*KISIWA CHA MAJINI*
SEHEMU YA KWANZA
Sikuwahi kuona sherehe kubwa ya harusi kama ile niliyoiona katika visiwa vya Ngazija nchini Comoro mwaka mmoja uliopita.
Ilikuwa harusi ya binti wa Rais wa Moroco Yasmini binti Sharif Abdilatif aliyekuwa akolewa na mwana wa mkuu wa majeshi ya ulinzi wa Moroco
Abubakar Mustafa Al- Shiraz aliyekuwa akiishi Ufaransa.
Sisi tulikuwa tumetoka Zanzibar. Mke wa mkuu wa majeshi ya Comoro Kulthum alikuwa Mzanzibari tena Mkojani wa Pemba, ndiye aliyetoa mwaliko kwa ndugu zake walioko Zanzibar.
Zilitolewa kadi kumi za mwaliko kwa watu kumi. Kwa vile na mimi nilikuwa na nasaba na Kulthum nikapata kadi moja na tikiti ya ndege ya kwenda Ngazija.
Wakati ule nilikuwa na umri wa miaka ishirini na mine. Nilikuwa bado kijana na shughuli zangu zilikuwa ni uvuvi. Nilikuwa sijaoa bado lakini nilikuwa katika maandalizi ya kutafuta mchumba.
Ndege tuliyosafiri nayo ilifika Comoro saa kumi jioni. Ndoa ilikuwa inafungwa saa mbili usiku baada ya swala ya isha katika msikiti wa Riadha, msikiti mkuu wa ijumaa nchini humo. Nyumbani kwa bwana harusi kulikuwa kumejaa shamra shamra. Kadhalika nyumbani kwa Rais Sharif Abdulatif nako kulikuwa hakutoshi.
Kulikuwa na hoteli mbili kubwa zilizokodishwa siku ile kwa ajili ya sherehe za harusi. Na kulikuwa na hoteli nyingine kadhaa zilizokodiwa kwa ajili ya wageni walioalikwa kutoka nchi mbalimbali.
Sisi tulifikia katika hoteli ya Zaharani. Jina la hoteli hiyo lilifanana na jina langu. Jina langu ni Zaharani Shazume. Hoteli hiyo ilikuwa jirani na msikiti wa Riadha mahali ambapo ndoa ya Yasmin na Abubakar ingefungwa usiku ule.
Kwa kawaida msikiti wa ijumaa hujaa watu siku za ijumaa lakini siku ile kwa mara ya kwanza ulijaa watu katika swala ya isha.
Kulikuwa na ulinzi mkali wa polisi na maafisa usalama waliokuwa na kazi ya kuhakikisha usalama unakuwepo katika eneo hilo.
Nilijitahidi sana nipate safu ya mbele lakini sikuweza. Safu hiyo ilikuwa imejaa masheikh na maafisa usalama. Nilibahatika kupata safu ya tatu yake.
Baadaya swala ya isha Rais wa Comoro Sharif Abdulatif alitakiwa kutoa idhini ya kumuozesha mwanawe.
Wakati anatoa idhini alipokea simu hapo hapo iliyomtambulisha kuwa binti yake Yasmin alikuwa ameanguka nyumbani na alikuwa akitokwa na povu mdomoni.
Shughuli ya ufungishaji ndoa ikasimama. Hapo hapo Rais Abdulatif na wasaidizi wake pamoja na maafisa usalama walitoka kwenda nyumbani.
Habari iliyopatikana baadaye ilieleza kuwa Yasmini alikuwa ameanguka na kupoteza fahamu huku akitokwa na povu midomoni. Baba yake alipofika na kumuona aliamrisha apelekwe hospitali haraka.
Gari la hospitali lilikuwa limeshafika. Yasmin alipakiwa na kukimbizwa hospitali. Gari hilo la hospitali lilifuatana na gari la maafisa usalama na gari la rais mwenyewe.
Lakini gari alilopakiwa Yasmin likapata ajali kabla ya kufika hospitali. Tairi lake la mbele la upande wa kulia lilipasuka na kusababisha gari hilo kuyumba na kuligonga gari jingine kabla ya kupindukia kwenye mtaro uliokuwa kando ya barabara.
Heka heka ikawa kubwa!. Magari ya maafisa usalama yakasimama. Maafisa hao wakashuka na kukimbilia kutoa msaada. Dereva wa gari la hospitali alipotolewa alikutwa akiwa ameshakufa. Yasmin mwenyewe hakuonekana. Wauguzi wawili waliokuwa naye walikutwa wamezirai. Tukio hilo lilizua taharuki kubwa.
Rais Abdulatif hakuamini macho yake, akawa anauliza kwa ukali “Binti yangu yuko wapi?”
Lakini hakukuwa na aliyejua. Yasmin alikuwa ametoweka ghafla. Kila aliyeshuhudia alishangaa.
Harusi ikavunjika. Badala ya furaha sasa ikawa huzuni. Bwana harusi na mke wa Rais Sharif Abdullatif Bi Kulthum
*SEHEMU YA PILI*
walikuwa wanalia kutokana na muujiza huo.
Usiku ule ule Rais Abdullatif aliita masheikh ikulu na kuwauliza kama walikuwa wanajua kilichomtokea binti yake.
