya alipagawishwa na mambo hayo, wakati huo huo mlango wa chumba hicho ulifunguliwa akaingia kiumbe cha ajabu. Kiumbe huyo alionekana sio binadamu wa kawaida, alikuwa na kichwa chenye mapembe, mwili mkubwa huku sehemu mbali mbali za mwili wake yakionekana magamba ya nyoka. Mbali na hayo, mtu huyo meno yake yalionyesha ni meno ya dhahabu lakini vile vile masikio yake yalikuwa yamepanda juu japo macho yake yalikuwa ya kibinadamu. Katika paji la uso wa kiumbe huyo wa kutisha zilionekana namba 666.
"Karibu Seya, mimi ndio mtu pekee nitakae kutatulia tatizo lako" Alisema kiumbe huyo huku akizidi kumsogelea Seya pale kitandani.
Seya hakusema neno lolote, bado moyoni akiwa na woga jambo ambalo lilimpelekea kukataa kile ambacho kiumbe wa ajabu alicho dhamiria kukifanya juu yake.
"Seya siku nzima umehitimisha, na hii ni siku ya pili tangu uingie Tropea. Tambua unamuda mchache sasa kuendelea kuwa huku sababu Duniani umeacha mwili wako na upo katika harakati za kuzikwa. Endapo kama hutouwahi mapema basi habari yako itakuwa imefika kikomo " Kwa jazba kiumbe huyo aliongea. Maneno hayo yalimshtua Seya, akataharuki kujigundua kuwa yupo katika hali ya nafsi. Wakati alipokuwa ameshikwa na bumbuwazi, ghafla mbele yake ukutani ukatokea mwanga mfano wa Tv, katika mwanga huo akaonyeshwa kinacho endelea Duniani. Ndipo Seya akapata kuona namna ndugu wanavyomlilia, umati wa watu ukiwa umehudhuria msiba wake, lakini pia alipata kuuona mwili wake ukiwa katika harakati za kuhitimisha maandalizi ili ukazikwe.
Hakika alijihisi kuchanganyikiwa Seya ilihali muda huo kiumbe huyo wa ajabu alimfuata kitandani, akamsogelea ikiwa akakumbuka agizo aliloambiwa kabla hajafika mahali hapo alipo. Maneno yale yalijirudia kichwani mwake, mara baada kuyakumbuka alitulia akisubiri kiumbe huyo atamfanya nini. Kilicho fuata hapo ni tendo la ndoa.
*******
Ilikuwa ni kisa kifupi mzee Ndole alichokuwa akiwasimulia vijana wale pale kijiweni, kisa ambacho kiliwaacha midomo wazi vijana hao.
"Sawa mzee lakini bado hatujaona sababu inayotufanya tusimsaidie kijana mwenzetu" Alisema kijana mmoja.
Mzee Ndole alishusha pumzi huku akionekana kutaka kusema jambo, lakini kabla hajasema chochote kijana wa pili aliongeza kusema
"Na je, hayo mambo ya Tropea umeyajuaje? Au na wewe ulikuwa huko?.."
"Naam! Kabisa maswali yenu mazuri." Alisema mzee Ndole kisha akaendelea kusimulia kisa hicho cha kusisimua, kisa kifupi kilicho muhusu mama Bingo.
Mara baada kumalizika kwa tendo hilo, tayari upande wa pili Duniani kila kitu kilikuwa kimeshakamilika, na mwili wa Seya ulikuwa kwenye machera ukipelekwa kuzikwa. Lakini kabla haujafikishwa kaburini, ghafla Seya akawa amekohoa. Ni jambo ambalo liliwashangaza watu wengi, kwa maana hiyo Seya tayari alikuwa ameshatoka Tropea, hivyo kitendo cha nafsi yake ukauvaa mwili wake kilimpelekea kuzinduka. Lakini endapo kama angelizidi kukataa kufanya jambo lile, basi Seya angelikuwa bado yupo Tropea.
Siku zilisonga miezi ikasogea, hatimaye sasa Seya akapata ujauzito na akajifungua mtoto wa kiume ambaye ndio Bingo. Mzee akaweka kituo kwanza punde akaendelea kusema, Bingo sio damu ya mzee Abacha kama wengi mnavyo dhania, bali Bingo ni mtoto wa sultani wa Tropea mmiliki wa ngome ya mizimu ya Abid. Na ndio maana kijana yule begani ana muhuri, muhuri ule unamaana kubwa ingawa anaishi nao pasipo kujua.
Na vile vile kuhusu mimi kufahamu hayo ni sababu nilikuwa na ukaribu sana na mama Bingo, hivyo aliniambia yote yaliyotokea huko. Seya hakunificha kitu, na magonjwa hayo anayoumwa ni shauri ya kukaidi masharti aliyopewa huko Tropea. Pindi alipokuwa huko aliambiwa mtoto atakapo zaliwa arudi tena Tropea lakini Seya hakufanya hivyo kitendo ambacho kilimpelekea kupigwa pigo la magonjwa yasio pona. Maradhi hayo ni shauri ya kuyakaidi masharti au agizo kutoka Tropea mji wa wafu. Alihitimisha mzee Ndelo kwa kuwasimulia mkasa huo mfupi ulio muhusu mama BINGO. Baada ya kusema hayo akawapa onyo vijana hao waliotaka kumsaidia Bingo.
