KISA CHA NABII NUH(a.s) NA MWANAMKE ALIYESAHAULIKA
Wakati nabii Nuh (Aleihi salaam) alipokuwa akiiunda mashua itakayowaokoa waja wema na viumbe vingine kutokana na gharka, alikuja mwanamke mmoja mzee na kumwuuliza, " Mashua hii itasafiri lini?" Nabii Nuh alimjibu, "bado." Basi yule mama kaketi pale akisubiri hadi jioni ilipofika akaenda zake kwake nyumbani.
Siku ya pili karudi mapema asubuhi akaketi akimsubiri nabii Nuh amalizie kuitengeza mashua ili wasafiri. Aliketi mpaka ulipoingia usiku akarudi kwake.
Ikawa ndio mtindo wake kila siku aje amtizame nabii akifanya ile kazi ya kuunda meli hadi jioni kisha arudi kwake. Nabii alipoona yule mama yuajichosha kwa kuja kwake kila siku akamwambia asije tena atamtaarifu Meli ikiwa tayari kung'oa nanga ili wasafiri wote.
Ilipofika wakati Allah ameamrisha Mbingu na ardhi zitoe maji yake, meli iliolea baharini akiwemo Nuh,wafuasi wake na wanyama aliowakusanya yule mwanamke alisahaulika. Kwa sababu Nuh alighafilika kumtaarifu kama alivyomuahidi kwenda kumtwaa ili wasafiri pamoja.
Basi yakapita masiku ya kupita hadi gharka ilipokoma, Nabii Nuh akauona mji mpya ambao alikuwa haujui. Sehemu hiyo ilikua kavu na waliposhuka melini akaona kwa mbali taa yawaka kwenye nyumba moja akaenda kuangalia ni nani yupo pale. Alipofika alistaajabu kumwona yule mwanamke aliemwahidi kua atamchukua safarini na akamsahau, akamwuuliza yule mama, " ni vipi kwani huku hakunyesha?" Yule mama akamjibu , "La,hakujanyesha huku kwa mda ispokuwa tu mangurumo ya radi,umeme na upepo mkali." Nabii Nuh alishindwa kuelewa haya maana dunia nzima ilinyesha na mafuriko ya ajabu ambayo hayajawahi kutokea. Basi akamwuuliza mola wake kuhusu hili na Allah akamjibu, " hakika sisi tumemsitiri mama huyu ili kuilinda ahadi yako ulompa."
Tags
Elimu