Kila sheikh alisema lake. Wako waliomwambia kuwa binti yake alikuwa amechukuliwa na wachawi. Wako waliomwambia kuwa haikuwa muafaka kwa binti yake kuolewa na Abubakar ndiyo sababu tukio hilo limetokea. Na wako waliomwambia kuwa Yasimin alikuwa amechukuliwa na jini aliyekuwa amemchunuka.
Rais Abdullatif hakujua ashike kauli ya sheikh yupi. Kwa vile lilikuwa limeshamfika alikubaliana na mashikh wote na kuwataka mashikh hao kutumia elimu zao kumrudisha binti yake. Aliahidi mamilioni ya shilingi za ki Comoro kwa sheikh yeyote atakayefanikiwa kumrudisha Yasmin.
Licha ya Rais Abdullatif kusubiri kwa zaidi ya miezi mitatu. Hakukuwa na sheikh yeyote aliyefanikiwa kumrudisha Yasmin! Yasmin akabaki kuwa historia kwani hakupatikana tena. Ulikuwa msiba ambao kila mkazi wa Comro alihisi kuwa hautasahaulika.
Hivi sasa mwaka mmoja umeshapita tangu tukio hilo la kuhuzunisha litokee. Tangu wakati ule sikuwahi tena kurudi Moroco. Nilikuwa Unguja nikiendelea na shughuli zangu za uvuvi.
Sasa siku moja ambayo sitaisahau maishani mwangu tulikuwa kwenye boti letu tukielekea maji makuu kuvua samaki. Ndani ya boti hilo tulikuwa wavuvi saba.
Ilipofika saa nne asubuhi tulikuwa mbali sana. Boti yetu ilipigwa na dharuba kali. Mashine ya boti ikazima ghafla. Tilijaribu kuiwasha lakini boti haikuwaka. Ikawa inakokotwa na maji.
Tulipumzika kidogo kisha tulijaribu kuiwasha tena na tena lakini hatukufanikiwa kuiwasha Mashine ilitugomea kabisa. Hatukujua ilikuwa imepatwa na hitilafu gani.
Hapo ndipo tulipoanza kufadhaika. Hatukuwa na la kufanya, tukawa tunatazamana!.
Tulikuwa tumepelekwa mbali sana kiasi kwamba hatukuweza kuona vyombo vyovyote ambavyo vingeweza kutusaidia. Tukakata tama kabisa.
Injini ya boti inapozima boti inakuwa kwenye hatari ya kupigwa na dharuba na kupinduka. Kama hilo lingetokea ungekuwa ndio mwisho wetu!
Hata hivyo bahari ilikuwa tulivu. Tatizo letu ni kuwa safari yetu haikuwa na mwisho wala muelekeo maalumu. Boti yetu ilikuwa inakokotwa kufuata upepo unakokwenda.
Mpaka jua linakuchwa hatukuwa tumetokea kwenye nchi yoyote wala kisiwa chochote. Ndani ya boti tulikuwa na vyakula vya akiba lakini hakukuwa na yeyote miongoni mwetu aliyesikia njaa.
Usiku ukapita kwa taabu huku tukiendelea kupelekwa. Asubuhi tuliendelea tena na jitihada ya kuiwasha injini lakini injini ilikataa katakata kuwaka. Tukaendelea kukokotwa hadi jioni. Hapo tukatoa vyakula vyetu na maji tukala kidogo tu.
Tulilala tena kwenye boti hadi siku ya tatu na ya nne. Vyakula vikatuishia licha ya kwamba tulikuwa hatuli sana. Tulibakisha maji kidogo tu.
Sasa tukahisi kwamba kama hatutakufa maji tutakufa kwa njaa kwani kwa siku hizo nne tulizokuwa baharini tulikuwa tumekonda.
Alfajiri ya kuamkia siku ya tano ndipo tulipotokea kwenye kisiwa. Sote tukashukuru ingawa hatukujua kilikuwa kisiwa gani na kilikuwa katika eneo gani.
Kilikuwa kisiwa kikubwa ingawa hakikuwa kikubwa sana. Kwa vile tulikitokea wakati wa usiku hatukukiona kwa sababu ya giza. Tulikiona kulipoanza kucha. Wakati tunakiona tulikuwa tumekikaribia sana. Sote tukapata furaha na matumaini ya kuokoka.
Mawimbi yaliendelea kutusukuma kidogodogo na kutufikisha kwenye maji madogo kabisa.
Suala kwamba kisiwa hicho kilikuwa kisiwa gani na kipo wapi halikuwa na umuhimu kwetu. Kilichokuwa muhimu ni kuwa tumefika mahali ambapo tungeweza kuyasalimisha maisha yetu nap engine kupata msaada wa kutuwezesha kurudi kwetu.
Tulishusha nanga na kushuka kwenye boti. Maji yalikuwa yakitufikia kwenye magoti. Tukaliacha boti na kutembea kwa miguu kwa kuyasukuma maji hadi tukafika ufukweni mwa bahari. Mahali tulipotokea hapakuwa na muinuko mkubwa. Tukapanda kwenye nchi kavu na kuanza kutembea kwemye vichaka huku tukiangaza macho huku na huku.
Kulikuwa na kunguru wengi waliokuwa wakiruka ruka kwenye miti. Jinsi walivyokuwa wakipiga kelele walikuwa kama wanaotukaribisha katika kisiwa hicho kilichokuwa kimya.
