Simulizi : Siku 100 Za Mateso Ya Kuzimu
Sehemu ya tano - 5
Amosi alianza kutimua mbio kurudi kule alikowaacha wenzake, tendo lile wakati linafanyika huku nyuma vile vicheko vya watu wasionekana viliibuka tena.
Wakati anazidi kukimbia ile sauti ya mama yake iliyokuwa ikiomba msaada ilisikika ikimwita kwa jina lake na kumwomba msaada. Amosi aliziba masikio alikwisha tambua mauzauza yale yalihusiana na majini.
Aliendelea kukimbia bila kuchoka, Mungu si Athumani, akafanikiwa kutokezea kwenye fukwe, mahali alikowaacha wenzake.
Alikuwa akihema huku akiwa na wasiwasi mkubwa.
“Ni nini?..umepatwa na kitu gani?” alikutana na maswali lukuki kutoka kwa wenzake ambao aliwaacha ufukweni.
“Kuna majini!! Nimekutana na majini...huko porini kuna majini!!” Amosi alijibu kwa wahaka, akili yake ilikuwa imepagawa vibaya sana.
“Majini?” mtu mmoja akauliza kwa mshangao.
“Ndio...Majini”
“Kwa hiyo aliyekuwa anapiga kelele za kuomba msaada siyo mama yako?” Mzee William akahoji kwa kiherehere.
“Ndiyoo.”
Baada ya jibu hilo, wale watu walionusurika kwenye ajali ya ndege ya Panasonic Airline walibaki kimya, kila mmoja akifikiria lake ndani ya kichwa chake.
“Nadhani kunusurika kifo kwenye ajali ya ndege ndio kumeifanya akili yako ichanganyikiwe...” Mzee William alisema.
“Awali ulituleza mama yako ulimsafirisha kama maiti ndani ya ndege, sauti ya mtu inasikika ndani ya msitu, unasimama unasema huyo ni mama yako.
“Unapuyanga msituni kama mwendawazimu unarejea hapa unatueleza ndani ya msutu huu kuna majini sijui vitu gani...hii si jambo la kiungwana, nadhani ulitakiwa kutulia na wenzako tukiongoja msaada. Hilo unalolifanya ni kuongeza hali ya wasiwasi kwa watu hawa ambao kimsingi wanahitaji msaada wa mwili na akili.” Alisema mzee William.
Watu wote wakatikisa vichwa kuafiki maneno ya mzee yule. Macho ya wenzake yalimtizima kama punguani ambaye amethiriwa na Pombe.
Amosi akaishiwa nguvu, alitamani aingie kwenye nyoyo za wale watu awaleze ukweli halisi juu ya vituko vilivyopo ndani ya kisiwa kile walichoangukia.
“Unapuyanga msituni kama mwendawazimu unarejea hapa unatueleza ndani ya msutu huu kuna majini sijui vitu gani...hii si jambo la kiungwana, nadhani ulitakiwa kutulia na wenzako tukiongoja msaada wa kuturudisha katika nchi zetu. Hilo unalolifanya ni kuongeza hali ya wasiwasi kwa watu hawa ambao kimsingi wanahitaji msaada wa mwili na akili,” alisema mzee William.
Baada kauli hiyo, Amosi akaishiwa nguvu, alitamani aingie kwenye mioyo ya wale watu awaleze ukweli halisi juu ya matukio ndani ya kisiwa kile walichoangukia. Macho ya watu wale yalimtizima kama punguani ambaye amethiriwa na Pombe, ambaye amenusrika kifo kwenye tundu la sindano.
Kila mtu alimpuuza kwa kiwango kikubwa, alibaki amebung’aa huku uso wake ukionesha kuchanganyikiwa vibaya sana.
Abiria wale waliketi sehemu moja kila mmoja akiwa na tumaini kubwa la kupata msaada wa siku inayofuatia, vikohozi na kwikwi za maumivu za hapa na pale zilisikika.
Amosi naye akaketi hatua chache huku kichwa chake kikiwa kimevurugwa vibaya sana, dakika thelathini zilipita tangu kioja kile kitokee.
Wakati huo ilikuwa yapata saa nane usiku, giza lilikuwa kubwa, hapakuwa na kilichokuwa kinasikika zaidi ya moto uliokuwa ukimalizia kunguza mabaki ya ndege ile ya Panasonic Airline, mawimbi ya bahari yaliyokuwa yakijibamiza kivivu ukingoni mwa fukwe pia yalitoa sauti ndogo.
Kila mtu alimini hadi wakati huo hawakupata msaada kutokana majira yale kuwa ni usiku, mategemeo yao walimini siku inayofuatia ndio wakati wa ukombozi.
Wakati mambo hayo yakipita vichwani mwao, kwa upande wa Amosi yeye alikuwa kwenye mgogoro mkubwa wa kifikra, matukio yalikuwa yamemtokea ndani ya muda mchache yaliharibu kabisa akili yake.
Ubongo wake haukuwa kwenye suala la kuondoka, alichokuwa anakitaka kwa upande wake ni kumaliza ile sintafahamu iliyokuwa imeibuka ghafla katika msitu ule.
Kila alipokuwa akifikiria uwezekano wa kutokea mambo yale katika maisha ya kawaida akili yake ilikuwa inakataa kabisa kukubaliana na jambo hilo.
“Au inawezekana kweli nimechanganyikiwa!!” alijiuliza mwenyewe.
“Hapana, sijachanganyikiwa nina uhakika wa yale niliyoyashuhudia ni sahihi kabisa” Amosi akawa kwenye mkanganyiko wa kupingana na fikra zake mwenyewe.
