SIKU 100 ZA MATESO YA KUZIMU
SEHEMU YA NNE - 4
Kama ni hivyo ni jambo la kumshukuru Mungu...lini wanarudi?” swali lile liliuchoma moyo wa Kiba, hakujua nini alitakiwa akiseme kwa mzee yule.
“Mbona kimya..?” mzee aliuliza tena huko uso wake ukionesha udadisi.
“Siku si nying...”
“Nkriii...nkriiii...nkriiii,” kabla hajamalizia mara simu yake ya mkononi iliita kwa nguvu, akili yao ikahamia kwa kwenye simu.
“Hellow.”
“Kaka upo nyumbani?” ilikuwa ni sauti ya mdogo wake wa kike aitwaye Sarah.
“Ndio, nipo nyumbani”
“Fungulia Aljazeera kuna habari ya kushangaza.”
“Habari gani?” Kiba aliuliza huku akishika rimoti na kuweka Chanel ya ile.
“Kuna ndege inaitwa Panasonic Airline ya Marekani ilikuwa imebeba abiria zaidi ya 250 imepotea na haijulikani ilipo,” sauti ya Saraha ilisikika.
“Mungu wangu!” Kiba alihamaki, ndege ambayo alikuwa akipewa habari zake ndiyo ambayo siku wa kuamkia siku hiyo, Amosi alimweleza ataitumia kusafiri na maiti ya mama yao.
Akawa ameduwaa mbele ya Televisheni, huku simu ikiendelea kuwa sikioni, ufahamu wake ulikuwa kwenye taharuki kubwa kwa taarifa zilizokuwa zikipenya kichwani mwake.
BREAKING NEWS:
“250 people including two pilots of Panasonic Airline are suspected to be died just after flight they were tlavelling with, lose track of direction” (Watu 250 na marubani wawili wa ndege ya Panasonic Airline wanadaiwa kupoteza maisha yao kutokana na ndege hiyo kupotea) ilikuwa ni sehemu ya taarifa za awali ambazo ziliripotiwa kwa kurudiwarudiwa na televisheni ya Aljazeera.
“Amosi kafa....amosi amekufa... amosi kafariki” Kiba alishindwa kabisa kujizuia, ujasiri wa kiume ulimponyoka, alijikuta akipiga kelele kama mwehu.
Mzee Mikidadi ambaye muda wote alikuwa kimya, alijikuta na yeye anaingia kwenye jakamoyo kubwa, sauti ya Kiba ikamstua kila mtu.
“Mbona siielewi” mzee yule alilalama.
Kiba akaendelea kupayuka, alichanganyikiwa.
“Hebu sema wewe mtoto, kuna nini? Kwa nini husemi.. eboo!” mzee Mikidadi alibweka.
Sauti ya Kiba iliwavuta majirani ndugu na jamaa, muda mfupi tu Kiba alikuwa amezungukwa na watu wengi wa karibu wakitaka aeleze ni kitu gani kilikuwa kikimliza.
“Nitawaeleza...” hatimaye baada ya kupata utulivu alisema.
“Kuna jambo baya mno limetokea”
“Lipi?” mzee mikidadi alidakia kwa kiherehere”
“Jana usiku Amosi alinipigia simu...”
“Eeh!”,
“Akanieleza mama amefariki dunia masaa 24 yaliyopita......” alisema kisha akaweka kituo na kuwatizama wadogo zake akiwemo baba yao mzee Mikidadi.
Sura zao zilionesha mstuko mkubwa kwa taarifa ile, na kauli ile ikatosha kuamsha vilio vingine vikubwa kwenye mji ule.
Watu wa karibu wakawa na kazi moja tu, kuituliza familia ile. Hofu kubwa ya kumpoteza mzee yule kwa presha kutokana na uzito wa taarifa ile uliendelea kuondoa utulivu wa Kiba, hata hivyo hapakuwa na lakufanya zaidi ya kusema ukweli wa kila kitu. Hapakuwa na siri tena.
“Mbaya kuliko vyote...”Kiba akaendelea.
“Amosi alisafiri na maiti ya mama kwenye ndege ya Panasonic Ariline, ambayo taarifa zilizopo ni kwamba ndege hiyo imepotea, na abiria wote wanasadikiwa kupoteza maisha,” taharuki nyingine ikazuka.
Ghafla mzee Mikidadi presha ikampanda, ndani ya muda huohuo alianguka chini na kupoteza fahamu, presha ilikuwa imepanda na kufikia 140/110 mmHg, hatari ya kupoteza maisha yake ikiwa kubwa, watu wakazidi kuchanganyikiwa.