Tukaendelea kutembea tukiingia ndani zaidi ya kisiwa. Mtarajio yetu yalikuwa kupata mji au kijiji kilichokuwa kinakaa watu ili tuweze kusaidiwa.
Baada ya mwendo wa kama nusu saa tulianza kuona vibanda vilivyokuwa vimebomoka. Tukapata matumaini kuwa kulikuwa na watu waliokuwa wanaishi katika kisiwa hicho. Pia tulikuta visima viwili vya maji ambavyo vilikuwa vimekauka.
Wakati tunaendelea kwenda ghafla tuliona tumetokea kwenye barabara pana ya changarawe. Tukaifuata ile barabara mpaka tukatokea katikati ya mji. Ulikuwa mji mzuri uliokuwa na barabara na majumba. Lakini nyumba zote zilikuwa zimechakaa na kubomoka. Baadhi yake zilionekana kama mahame.
Jambo ambalo lilitushangaza ni kuwa hatukuona mtu hata mmoja. Mji wote ulikuwa kimya kabisa. Tulikuwa ni sisi peke yetu tu. Tulikatiza mtaa hadi mtaa kutafuta wenyeji wa kisiwa hicho lakini hatukuona mtu.
Udadisi ukatufanya tuanze kuingia katika zile nyumba. Tuliingia katika
nyumba ya kwanza. Tukakuta vitu vya ndani vilivyochakaa na kukongoroka. Vilikuwa kama vitu vya zamani visivyotumika tena. Katika kutafiti tafiti tulishituka tulipokuta mafumvu na mifupa ya binaadamu. Kuna iliyokuwa imelala kwenye kitanda na mengine ilisambaa ovyo.
Tukatoka haraka katika nyumba ile na kuingia katika nyumba nyingine, nako tulikuta vitu mbalimbali vya ndani ya nyumba vilivyokuwa vimechakaa na mifupa ya binaadamu.
Tukawa tunatazamana kwa hofu. Kila mmoja wetu alikuwa akijiuliza moyoni mwake, kulikoni? Lakini hatukupata jibu.
Katika mitaa mengine tulikuta mafuvu na mifupa ya binaadamu ikiwa barazani mwa nyumba na kando kando ya barabara. Tulivyozidi tena kwenda mbele tulikuta mifupa ya mikono nay a miguu ya binaadamu ikining’nia kwenye miti. Tukawa tunazidi kuitazama ile mifupa huku tunazidi kwenda.
Ghafla tukatokea kwenye jumba moja kubwa. Jumba hilo ndilo lililokuwa kubwa na zuri kuliko jumba lolote katika kisiwa hicho.
Mbele ya jumba hilo kulikuwa na bustani ya maua na miti ya vivuli. Kutokana na uzuri wa jumba hilo tukaona tuingie ndani ili tuangalie lilivyo.
Tulipoingia tu pua zetu zilikaribishwa na harufu nzuri ya manukato yaliyokuwa yananukia humo ndani. Tulitembea katika sakafu ya marumaru iliyonakishiwa maua ya kupendeza.
Tulikuwa tumeingia katika ukumbi mpana uliokuwa na madirisha na mapazia ya hariri. Tulikuta meza, viti na makabati. Zilikuwa fanicha za kifahari sana.
Baada ya kuupita ukumbi huo tulitokea katika kumbi nyingine ndogondogo zilizokuwa na vyumba vipana. Tukawa tunaingia kila chumba kuchunguza.
Katika chumba cha kwanza tulikuta kitanda kilichotandikwa vizurii. Pia tulikuta makabati ya vioo yaliyokuwa yanapendeza.
SEHEMU YA TATU
“Inaelekea kuna watu wanaoishi ndani ya jumba hili” Mwenzetu mmoja akasema.
“Lakini mbona hatuwaoni hao watu?” Mwingine akauliza.
“Ndiyo hatuelewi sasa” aliyesema mwanzo akamjibu.
Tulitoka katika kile chumba tukaingia katika chumba kingine. Pia tulikuta kitanda na makabati. Tukawa tunatazamana kwa mshangao. Kutoka hapo tulichangukana. Kila mmoja akawa anafungua chumba alichotaka na kuangalia ndani.
Mimi niliingia katika vyumba viwili. Nilipoingia chumba cha tatu nilishituka nilipomuona msichana mzuri amelala kitandani. Alikuwa amelala usingizi kabisa huku amejifinika shuka kuanzia miguuni hadi shingoni. Uso wake uliokuwa wazi ulikuwa umeelekea upande wangu.
Nilipomuona nilisita kwenye mlango na kujiuliza msichana huyo ni nani na kwanini alikuwa peke yake katika jumba hilo.
Baada ya kusita kidogo niliingia ndani. Nilikuwa nataka kuhakikisha kama alikuwa hai kweli au amekufa.
Nilipofika karibu yake, msichana huyo alifumbua macho ghafla. Akashituka aliponiona.
“Wewe nani?” akaniuliza kwa mshangao akitumia lugha ya kingazija ambayo nilikuwa siijui vizuri. Lakini nilimjibu kwa Kiswahili.
“Mimi ni mgeni katika kisiwa hiki na katika jumba hili, je wewe ni nani?”
Alikuwa anajua Kiswahili. Akanijibu kwa Kiswahili cha kipemba.
“Miye ni Yasmin, binti wa Rais Shariff Abdilatif wa Comoro!”