Mzee Ndelo alipokwisha kusema hayo aliondoka zake. Muonekano wake upo rafu sana, kamwe mtu asingemdhania aidha kukaa naye kuanza kuzungumza masuala ya msingi lakini ghafla vijana hao wakajikuta wakijua siri nzito, yenye utata kuhusu Bingo na mama yake kupitia mzee huyo ambaye alidharaulika kwa kiasi fulani lakini pia sio vijana hao, vile vile kijana Bingo alijua suala hilo baada kujibanza sehemu pindi aliposikia kwa mbali mzee Ndelo akisimulia mkasa huo wa kusisimua.
Baada Bingo kujua ukweli huo, akageuza shingo yake kutazama bega lake la kushoto kisha la kulia ambapo kwenye bega la kulia alipata kuiona chapa ya fuvu. Alitaharuki sana, alishindwa kujua ni nini chanzo ya chapa hiyo, lakini pia inamaanisha nini! Kabla hajapata jawabu sahihi, ghafla akaguswa bega lile lile lenye chapa. Upesi akageuka, kwa mara nyingine tena akakutana uso kwa uso na yule mrembo aitwaye Roya.
"Kwanini unanifuata fuata?.." Kwa hasira pasipo woga Bingo alimuuliza Roya.
"Mnanifanya naishi kwa mashaka, kwani nimewachukulia kitu gani?.." Aliongeza kuhoji Bingo.
"Ahahahah Hahaha ha" Roya akacheka kwa madaha huku akipiga makofi. Alipo hitimisha cheko lake akasema. "Punguza jazba Bingo, hasira hasara. Sijaja kwa ubaya ila nimekuja kukupa muongozo namna ya kufika mji wa Tropea, huko ndipo kuna dawa ya kumponya mama yako na si vinginevyo.. " Roya alipomaliza kusema maneno hayo akapotea huku akiamuacha Bingo akijiuliza kuhusu mji huo wa Tropea, mji uishio wafu.
Kitendo hicho kilimuogopesha sana Bingo, haraka sana akatimua mbio kurudi nyumbani kwao. Alipofika alipitiliza moja kwa moja mpaka chumbani kwa mama yake, huko aliketi kando yake kisha akasema.
"Mama, hivi mimi ni mtoto wa wa nani? Nataka uniambie ukweli pasipo kunificha" Maneno ya Bingo yalimshtua mama yake, aligeuka akiwa pale pale kitandani kisha na kumtazama kwa mashaka.
"Kwanini unasema hivyo? Ama kwa kuwa baba yako ameamua kututelekeza?.." Alihoji kwa sauti ya upole iliyojaa taharuki ndani yake.
"Si hivyo mama, hivi Tropea ni wapi?.." Aliongezea kuhoji Bingo, swali ambalo lilizidi kumuweka katika wakati mgumu mama yake, kiasi kwamba akashindwa kujua mwanaye maneno hayo ameyatoa wapi.
"Bingo mwanangu, ni simulizi ndefu sana lakini kwa sasa bado mapema kufahamu ukweli lakini siku yoyote nitakukwambia"
"Nini? Sio vizuri mama. Ni vile hujui tu tabu gani mwanao naipata, ila laiti kama ungeijua basi ungeniambia ukweli ili nikachukua mamuuzi yaliyo sahihi" Alifoka Bingo.
"Mamuuzi gani? Na tabu gani ambayo unaipata? Na jina hilo umelisikia wapi? Bingo hali yangu yenyewe hii lakini bado unataka kuniweka roho juu, kwanini lakini?.." Alisema mama Bingo akimuasa mwanaye ambaye alionekana kughazibishwa na jambo hilo la siri. Hapo Bingo hakusema jambo lolote, zaidi alinyanyuka na kisha kuondoka zake na kwa kuwa tayari usiku ulikuwa umeingia, hivyo alifanya maandalizi ya chakula cha usiku.
Muda wa kula ulipowadia Bingo alikuwa kimya, aliongea tu wakati anaelekea chumbani kwake kulala. Kitendo hicho kilionyesha wazi kabisa amekasirishwa na siri ile ambayo mama yake ameendelea kuikumbatia. Alipolala, punde usingizi ulipo mpitia usiku kwa mara nyingine tena akaota ndoto ya ajabu sana, aliota kuwa yupo makaburini saa za usiku. Mbele yake aliona jeneza likiletwa mahali alipokuwa amesimama huku akiwa na hofu kali, mwili wake ukitetemeka hali ya kuwa kijasho chembamba nacho kikimtoka.