*******
Amosi aliingia ndani ya msitu wenye giza totoro, sauti ya mtu ambaye alimsafirisha kama maiti ndani ya ndege iliendelea kusikika mbele zaidi kadiri alivyokuwa akiendelea kuifuata.
Sauti hiyo ilikuwa ikiomba msaada!!
Japo kulikuwa na giza ndani ya msitu ule, lakini moyo wake haukuwa na hofu, aliendelea kuifuatilia ile sauti bila kuchoka wala kuhofia lolote, akiwa ametembea umbali wa kilometa moja na nusu, mara sauti ile ikanyamaza.
Hatua kama kumi mbele yake, akahisi uwepo wa mtu aliyesimama wima. Mtu huyo alisimama akiwa kampa mgongo, hakujua kama ni mwanamke ama mwanaume kutokana na giza, alichofanya ni kumsogelea.
Kadiri alivyokuwa akimsogelea ndivyo macho yake yalivyokuwa yakilizoea giza, akaendelea kuyakaza macho yake kwa mtu yule aliyekuwa mbele yake.
Akiwa hatua tatu nyuma yake, hatimye alimtambua mtu aliyekuwa amesimama mbele yake, alikuwa ni marehemu mama yake Bi. Greta Shang’wera!.
Bila kutegemea ule ujasiri ukamtoka, akasimama nyuma ya mtu yule, alihisi pate mepesi yakimjaa kinywani na mwili ukamsisimka, ubaridi wa ajabu ukamtambaa mauongoni mwake.
“Mama,” akaita kwa sauti ya chini huku macho yake yakiendelea kuwa makini na mtu huyo.
Kimya. Hakuna alichojibiwa.
Mtu aliyekuwa mbele yake alibaki ameganda, hapakuwa na kiuongo chochote kilichotikisika.
“Mama!!” akaita tena.
Kimya kingine.
Alichofanya ni kusogea mbele ya mtu yule aliyeamini ni mama yake mzazi na kumtizama usoni.
Lahaulaaaa!!!!!!.....Hakuamini kwa kile alichokiona.
Sanamu la kuchonga lililokuwa na mwonekano kama wa mama yake lilikuwa wima limekakamaa huku likionekana kuwa na miaka mingi tangu litengenezwe na kutelekezwa mule mstuni!!.
Amosi alipiga hatua moja kubwa na kurudi nyuma, uso wake ukionekana kuwa na hofu na taharuki kubwa, kamwe hakutegemea kukutana na kioja kile.
Mwonekano wa Kinyago kile kilichochongwa na fundi mwenye kipaji cha hali ya juu kilikuwa hakina tofauti kabisa na haiba ya mama yake mzazi.
“Nini hiki!!...wewe nani..” akasema kwa sauti ya wasiwasi huku akirudi nyuma.
Ule utashi wa kutoamini mambo ya nguvu za giza kwenye maisha yake ukamwishia, kwa mara ya kwanza nafsi yake ikakiri kwamba kulikuwa na mambo ya kichawi yaliyokuwa yanatokea wasaa ule.
Akiwa hatua chache mbele ya kile kinyago katikati ya msitu mkubwa na giza nene. Mara sauti za vicheko zikasika zikitoka kila kona, ilikuwa ni kama vile kulikuwa kuna watu waliokuwa wamemzunguka wakimtizama namna anavyohaha kutokana na kioja alichokiona.
“Hahahaha....hahahah...uwiii..hahaha,” sauti za vicheko zilisikika, Amosi akazidi kuhaha huku na kule, akawa anatupa macho kila mahali ambako vicheko vilisikika akitegemea kuona watu alioamini walikuwa wakimcheka yeye.
Lakini hakuona chochote zaidi ya miti na vichaka vya hapa na pale vilivyokuwa tupu...bila kutegemea Amosi akatokwa na mkojo.
Tendo lile likazidisha vicheko kwa watu wasionekana wala kujulikana. Sauti zao zilikuwa za watu ama viumbe vya rika na jinsia tofuati.
“Ninyi ni akina nani?” Amosi akakoroma kwa kwa sauti iliyoonekana kupaniki huku ikiwa na wasiwasi na mashaka makubwa.
Alipombwatuka kwa sauti ile ya ukali lakini yenye viashiria vya hofu na mashaka, mara vile vicheko vikanyamaza kwa pamoja.
Ukimya ule wa awali ukajirudia, kukawa ni kama vile palikuwa hakuna kilichokuwa kimetokea.
ITAENDELEA
SHEA NA KWENYE MAGROUP MENGINE ILI MAMBO YAWE YENTE.
Tags
simulizi