Nilishituka sana aliponiambia yeye ni binti wa Sharif Abdulatif wa Comoro.
Papo hapo nikakumbuka ile harusi iliyovunjika kati ya binti wa rais wa Comoro na mwana wa mkuu wa majeshi ya ulinzi nchini humo.
Mimi nilikuwa mmoja wa waalikwa kutoka Zanzibar na nikashuhudia maajabu. Yasmin alitoweka katika mazingira ya kutatanisha baada ya gari iliyokuwa inampeleka hospitali kupasuka tairi na kuingia kwenyenye mtaro. Yasmin alikuwa anakimbizwa hospitali baada ya kuanguka ghafla wakati baba yake Rais Sharif Abdulatif anataka kutoa idhini ya kumuozesha binti yake.
Baada ya kutoweka ghafla kwenye gari, Yasmin hakupatikana tena na sasa mwaka ulikuwa umeshapita.
Ingawa sikuwahi kuonana naye uso kwa uso lakini niliona picha zake katika magazeti na televisheni wakati habari zake zilipokuwa zinaandikwa na kutangazwa.
Alikuwa ndiye Yasmin kweli binti wa Rais Sharif Abdulatif wa Comoro.
Kwa kweli tukio la kumkuta ndani ya jumba hilo na katika kisiwa kile kisicho na watu, mbali ya kunishitua, liliniongezea hofu mara dufu.
“Wewe ni binti wa Rais wa Comoro” nikamuuliza kwa mshangao.
Huku akinyanyuka kwenye kitanda na kuketi msichana huyo alinijibu.
“Ndiye mimi. Rais Sharif Abdulatif ni baba yangu”
Nikiwa kwenye mshangao niliendelea kumtazama msichana huyo bila kummaliza. Alikuwa amevaa shumizi inayoonya. Alipoketi alijifunga ile shuka kwenye mwili wake kama mtu aliyekuwa anaona baridi. Lakini nilijua alikuwa anajisitiri kwa sababu sumizi aliyovaa ilikuwa inaonya.
Kwa tamaduni za kiislamu na za kule Comoro mwanamke hatakiwi kuonekana mwili wake pamoja na kichwa chake.
Lakini Yasmin kwa sababu ya kutaharuki alisahau kujifinika kichwa. Nywele zake za mawimbi zilizokuwa ndefu zilikuwa zimeshuka na kumfikia mabegani.
“Yasmin umefikaje huku?” nikamuuliza.
Yasmin akanitazama. Macho yake makubwa yenye mboni za rangi ya kahawia yalinifanya nikiri kimoyomoyo kuwa Yasmin alikuwa mzuri.
Badala ya Yasmin kunijibu, na yeye akaniuliza.
“Kwani wewe umefikaje hapa?”
“Mimi siko peke yangu, nina wenzangu na tumefika hapa kwa bahati mbaya. Sisi ni wavuvi kutoka Zanzibar. Chombo chetu kilipigwa na dharuba kikapata hitilafu. Kwa siku nne kilikuwa kinaelea kwenye maji, hatujui tunakokwenda. Leo siku ya tano ndio tumetokea kwenye kisiwa hiki”
“Huko ulikopita hadi umetokea hapa, umeona nini?”
“Tumekuta nyumba hazina watu. Pia tumekuta mafuvu na mifupa ya watu kila mahali”
“Basin a nyinyi ndio mtakuwa hivyo hivyo, hamtapona”
Yale maneno yalinitisha na kunifadhaisha.
“Yasmini kwanini unaniambia hivyo. Mimi ni ndugu yako wa Zanzibar. Hata katika harusi yako na mwana wa mkuu wa majeshi ya ulinzi wa Moroco nilialikwa na nilikuja Comoro lakini wewe ulitoweka katika mazingira ya ajabu. Na leo ndio nakuona hapa” nikamwambia Yasmin kwa hofu.
“Nashukuru kwamba leo nimetembelewa na ndugu yangu wa Zanzibar na nashukuru kwamba umenijua lakini naona uchungu kuwa nitayashuhudia mauti yako muda si mrefu”
>Kwanini unaniambia hivyo Yasmin?. Niambie”
Yasmin bdala ya kunijibu aliangua kilio.
Wenzangu mmoja mmoja wakaanza kuingia mle chumbani na kushangaa kumuona yule msichana akilia.
“Je ni nani huyu?” Mmoja wa wale wenzangu akaniuliza wakati wenzetu wengine walikuwa wamepigwa na butwaa.
“Ni msichana nimemkuta amelala humu chumbani. Nilipoingia alizinduka na kuniambia anaitwa Yasmin. Ni binti wa Rais wa Comoro” nikawaeleza.
“Ni binti wa Rais wa Comoro?” Baadhi ya wenzangu wakaniuliza kwa mshangao. Walidhani labda nilikosea kusema.
SEHEMU YA NNE
“Ndiyo, mwenyewe ameniambia hivyo na mimi pia namfahamu. Nilihudhuria katika harusi yake nchini Comoro mwaka uliopita.
“Si ilisemekana kuwa yule binti alitoweka?” Mmoja wa wenzangu akauliza.
“Ni kweli. Mimi pia nimeshangaa kumkuta katika kisiwa hiki, tena akiwa peke yake. Na amenieleza kitu cha kutisha”
“Kitu gani?”