Watu wale waliolibeba jeneza walizidi kumsogelea Bingo, ajabu walipomkaribia wakapotea na punde si punde mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali pamoja na radi za hapa na pale ilianza kunyesha. Alizidi kuogopa Bingo, ikiwa muda huo huo hajui wapi pa kukimbilia zaidi alibaki kusimama akisubiri nini hatma yake. Mbele yake lilionekana kaburi pia, kaburi ambalo lilionyesha kuwa lazamani sana. Kaburi hilo ghafla likaanza kutikisika, muda mchache baadaye ulitokea mkono hivyo hivyo mpaka mwili wote ukawa kwenye uso wa dunia. Mtu huyo alikuwa amevaa sanda iliyo chakaa, sehemu mbali mbali za mwili wake walimtoka wadudu lakini pia alikuwa akitoa harufu mbaya sana.
"Mungu wangu" Alisema Bingo huku akirudi nyuma akimuogopa yule mtu aliyefufuka lakini wakati anarudi nyuma, bado mambo yakawa ni yale yale, wafu waliendelea kufufuka kadri muda ulivyokuwa ukisogea. Ndani ya muda wa nusu saa mamia ya wafu walionekana pale makaburini. "Bingo.." Ilisikika sauti nzito ya ajabu ambayo ilijirudia mara mbili mbili. Sauti hiyo ilimuita Bingo. Bingo kutokana na woga pia na hofu aliyokuwa nayo aliogopa kuitika. Alibaki kurudi nyuma tu ilihali wale wafu nao wakimfuata, punde hatua zake zilifika ukingoni. Kuna kitu alikigusa nyuma kwa kisigino, hivyo akageuka nyuma ili atazame kitu hicho, aliona jeneza lile ambalo hapo awali aliliona likiwa limebebwa na watu kabla hawajapotea katika mazingira tatanishi. Na ndani ya jeneza hilo aliuona mwili wake, kitendo ambacho kilizidi kumuogopesha akajikuta akikimbia huku na kule kama mwenda wazimu. Lakini mwishowe alijikuta akiwa katikati ya kundi lile la wafu, na katika wafu wale alikuwemo na mfu ambaye alifanana naye kila kitu achilia mwili ule aliouona ndani ya jeneza. Balaa.
"Bingo, wewe ndio mrithi wa ngome ya Abdy. Hivyo jiandae wakati wa kuelekea Tropea umekaribia, kwa sababu wewe ni damu yetu" Maneno hayo aliyasema yule mfu ambaye amefanana naye. Baada sauti hiyo wafu wale wengine walipotea akabaki yule mfu aliyefanana nae. Aliongeza kusema "Sifikirii kama utakwepa njia hii ya kufika Tropea, lakini pia kufika kwako huko sio kama ndio utakuwa mwisho wa maisha yako hapa duniani. Tambua hata sisi tulikuwa kama wewe"
"Kwanini mnanifuatilia sana? Na hiyo ngome ya Abdy inanihusu nini mimi?.." Aliuliza Bingo kwa sauti ya woga.
"Ahahahah. Hahahhaa" Mfu yule aliangua kicheko, cheko la kutisha lililoshabiana kila kitu na ngurumo ya mvua. Radi ikamurika, punde ngurumo nzito ikapaza. Ilizidi kumtia woga Bingo.
"Abdy, hii ni ngome tata sana iishio Tropea. Tropea huu ni mji ambao watu wake ni wafu. Kwahiyo basi kuna mgongano baina ya ngome hiyo na ngome ya Shuda. Hizi ni ngome mbili tofauti ingawa zote wafuasi wake ni wafu,. Mtoto wa Sultan Starlon anataka kumiliki ngome zote mbili ikiwemo ya baba yake lakini pia ngome ya baba yako Sultan Abatish ambaye tayari ni mzee. Kupitia hilo Abatish ameamuwa kutuma watu wake waje kukutafuta wewe binadamu mwenye asili ya Abdy ili ukapigane kuikomboa ngome hiyo iliyo mashakani" Alipokatisha cheko lake alijibu.
" Je, hakuna mtu mwingine mpaka mimi?"
Aliuliza tena Bingo kwa taharuki kubwa akitishwa na maneno hayo aliyoyasema mfu huyo. Kabla mtu huyo hajamjibu, Bingo aliongeza kusema. "Hamuoni kama mimi nipo katika harakati za kumlea mama yangu kipenzi ambaye yapata miaka mingi akiwa mgonjwa?.. "
" Ahahahahaha " Aliangua kicheko mfu huyo kwa mara nyingine tena. Kwisha kuhitimisha kicheko chake akasema. "Unataka mama yako arudi katika hali yake? Basi kama unatamani iwe hivyo karibu Tropea, njoo uokoe ngome ya Abatish ili mama yako awe huru sasa.. "
Alisisitiza mfu huyo kisha akanyong'onyea na punde si punde akageuka nyoka akatokomea kwenye wigo wa kaburi.
Hapo Bingo akashtuka kutoka usingizini huku akihema juu juu wakati huo huo maneno yale aliyoambiwa na yule mfu kwenye ndoto yakijirudia kichwani mwake. Akakumbuka pia na maneno yale aliyoambiwa na yule Ajuza wa ajabu kwenye ndoto mara baada kumuelezea habari kuhusu upatikanaji wa dawa itakayo mfanya mama yake kupona.
"Dawa ipo Tropea! Mji uishio wafu itakulazimu ufe ili kufika huko"
Tags
simulizi