Katika Makala hii, Mwandishi amechambua kitabu cha Maisha na Desturi za Wanyamwezi, kilichoandikwa na David Yongolo anasema ingawa kuna mabadiliko makubwa katika mila na utamaduni, Wanyamwezi bado wanatunza mila na desturi katika masuala ya posa na ndoa ambapo posa hutolewa kwa kuzingatia madaraja kulingana na kipato na hali ya binti anayeposwa. Daraja la kwanza ni ndoa ya sheria yaani kuposa.
Kabla ya mwingiliano wa tamaduni za kiarabu na kizungu ambao walifika Tanzania na kuleta nguo, shanga na fedha, watu walikuwa wakitumia kulipa mahari yao kwa kutoa majembe, pembe na mifugo. Kijana wa kiume akiwa na makamo ya kutosha kuoa humchagua binti mmoja akamposa; binti akikubali basi hutumwa bibi yake apeleke habari kwa wazazi wake. Wazazi wa binti hudodosa sana kuuliza ukoo wa kijana yule pamoja na mwenendo wake kama ni mwema.
Wakipata habari njema, hukubali kumwoza binti yao. Iliyopo sasa, bwana hupeleka habari kwa wazazi wake kutaka wampe mali ya kuolea. Wazazi wake hutafuta washenga maarufu kama bakombe kwa lugha ya Kinyamwezi. Huchagua washenga wawili wenye ushawishi, busara, hekima na kipaji cha kuzungumza kwa ufasaha na wenye sifa ya uaminifu.
Washenga hao walipewa fedha ambazo kwa sasa ni sawa na Sh 40,000 hadi 60,000 kama kishika uchumba na fedha zilitolewa kulingana na kipato cha familia ya kijana anayetaka kuoa. Kwa Kinyamwezi malipo hayo huitwa kitandula kaya na hutolewa kwa baba ya binti. Baba wa binti huwa na hiari kutoa hesabu ya mahari kadiri atakayo; kwa kawaida ya wote ilikuwa Sh 120 na iwapo baba wa mchumba ni tajiri pengine huhitajiwa mahari ya Sh 200 fedha ambazo kwa sasa ni sawa na Sh milioni moja.
Hata hivyo, sehemu nyingine za Unyamwezi kiasi cha mahari hufuata kiasi cha kishika uchumba, yaani kila shilingi moja iliyopelekwa kwa kishika uchumba ni sawasawa na Sh 10 sawa na Sh laki moja katika mahari. Ina hii ya mahari hutumiwa na baadhi ya Wanyamwezi. Baada ya kutolewa mahari yote yaliyotakiwa, washenga hupewa mbuzi wawili, dume na jike ikiwa wajomba wa binti wapo mbuzi wote huchinjwa pale pale, lakini ikiwa hawapo, huchinjwa dume tu na jike hupelekwa kwa wajomba wa binti.
Mbuzi hao huitwa kwa Kinyamwezi ‘mabugo.’ Baada ya kuchinjwa mbuzi huyo, akina mama wa upande wa bwana harusi hushangilia kwa vigelegele kuashiria kuwa shughuli ya posa imekamilika. Wamalizapo shughuli zote hizo, huagana na kupanga kuonana tena siku harusi itakapofungwa. Siku za harusi zikitimia, mama wa bibi harusi huandaa pombe ya harusi ambapo maharusi hualika rafiki zao.
Bwana harusi hualika vijana wenzake kwenda kwa wakweze wakati wa jioni kufanya maadhimisho ya mkesha wa harusi. Vijana 10 wa rika moja au kukalaga ndalo kwa lugha ya Kinyamwezi huenda kwenye mkesha huo pia bibi harusi hualika marafiki zake wachache. Vijana wa kiume huoshwa miguu yao na huku wakiimbiwa nyimbo za harusi, hukesha usiku kucha bila kulala usingizi na atakayezingia humwagiwa maji usoni.
Alfajiri mapema kabisa, mama wa bibi harusi huwaletea wakwe zake ugali na baada ya kula hurudi makwao kupumzika kisha kurejea tena jioni kwa shughuli ya harusi. Asubuhi siku ya harusi dada wa bwana harusi hutoka kwenda vijijini kuwaalika vijana wenzake. Wakati wa kwenda, huchukua upinde na mshale na kiatu kimoja cha mti. Huenda kwa furaha na shangwe ya vigelegele na nyimbo kadha wa kadha.
Pia bibi harusi hualika wenzake na kuchukua mwiko na ufagio na huku wakiwa wamejipakaa ‘uwanga’ twa ikiwa karibu kwa bwana harusi; hufika huko kwa kusudi la kuipa baraka mali iliyotolewa kuwa mahari kitendo ambapo Kinyamwenzi huita kukapandigila nsabo. Inapotimu saa moja au saa mbili usiku bwana harusi, ndugu, jamaa na marafiki pamoja na wapiga ngoma hukusanyika kisha kwenda kwa bibi harusi. Msafara huo huenda ukiwa unacheza ngoma mpaka nyumbani kwa bibi harusi.
Wakiwasili huzuiwa kuingia katika nyumba hiyo hadi watoe Sh mbili sawa na Sh 20,000 kwa thamani ya fedha ya sasa. Baada ya kuingia huhitajiwa tena kutoa Sh 20,000 za kuangukia upinde ndani ya nyumba. Maana yake humo nyumbani mwa bibiharusi huhitajiwa upinde; hivyo kukatwa vijiti viwili vyenye pande vinavyotundikwa juu; hapo huwekwa upinde pamoja na mshale, kama ishara ya kumtaka mume kushika yaani alama ya mume lazima ashike staha baada ya kuoa.