“Mh! Ameniambia anaona uchungu kuwa atayashuhudia mauti yetu muda si mrefu!”
Wenzangu wote wakashituka, ndipo nilipojua kuwa hakuna mtu anayependa kufa.
“Kwanini amekwambia hivyo?” Sautu za kuuliza zilisikika kutoka kwa wenzangu.
“Ndio nilikuwa namuuliza, naona analia”
“Asilie, atueleze ili tujue…”
“Usilie dada yangu, nyamaza utueleze ili tujue jinsi ya kujihami” nikamwambia msichan huyo.
“Pia atueleze jinsi alivyofika katika kisiwa hiki cha ajabu” Mtu mwingine akasema.
Yasmin akajifuta machozi yake kwa shuka aliyokuwa amejifunga kisha akainua uso wake na kututazama. Sasa macho yake yalikuwa mekundu na uso wake ulikuwa umeiva.
“Wiki moja kabla ya harusi yangu huko Comoro nilikiota hiki kisiwa. Nikamuota kichaa mmoja akiniambia siku zako zimekaribia za kuja kukaa katika kisiwa hiki” Yasmin akaanza kutueleza. Tukawa tunamsikiliza kwa makini.
Akaendelea. “Nikamwambia yule kichaa, siwezi kuja kukaa hapa, mimi natarajia kufunga ndoa hivi karibuni. Nitakwenda kukaa Ufaransa si hapa
“Yule kichaa akaniambia, ndoa yangu nitafunga na yeye kwani yeye alinichunuka tangu nilipokuwa ninasoma na hatakubali niolewe na mtu mwingine.
“Nilipoamka asubuhi nilipuuza ile ndoto. Sikumuelezea mtu yeyote na kwa kweli nilifanya kosa kuipuuza, pengine nisingekuwa hapa leo hii. Yaani mpaka leo hii ninajuta”
Msichana huyo akaendelea kutuelea. “Ile siku ya harusi yangu ilipofika saa mbili usiku niliona kizunguzungu. Macho yangu yakafunga kiza. Nikaona kama moyo wangu unanisokota na ghafla nikapiga ukelele na kuanguka chini. Baada ya hapo sikujijua tena
“Nilizinduka asubuhi na kujikuta nomo ndani ya jumba hili katika kisiwa hiki. Mbele yangu nikamuona yule kichaa niliyemuota akiniambia kuwa nitakuja kukaa hapa”
“Yule mtu niliyemuota hakuwa binaadamu bali alikuwa jinni aliyekuwa amenichunuka. Siku ile nilipomuota nilimuona katika sura ya kibinaadamu kichaa lakini nilipozinduka nikiwa katika jumba hili alikuwa katika sura na umbile la kijini” Yasmin aliendelea kutueleza. Kisa chake kilikuwa kimetushangaza na kutuogopesha.
Akaendelea. “Huyo jinni aliponiona nimeshituka aliniambia Yasmin usiogope umeshafika nyumbani kwako, mimi ndio nitakuwa mume wako. Utaishi katika jumba hili na hutarudi tena kwenu.
“Akaniambia kwamba yeye ni jini wa ukoo wa kisubiani makata. Jina lake ni Harishi wa Harishn. Chakula chake ni damu ya binaadamu. Ameniambia wazi kuwa yeye ni jini mbaya aliyelaaniwa na ameshaua watu wengi.
“Akanihadithia kisa cha kisiwa hiki. Aliniambia kilikuwa kinaishi watu zamani na mfalme wao alikuwa akiishi katika jumba hili. Lakini yeye harishi ndiye aliyewaua mmoja mmoja kwa kuwafyonza damu hadi kukimaliza kisiwa chote.
“Watu wachache waliobaki waliondoka na kikiacha kisiwa kikiwa kitupu. Ndiyo sababu mlikuta magofu matupu na mifupa ya watu waliouliwa na Harishi. Siku za mwanzo mwannzo mji huu ulikuwa haukaliki kwa harufu zilizotokana na maiti za watu. Kunguru wa Zanzibar walihamia hapa kujipatia riziki zao. Sasa hivi iliyobaki ni mifupa mitupu.
“Kwa sasa kisiwa hiki kinajulikana kama kisiwa cha mauti. Wavuvi ambao hawajui habari za kisiwa hiki wakifika hapa kushona nyavu zao Harishi aliwaua mmoja mmoja kwa kuwafyonza damu”
Maelezo ya Yasmin yalitufanya tutazamane mara kwa mara huku nyuso zetu zikiwa zimepigwa na butwaa. Hatukuwahi kusikia kisa cha ajabu kama kile.
“Mimi nilikuwa nikilia peke yangu hadi sasa silii tena. Ni kama nimeshazoea kuishi na yule jinni” Yasmin aliendelea kutueleza.
“Kila wiki ankuja mara moja. Au kama nina dharura ninamuita, anakuja. Humu ndani mna kila kitu. Mna kila aina ya vyakula. Huwa najipikia mwenyewe chakula ninachotaka. Vyakula vikipungua ananilete vingine.
