Unahitaji Kuamua Vyema...
______________________
Hivi unafahamu kwamba hapo ulipo pamoja na hivyo ulivyo leo ni matokeo ya maamuzi yako uliyofanya jana?
Unatakiwa kujua kwamba Kwa chochote kile kinachotokea maishani mwako kinaendeshwa na maamuzi. Hivyo basi endapo hakutakuwa na maamuzi yatakayofanywa hakuna chochote kile kitakachotokea...
Na ndiyo maana kanuni ya kichocheo na matokeo inasema kwamba " kila matokeo yana kichocheo chake"
Hii inamaanisha kwamba maamuzi utakayoyafanya ndiyo yatakuwa kama kichocheo, halafu kile utakachokipata baada ya kufanya maamuzi ndicho kitakuwa matokeo yenyewe!
Mbali na hilo huna budi kufahamu kwamba, vile utakavyokuwa kesho itategemeana na maamuzi utakayoyafanya leo!
Kutokana na ukweli huo ninawiwa kukufamisha kwamba, ni muhimu kufanya maamuzi ya busara leo hii, ili kesho yako ije ikushukuru kwa maamuzi uliyoyafanya jana!
Vilevile unatakiwa kujua kwamba ukishindwa kufanya maamuzi sahihi utaishia kulaumu. Mbali na kulaumu sana unapaswa kujua kwamba hakuna utakachobadili, kwani hakuna kiwango cha lawama ambacho kitabadlili kilichotokea!
Kutokana na ukweli huo, huna budi kutafakari kwa umakini kabla hujafanya maamuzi yoyote yale...
Sambamba na hilo kitu kimoja unachopaswa kuondoka hapa nacho hapa ni kwamba wakati unafanya maamuzi unakuwa huru, lakini ukishaamua maamuzi hayo yanakufunga nawe unageuka na kuwa mfungwa kutokana na maamuzi yako mwenyewe!
Hata hivyo kwa mujibu wa Daren Hardy katika kitabu chake kiitwacho the compound effect yeye anasema kwamba "sote huzaliwa tukiwa sawa hapa duniani, yaani tukiwa uchi, wajinga, na wenye kuogopa lakini tunaishia kuwa watu tofauti kutokana na aina ya maamuzi tunayoyafanya!
Mpenzi msomaji unatakiwa kujifunza kwamba maamuzi yetu yanaweza kuwa rafiki wetu mzuri au adui mbaya wa kutupwa!
Chochote kile kilichopo maishani mwako (kibaya/kizuri) jua wewe mwenyewe umekileta kupitia maamuzi Yako!
Sambamba na hilo unatakiwa kujua kwamba hata kutokuamua ni kuamua pia, kwani kupitia kutokuamua kwako utapata matokeo fulani!
Watu wengi hujikuta wanapatwa na kigugumizi linapokuja suala la kufanya maamuzi kuhusu maisha yao pamoja kesho zao! Hata wewe huenda umekuwa ukikumbana na hali hiyo!
Unatakiwa kujua kwamba, kupitia kutokuamua kwako utapata matokeo ya namna mbalimbali maishani mwako!
Je ni aina gani ya matokeo, utakayoyapata kupitia kutokuamua? Mpendwa msomaji endapo hutoamua utapata matokeo yafuatayo: maisha yako, hali zako, masuala yako pamoja na mambo yako yote yatabaki kama yalivyo!
We unafikri nini kitayabadilisha Mambo hayo kama hutoamua kuyabadilisha kupitia kufanya maamuzi sahihi?
Au unataka kumaanisha kwamba kuna muujiza utatokea utakaobadili hali hizo maishani mwako?
Mpenzi msomaji unatakiwa kujua kwamba, kama hutafanya maamuzi kuhusu baadhi ya vipengele maishani mwako hakuna atakayekuamlia! Hakuna atakayeleta mabadiliko!
Mbali na hilo unatakiwa kujua kwamba, kuna baadhi ya mambo hayakuhitaji useme unamsubiri Mungu abadilishe, au afanye muujiza bali unatakiwa kufanya maamuzi juu ya mambo hayo!
Ndiyo maana unaambiwa tafuta nawe utapata! Suala la kutafuta linahitaji maamuzi pia! Kwamba usipoamua kutafuta huwezi ukatafuta! Na usipotafuta huwezi ukapata?
Natambua kabisa kwamba unapitia hali ngumu, natambua kabisa kwamba unatengeneza kipato cha chini, natambua kabisa kwamba unapitia magumu kwenye mahusiano na ndoa Yako, natambua kabisa kwamba hauna matumaini, natambua fika kabisa kwamba wewe ni maskini, natambua kabisa kwamba umechoka na maisha na pengine umeshakata tamaa, natambua mengi sana kuhusu maisha yako...
Anyway sipo hapa kukumotivate, bali nipo hapa kukufahamisha kwamba hayo yote yataendelea kuwepo katika maisha yako mpaka siku utakayofanya maamuzi ya kuyaondoa maishani mwako!
Kuna mwanasayansi mmoja aitwaye Isaack Newton, huyu mwanasayansi alikuja na kanuni ya inertia! Kanuni ya inertia inasema kwamba "vitu vilivyotulia vitabaki katika hali ya utulivu, mpaka pale itakapotokea fosi kutoka nje itakayovisukuma, ikiwa vitu vilivyo katika mwendo vitabaki katika hali ya mwendo mpaka pale vitakaposimamishwa"
Kanuni hii inatufundisha Mimi na wewe Kwamba, tusipoamua mambo yetu yatabaki kama yalivyo. Unatakiwa kujua kwamba maamuzi huwa ni kama fosi itakayoyasukuma!
Ukiachilia mbali hilo kanuni hii inatufundisha kwamba tukishaamua, maamuzi yatatuweka katika hali ya mwendo hivyo tutafanya mambo yatokee! Pamoja na kutokomeza changamoto mbalimbali tunazokumbana nazo!
Mpenzi msomaji badala ya kusubiri mambo yatokee, unatakiwa ufanye maamuzi yatakayopelekea kutokea kwa mambo hayo!
Kwani huu siyo wakati wa kusubiri mambo yawe sawa bali ni wakati wa kuweka mambo sawa, vilevile wakati tulio nao sasa siyo wakusubiri mambo yatokee bali ni wakati wa kuamua na kufanya mambo yatokee!
Nimalizie kwa kusema kwamba wote huwa tunaamua na hakuna ambaye hajawahi kuamua!
Unaweza ukaamua kuendelea kulala au kuamka!
Unaweza kuamua kubaki kuwa maskini au kupambana na umaskini!
Unaweza ukaamua kuendelea kubaki kwenye mahusiano yasiyo na tija au ukayavunja!
Unaweza ukaamua kubaki kuendelea kuteseka!
Hayo yote ni maamuzi unayoweza kuyafanya! Kutokana na hilo huna budi kujua kwamba kila Kitu maishani mwako kinahitaji uamuzi wako kwani unaamua! Unachagua!
Mbali na hilo nimedokeza kwamba hata kutokuamua ni kuamua pia Kwani kupitia kutokuamua kwako utapata matokeo fulani...
My friend huna budi kuamua vema ili upate vema!
Na Huu ndiyo mwisho wa somo la leo!
Kesho tutajifunza kwanini watu wengi huwa hatufanikiwi katika kufanya maamuzi sahihi!
Share ujumbe huu uwafikie wengi kwa kadri ya uwezo wako!
Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; mwalimu, mwandishi, muelimishaji katika eneo la maendeleo Binafsi, life coach and consultant!
Unaweza ukawasiliana nami kupitia Whatsapp no +255744284329
Tags
Elimu