MTEMI ISIKE KATIKA HISTORIA YAKE
Alitawala kuanzia mwaka 1885, yeye alikuwa mtoto wa Mt Kiyungi kama alivyokuwa Swetu Kalonga ambaye aliwaua nduguze wa tumbo la Fundikira ili tumbo la Kiyungi litawale kwa nafasi bila kuingiliwa na tumbo la Fundikira. Swetu Kalonga kwa mara nyingine tena alimshawishi kaka yake Isike wawaue tumbo la Fundikira ili wajihakikishie utawala utabaki katika tumbo lao la Kiyungi.
Mt Isike alikubali ndipo akapanga mipango na wazee (wanikulu) wamwite Nyanso Bint Fundikira toka kwake Ndevelwa na akifika Ikulu ya Itetemya wamuue, wakachimba shimo na wakachomeka mikuki na miti yenye ncha kali ndani yake kisha wakaliwekea fito nyembamba kwa juu na kulifunika kwa majani wakaweka kiti juu yake ili atakapokuja Nyanso wamkaribishe akae katika kiti hicho atumbukia shimoni ili mikuki imchome mpaka afe..
Kwa bahati wakati wakipanga mipango hiyo nje alikuwepo mtoto wa kaka yake Ifuma akiitwa Kipini aliwasikia yote waliyopanga , Kipini yeye alikuwa mwehu ndipo alipokuja shangazi yake Nyanso kuitikia wito wa Mt Isike yeye Kipini alianza kumwambia Nyanso "sengi ngenewikale hanahohisumbu wasimbagaliina watulaga na masonga walikova wakuwulage, ngeneugeme kwikalanaho" ndipo Nyanso na wazee wakabaki wanashangaa mlinzi mmoja wa Nyanso akaenda akakiondoa kile kiti akakikalia yeye kwanza , akasimama akaanza kuchoma choma na mkuki pale palipokuwa kiti akaona mchanga unatumbukia ndani ya shimo ndipo Nyanso akamuuliza Mt Isike "nasumulakii mbona uliova kuniwulaga?
Mt Isike akawa hana jibu. Nyanso akakasirika sana akaamua kuondoka na kurudi Ndevelwe, Kisha akaenda bomani kwa DC akaomba msaada wa kumpiga vita Isike ili wamuondoe kwenye utawala na huo ulikuwa mwaka 1889. Dc akamwita kamanda wa majeshi ya Ujerumani aitwaye Bw Sakarani(Von Prince) na kumpa kazi ya kumuondoa Isike katika utawala.
Von Prince akaendesha vita ya kumpiga Mt Isike, vita vikapiganwa kwa miaka minne majeshi ya Ujerumani yalishindwa kumuondoa Mt Isike. Ndipo Sakarani akatuma ujumbe kwa Mtemi Isike kumwambia vita isimame. Mtemi Isike alikubali na vita ikasimama. Kumbe bwana Sakarani ( von Prince) alikuwa anataka kuichunguza Ikulu ya Itetemia na uimara wa jeshi la Unyanyembe ndipo akaamua kuomba msaada wa waarabukwa kiongozi wa waarabu akiitwa Msolopa akakubali kumpeleka Ikulu ya Itetemya kama vile kumpa pole kwa vita ya kupambana na Wajerumani . Von Prince akaenda kwihara akavaa nguo za kiarabu, kilemba na kanzu wakaondoka kwenda Itetemya wakiwa jumla watu wanne .Walipofika Mt Isike akawapokea baada ya kunywa chai akaomba awatembeze Ikulu ili wamsaidie kuitengeneza kwa kuwa ilipigwa mizinga mitatu lakini haikubomoka.Baada ya kuwatembeza wakala chakula cha mchana na wakaaga wakaondoka.
Baada ya kuisoma Ikulu ya Mtemi Isike, Von Prince akaagiza silaha mpya na zenye nguvu na za kisasa kwa wakati huo ili aivamie tena Ikulu hiyo. Ilipofika tarehe 22/2/1893 silaha ziliwasili
na majeshi ya ujerumani yalivamia tena Ikulu ya Itetemya , walipigana kwa takriban mwaka mmoja hivi majeshi ya Mtemi Isike yakashindwa vita, ndipo Mtemi Isike akakamatwa na walipotaka kumpeleka bomani akakataa Von prince akamwambia basi utanyongwa Mtemi isike akasema bora ndipo akamnyang'anya kamba mmoja wa askari akajifunga shingoni akapanda katika kiti akajinyonga.
Tags
Historia