“Pia ananiletea nguo za kifalme pamoja na dhahabu. Huwa anaiba nguo hizo katika kasri za wafalme na marais. Kila kitu ninachotaka ananiletea lakini hainisaidii. Maisha ya upweke yananifanya nijione kama nimo ndani ya kaburi”
Wakati Yasmin anatuhadithia kile kisa, nilimuuliza. “Umetuambia huyo jini anafyonza damu za watu na kuwaua, je wewe utaendelea kuwa salama kweli”
“Mimi nimeshakuwa mke wake. Ameniambia damu yangu ni haramu kwake. Hawezi kuniua ila hatanirudisha tena kwetu. Nitaendelea kuishi hapa hadi mauti yanikute” Yasmin alituambia.
Kwa kweli hayakuwa maneno ya kuogopesha tu bali pia yalikuwa yanasikitisha sana.
Maisha ya Yasmin yalikuwa yanasikitisha. Alionesha wazi kukata tama na pia niliona kwa vyovyote itakavyokuwa maish yake yatakuwa mafupi.
“Kwa hiyo sisi hatutapona?” Mwenzetu mmoja akamuuliza Yasmin
“Sipendi niwafiche, nawaeleza ukweli ili mujue kuwasaa zenu zimekaribia sana”
“Je kama tutaondoka ndani ya jumba hili na kwenda kujificha mahali pengine?”
“Mtajificha wapi ambapo hafiki. Kisiwa chote hiki amekimiliki yeye. Halafu yeye ni jini, lazima atawagundua tu”
“Sisi tuko watu saba. Kweli ataweza kutuua sisi sote kwa pamoja?”
“Nyinyi atawaua mmoaja mmoja. Leo akiua mmoja, kesho anarudi tena kuua mwingine hadi mtamalizika nyote. Akishaua mtu anamtupa nje aliwe na kunguru”
Msichana akatikisa kichwa peke yake kabla ya kuendelea.
“Halafu hataki kuona mtu humu ndani. Wivu wake ni mkali sana. Siku nyingine anakuja na hasira, anasema anasikia harufu ya mtu humu ndani, basi hunipiga hadi nazimia kisha huenda zake”
Kila mmoja wetu aliguna na kumtazama mwenzake.
“Unadhani atakuja lini tena?” nikamuuliza.
SEHEMU YA TANO
“Alinipa chupa. Mnaiona ile chupa iliyopo juu ya kabati? Chupa ile iko wazi. Kifiniko chake kipo pembeni. Ameniambia nisiifunge. Anapotaka kuja ile chupa inajaa moshi halafu inavuma. Ule moshi ukishajaa unatoka kwenye mdomo wa ile chupa na kuundaumbile la jinni halafu anakuwa jinni kabisa.
“Sasa nikitaka kumuita nachukua ile chupa naiweka naiweka karibu na mdomo wangu kisha nataja jina lake mara tatu, hazitapita dakika mbili chupa itajaa moshi. Moshi ule utatoka kwenye mdomo wa chupa na kugeuka Harishi”
“Sasa kama anakuja kila wiki tutapata muda wa kuishi na pengine tunaweza kupata msaada kwani tutakwenda kukaa fukweni kusubiri vyombo vinavyopita” nikamwambia Yasmin
“Jaribuni hahati yenu. Nawaombe Mungu awasalimishe” Yasmin alituambia kwa ungonge.
Nikawambia wenzangu. “Jamani maneno mmeyasikia. Hapa hapakaliki”
“Sasa tuondoke” Mtu mmoja akauliza.
“Inabidi tuondoke tusalimishe maisha yetu”
“Sasa tutakwenda wapi?” Mwingine akauliza.
“Twende ufukweni tuangalie vyombo vinavyopita, tunaweza kupata msaada”
“Sasa huyu msichana naye
tumchukue?” Mtu mwingine naye akauliza.
“Itakuwa ni jambo zuri tukimchukua kama mwenyewe atakubali” nikawambia wenzangu kish nikamtazama Yasmin.
“Bibie unaonaje kama tutakuchukua ili tukunusuru?” nikamuuliza yasmin.
“Kunichukua mimi hakutakuwa nusura kwangu wala kwenu kwa sababu mpaka sasa hamna uhakika wa usalama wenu hata kama mtakwenda ufukweni mwa bahari kusuiri vyombo vinavyopita” Yasmin akatuambia.
“Kwanini unatuambia hivyo?” nikamuuliza.
“Kwa sababu Harishi anaweza kututoke hapa hapa na kutuua sote kwa hasira’
Sote tukagunana kutazamana. Yasmin aliendelea kutuambia.
“kwanza akija hapa nyumbani hata kama mtakuwa mmeshaondoka atasema anasikia harufu ya binaadamu na atataka kujua ni nani aliyeingia humu na itakuwa ni balaa kubwa”
“Sasa unatushauri nini?” nikamuuliza Yasmin katika hali ya kukata tama.
“Nawashauri muondoke ndani ya jumba hili. Mwende popote mtakapoona mtaweza kujiokoa. Mimi niacheni hapa hapa”
“Sawa. Basi sisi tunondoka”
Yule msichana kwa kuonesha wema na ukarimu alituambia tumpishe mle chumbani avae nguo. Tukatoka ukumbini. Yasmin alipovaa alitoka akaenda jikoni. Akachukua vyakula na kututilia ndani ya mfuko.
“Sasa nendeni, msikae karibu kabisa” akatuambia.
Tukamuaga na kutoka. Tukaanza kutembea haraka haraka kwa kufuata ile njia tuliokwendea.