Baada ya tukio hilo wazee yaani wazazi wa pande zote mbili hucheza ngoma maarufu kwa jina la Ngelo. Ngoma hii huchezwa usiku kucha ambapo wazazi wa pande zote mbili hufanya mashindano na upande unaoonekana kulegalega hunyamazishwa na kutakiwa kulala, kitendo ambacho huchukuliwa kuwa ni aibu. Usiku wa manane shangazi wa bibi harusi hufika akiwa ameambatana na shangazi wa bwana harusi ambapo shangazi wa bibi harusi na wote huelekea kwenye chumba cha maharusi.
Wakifika mlangoni shangazi wa bibi harusi hupiga magoti na kugonga mlango huku akiimba nyimbo kwa kutaja koo za ndugu wa bibi harusi. Baada ya muda hufunguliwa na kupewa Sh 10,000 kisha hutoka na mlango kufungwa. Shangazi wa bwana harusi naye hupiga magoti na kugonga mlango huku akiimba nyimbo kutaja majina ya koo za ndugu wa mume. Hufukuliwa na kuingia ndani ila yeye hapewi kitu. Kitendo hicho ni ishara ya kuwaombea maharusi baraka.
Kunapokucha bwana harusi hupewa mbuzi mmoja ila kama baba wa bibi harusi ana mali nyingi hutoa ng’ombe badala ya mbuzi. Tendo hili kwa Kinyamwezi huitwa kumwingizya mukwilima mwikumbi. Hali kadhalika washenga wa bwana harusi hupewa mbuzi mmoja kama ujira wao. Wazee wa bwana harusi pamoja na wengine hupewa pombe na vyakula kisha hucheza ngoma kuanzia saa nane mchana hadi saa 12 jioni.
Siku ya tatu bibi harusi huogeshwa, kuvalishwa nguo nzuri na kuchanwa au kusukwa nywele zinazopambwa kwa shanga kwa ajili ya kufunga ndoa ambapo Wanyamwezi husema Kwihenda. Wakati huo mama wa bibi harusi huandaa karamu kwa ajili ya wazazi wenzao wa kike, Kinyamwezi huitwa kulya mayeye. Sherehe hiyo huchukua siku nne hadi saba zaidi. Kabla ya bibi harusi kuhamia kwa mumewe, wazazi wake huandaliwa sherehe na wazazi wa bwana harusi.
Baada ya sherehe hiyo hufuata sherehe isiyo kifani ya kuhamisha maharusi kutoka kwa bibi harusi kuelekea kwa bwana harusi. Pia kuna posa inayotolewa kutokana na binti kupata mimba kabla ya kuolewa. Ndoa hiyo maarufu kama Winga Wivulule kwa lugha la Kinyamwezi hufungwa, ikiwa kijana aliyetajwa anakiri kuwa mimba ni yake na yuko tayari kuoa.
Wakati wa kutoa posa kijana huondoka pamoja na dada zake na rafiki zake; humo njiani hukata bua la mtama ambalo hupelekwa kwa wazazi wa mwanamke ambao hulipokea kisha huhesabu pingili zake. Jumla ya pingili za bua hilo ni sawa na jumla ya mahari itakayotolewa baada ya mtoto kuzaliwa. Utaratibu wa harusi ni sawa na ule wa kwanza na mume atahamia kwa wakwe na kukaa huko hadi mkewe atakapojifungua mkewe ndipo mahari hutolewa.
Endapo mtoto atazaliwa kabla mahari haijapatikana, kijana hawezi kuruhusiwa kuondoka na mkewe bali ataendelea kukaa kwa wakwe. Pia kuna ndoa ya kimasikini maarufu kama Wilehya. Kwa mujibu wa ndoa hiyo, kijana asiyekuwa na uwezo humshawishi mchumba wake na kutoroka naye. Kitendo cha kumtorosha msichana hufanyika alfajiri ili wasipate kuonekana na mtu yeyote. Kabla ya kutoweka mwanaume hana budi kuacha Sh 2 sawa na Sh 20,000 kwenye kitanda cha msichana.
Bibi akiona fedha hizo hujua kuwa mjukuu wake ametorokea kwa mwanaume hivyo huzichukua na kumkabidhi baba wa msichana. Baada ya siku mbili baba hutuma watu wawili au watatu kuwafuata watoto wake, yaani binti yake pamoja na kijana aliyemtorosha. Kijana huwapokea na kutoa faini ya Sh 100,000 kisha kuchinja mbuzi mmoja na kuandaa karamu kwa wajumbe waliotumwa.
Hapo huwa amekamilisha mila na thamani ya ndoa hiyo ni sawa na zile nyingine, hata wakizaa watoto ni mali ya mwanamume. Hata hivyo, watu walidharau aina hii ya ndoa isiyokuwa na milolongo ya sherehe. Hata wazazi wa kijana walichekwa kwa kuendekeza umasikini kwa kukubali mtoto wao kuoa kwa njia ya aibu. Ingawa baadhi ya mila na desturi zimetoweka kutokana na mabadiliko ya mfumo wa maisha, Wanyamwezi wanazingatia mila hasa wakati wa kuposa.
Tags
TaboraYetu