Usiku wa siku hiyo, ulikuwa mrefu kwa kila mtu aliyekuwa kwenye kisiwa hicho aliona masaa yanakwenda taratibu mno, hakuna mtu aliyelihitaji giza, shauku ya kila mmoja ilikuwa ni kuona kunapambuzuka na msaada unapatikana.
Kama wasemavyo Waswahili hakuna marefu yasiyokuwa na ncha, hatimaye kukaanza kupambazuka. Kwa mbali, kile kibaridi cha asubuhi lilianza kuingia kwenye minofu ya miili ya watu wale, hata hivyo, hilo halikuwa ni tatizo kubwa kwao, walichokuwa wanakitaka kwa wakati huo ni msaada.
Majeruhi wale walijikunyata lakini moyoni wakiwa na matarajio makubwa. Kila mtu aliamini kile kilichokuwa kikwazo kwao kuchelewa kupata msaada, kimetoweka, walichokuwa wanangoja kwa wakati huo ni kupambazuke vizuri kwa siku mpya.
“Muda wa kupata msaada umewadia,” mtu mmoja miongoni mwao alisikika akisema, wengine wakatikisa vichwa kukubalina naye. Nyuso zao zilionekan kuwa na matarajio makubwa sana.
Jua la asubuhi lilianza kuchomoza, kwa mujibu wa saa zao ilikuwa inaelekea kuwa saa mbili kasoro, watu wale wakasimama, shauku ya kuona helkopta ama boti za ukombozi ikawa ya juu.
“Nadhani watakuja na Helkopta,” alisema mtu mwingine macho yake yakiwa angani kuangaza kila kona.
Wingu na bahari vilikuwa tupu, hapakuwa na dalili ya boti wala helkopta.
“Nitashangalia nikiona helkopta,” mwanamke mmoja alinong’ona
“Mimi nitamshukuru Mungu” wakawa wanaambiana wao kwa wao. Hata hivyo muda ukazidi kuyoyoma bila kuona wala kusikia sauti ya helkopta ama boti
“Tutapata msaada kweli?” mwingine aliuliza kwa mashaka.
“Tuendelee kusubiri.” Akajibiwa na mwenziye.
“Kweli watakuwa na taarifa juu ya kuanguka kwa Panasonic Airline?”
“Nina uhakika taarifa zitakuwa zimekwishaenea dunia nzima.”
“Sasa kwa nini hadi sasa hakuna dalili zozote za watu wa ukumbozi?”
“Inawezekana wanaendelea kutafuta mahali tulipoangukia.”
“Ni muda mrefu lakini umepita tangu tupate ajali. Na hii ni saa mbili”
“Tuwe na subira,” alijibu mtu yule.
Wakati wote ambao watu wale walikuwa kwenye presha ya kungoja vyombo vya ukumbozi, Amosi alikuwa ameketi kwenye mchanga akili yake ikiwa bado imechanganyikiwa vibaya mno.
Masaa yakazidi kwenda, saa tatu, nne, tano, hadi inafika saa nane mchana, hapakuwa na dalili yoyote ya msaada.
Watu wakaanza kupatwa na njaa, wengine wenye wajeraha wakawa dhoofuli-hali, baadhi ya watu wakakata tamaa, wengine waliokuwa na roho ngumu bado waliendelea kuamini watapata msaada.
“Amosi....Amosi..Amosi,” wakati huo huo sauti moja ilisikika nyuma ya mvualana yule, sauti hiyo ilitokea kichakani, iliita kwa kunong’ona, alipogeuka hakuamini alichokiona.
Mama yake mzazi akiwa amesimama ukingoni mwa kichaka huku akionekana mwenye wasiwasi na mashaka, alikuwa amevalia gauni refu na la kupendeza, gauni hilo lilikuwa likiburuzika chini kiasi cha kuziba kabisa visigino vya miguu yake.
Amosi alitambua vazi hilo ni yeye aliyelinunua masaa machache kabla ya mwanamke huyo kufariki dunia, wakati jambo hilo likiendelea kuvuruga akili yake, macho yake yakaendelea kutoamini kioja kingine kilichoibuka mbele yake.
Mwanamke yule ambaye ni mama yake mzazi aliyekuwa mfu ndani ya ndege kabla ya kupata ajali na kuibuka kama mzimu katika mazingira yale tata, aliendelea kusimama ukingoni mwa kichaka kile huku akibadilisha mapozi kama vile bibi harusi aliyesimama mbele ya mpiga picha na kufotolewa picha zitakazopamba ukurasa wa jarida la mapenzi.
Wakati kioja kile kikijidhihirisha kwenye mboni za macho yake, muda huohuo kumbukumbu ya mazungumzo yake ya mwisho na mwanamke yule alipokuwa hoi taabani kwenye hospitali ya St August akitaka anunuliwe gauni lile, ikamjia kichwani:
“Nakufa..mwanangu nakufa..”
“Usiseme hivyo mama madaktari wamesema unayonafasi ya kuishi.”
“Hilo halitawezekana, nakuomba ufanye jambo moja.”
“Lipi mama?”
“Kaninunulie gauni, nataka gauni la harusi...nikifa hakikisha unanivisha gauni hilo.”
Kumbukumbu ya mazungumzo yale ilipita kwenye kichwa chake, alibaki amemkodolea macho mtu yule aliyekuwa amesimama kwenye ukingo wa kichaka.
ITAENDELEA....
Tags
simulizi