Kisiwa kilikuwa kimya na kilichokuwa kinatisha. Kelele zilizosikika zilikuwa ni za kunguru waliokuwa wakilialia na kurukaruka kwenye miti kama waliokuwa wakiambizana “Hao! Hao! Hao!”
Tulikuwa tukiangalia huku na huku kwa hofu ya kutokewa na Harishi. Kuwa na silaha katika mazingira yale ilikuwa muhimu. Mimi nilikuwa na sime niliyokuwa nimeichomeka kiunoni. Wenzangu wawili walikuwa na mapanga. Wenzetu wengine walikuwa mikono mitupu.
Kwa sababu ya hofu iliyosababishwa na kelele za wale kunguru nilitoa sime yangu na kuishika mkononi. Sasa nikawa tayari kukabiliana na chochote kitakachotokea.
Mpaka tunatokea kule ufukweni mwa bahari tulizungukazunguka sana kwani tulikuwa tunapotea njia mara kwa mara. Kulikuwa na mti mkubwa ulioota kando ya bahari. Tukakaa chini ya ule mti.
Tulitoa vyakula tulivyopewa na Yasmin na kuanza kula. Vilikuwa vhyakula vizuri vikiwa mchanganyiko wa mikate ya mayai, keki, sambusa na biriani.
Wakati tunakula mawazo yangu yalikuwa kwa yule msichana. Kwa kweli nilimuhurumia sana kwa kuishi maisha ya peke yake katika kisiwa kile cha kutisha. Laiti ningekuwa na uwezo wa kumuokoa ningemuokoa lakini ndio hivyo hatukuwa na uwezo na bado sisi wenyewe pia hatukuwa na uhakika wa maisha yetu.
Hata hivyo nilimsifu kwa kuwa na moyo wa kijasiri na wa kiume kwani asingeweza kuishi na kuendelea kuwa hai hadi leo wakati yuko kwenye jinamizi la mauti. Kuishi na jini anayeua watu peke yake lilikuwa ni jinamizi la mauti mbali ya kule kuishi peke yake katika kisiwa kile kinachotisha!.
Nikajiambia kama chombo chetu kingekuwa kizima tungeondoka naye hata kama angekataa.
Baada ya kula kile chakula tulipata akili tukaanza kujadiliana.
“Sasa tufanye nini jamani?” Mwenzetu mmoja akauliza.
“Tuijaribu tena ile boti, inaweza kukubali” nikatoa wazo ambalo lilikubaliwa na wenzangu.
Tukaenda kwenye chombo chetu tukajaribu kukiwasha lakini chombo hakikuwaka. Kila mmoja wetu alijaribu kukiwasha kwa mkono wake. Hakukuwa na yeyote aliyefanikiwa.
Tukaamua kujitia ufundi kuanza kuichokoresha mashine ya boti. Kila mmoja alitia ufundi wake lakini pia hatukufanikiwa. Mimi nilijitupa chini kwenye mchanga nikawaacha wenzangu wakiendelea kushindana nayo.
Yalipita karibu masaa mawili. Hatimaye niliona wenzangu mmoja mmoja akiondoka kwenye boti na kutafuta mahali pa kukaa. Wote walikuwa wamekata tama kama nilivyokata mimi.
Mawazo yangu yakarudi kwa Harishi. Kama alivyotwambia Yasmin Harishi anaweza kutokea na kutumaliza kama alivyowamaliza watu wa kisiwa hicho.
Kwa muda sote tulikuwa kimya. Kila mmoja alikuwa akiwaza lake. Tulipokitokea kisiwa kile tuliona tuliona tumeokoka tukafurahi. Kumbe tumeepuka kufa maji, tumekwenda kwa muuaji mwingine anayefyonza damu.
Tuliendelea kukaa pale tukiangalia baharini hadi jua likaanza kuchwa. Hatukuona chombo chochote kilichopita karibu. Tulichokiona ni mawingu yaliyoonekana kama yanazama upeoni mwa macho yetu.
Wakati giza linaingia hatukujua tungejisitiri mahali gani usiku huo kwani kwa vyovyote vile tusingeweza kuupitisha usiku mahali hapo kutokana na baridi. Pia usalama wetu ulikuwa mdogo. Lolote lingeweza kutokea wakati wa usiku. Kuna vitu kama majoka na wanyama wakali ambao hujificha wakati wa mchana na kujitokeza wakati wa usiku.
Baada ya kuufikiria usalama wetu tulishauriana turudi tena katika lile jumba la yule msichana. Kuna waliopinga wakataka tupande juu ya mti ule tuupitishe usiku.
Lakini upepo mkali ulioanza kuvuma pamoja na ngurumo za radi ndio uliofanya tukubaliane kwa pamoja kurudi katika lile jumba kwani tulijua muda si mrefu mvua kali ingenyesha na kututosa.
SEHEMU YA SITA
Si tu tuliona tungeweza kujisitiri katika lile jumba pia tungeweza kufanya uchunguzi wetu na kujua kama huyo Harishi tuliyeambiwa ameshakuja au bado.
Tukaanza tena safari ya kurudi katika lile jumba. Mvua ilikuwa imeshaanza kunyesha kidogo dogo huku upepo mkali ukiendelea kuvuma pamoja na radi.
Tulitembea kwa mashaka mashaka tukikwepa kuwa karibu na miti kwa kuhofia kupigwa na radi.
Kulikuwa giza na hatukuweza kupata mwanga ila pale radi ilipopiga ndipo tulipoona tulikokuwa tunaelekea. Kutokana na giza hilo tulihangaika katika pori kwa muda kabla ya kufanikiwa kutokea katikati ya ule mji uliohamwa.
Tulikuwa tunaendelea kutota na mvua na huku tukiendelea kwenda. Tukawa tunalitafuta lile jumba. Tulidhani tusingeliona kwa urahisi lakini lilikuwa linawaka taa. Tukaliona kwa mbali. Tukalifuata.
Kwanza tulinyata kwenye madirisha. Tukawa tunachungulia na kutega masikio kusikiliza. Hatukusikia sauti yoyote. Kulikuwa kimya. Ndipo tukaamua tuingie.
Tukaingia ndani ya jumba hilo lililokuwa linawaka taa ndani. Lakini tuliingia kwa kunyata ili hatua zetu zisisikike. Jumba hilo lilikuwa kimya kama vile tulivyoliacha mchana.
Kila tulipofikia kona tulichungulia kwanza kabla ya kuendelea kwenda. Tukaenda hadi katika kile chumba tulichomkuta Yasmin binti wa rais wa Comoro.
Mlango wa chumba hicho ulikuwa umefungwa. Tukaenda jikoni tukapekua pekua na kukuta vyakula vilivyokuwa vimebaki. Tukakaa chini na kuanza kula kwani njaa ilikuwa inatuuma na hatukutarajia kupata chakula usiku huo.
Baada ya kula tulitoka humo jikoni tukaamua kutafuta mahali pa kulala ndani ya jumba hilo hilo. Karibu vyumba vyote tulivyofungua ukiacha kile cha Yasmin vilikuwa na vitanda. Kila kitanda kilikuwa na chumba kimoja kilichowezesha kulala watu wawili.
Tukaamua tulale kila chumba watu wawili. Tulikuwa tupo saba. Mmoja wetu akaamua kuchukua godoro kutoka chumba kingine na kuliingiza katika chumba tulichokuwemo mimi na mwenzangu. Akalilaza chini. Kwa vile yeye hakuwa na mwenzake wa kulala naye na asingeweza kulala peke yake, ndipo aliamua kuja kulala na sisi.
Mvua likuwa inaendelea kunyesha na radi ilikuwa inapiga. Kama tungekuwa tuko kwenye boti yetu tungejuta.
Mimi nilisoma aya zangu kisha nikajifunika shuka. Naamini na wenzangu kila mmoja alisoma dua yake kabla ya kulala.
Tulikuwa tumepanga tuamke alfajiri tutoke kwenye hilo jumba bila hata kumshitua Yasmin.
Hata hivyo usingizi hatukuupata kirahisi kwa sababu ya hofu. Tuliendelea kukaa macho hadi usiku mwingi. Wenzangu walipata usingizi lakini mimi sikulala.
Kulikuwa na wakati usingizi ulikuwa umeanza kunijia nikaamshwa na mwenzetu aliyekuwa amelala chini.
“Unasemaje?” nikamuuliza.
“Mkojo umenibana nisindikize chooni” akaniambia.
Vyoo vilikuwa nje.
Nikatenga shuka na kunyanyuka. Mwenzangu niliyelala naye alikuwa anakoroma.
“Twende!” nikamwambia yule aliyeniamsha.
Tukatoka pamoja. Vyoo vilikuwa ukumbini karibu na mlango wa kutokea.
Tulikwenda hadi karibu na milango ya vyoo. Kulikuwa na vyoo vinne. Mwenzangu alishaingia choo kimojawapo. Mimi nikasikia hatua za mtu nyuma yangu nikageuka. Alikuwa ni yule mwenzetu tuliyemuacha amelala, naye aliamka na kutufuata.
Alikuwa anakuja harakaharaka kutukimbizia. Nilijua ni sababu ya uoga. Wakati huo huo nikaona mlango wa chumba cha Yasmin unafunguliwa. Nikaingia chooni haraka ili niweze kumchungulia aliyekuwa anatoka bila yeye kuniona.
Ghafla nikaliona jitu likitoka katika kile chumba. Lilikuwa jitu la kutisha lililojifunga kilemba kikubwa. Lilikuwa na msitu wa nywele zilizotokeza nje ya kilemba chake. Lilivaa kanzu nyeupe iliyochafuka kwa madoa ya damu na iliyokatwa mikono.
Mikono yake minene iliyoota manyoya marefu ilikuwa imeshupaa. Mkono mmoja alishika upanga mrefu.
Uso wake ulikuwa na ndevu nyingi na sharafa kiasi kwamba sura yake haikuweza kutambulika. Kilichoonekana kwenye uso wake ni pua yake iliyofura kamailiyopachikwa na macho yake makubwa yenye makengeza.
Miguu yake ilikuwa pekupeku. Alikuwa na vidole virefu na vinene vya miguu, tena vilikuwa na kucha ndefu kama kucha za mnyama.
Hapo hapo nikahisi kwamba yule alikuwa ndiye Harushi. Alikuwa ametufuma vizuri ndani ya hilo jumba.
Uso wake ukiwa na hasira kali, macho yake ya makengeza yalielekea kwa yule mwenzetu aliyekuwa anatufuata. Alikuwa ameshafika karibu yake kiasi kwamba jitu hilo lilinyoosha mkono wake wa kushoto na kumshika shati.
Tags
simulizi