NILIOLEWA NA JINI BILA YA KUTARAJIA
SEHEMU YA PILI
Namba ya WhatsApp- 0683 944 333
______________________________________
Akanivuta mkono kisha akatoa kitu cha ajabu kilichofanya nishtuke.
Nikajikuta jasho jingi likinitoka pale kitandani, nikawa najiuliza kuwa ni ndoto ya aina gani na inamaanisha kitu gani? Je huyo mwanaume mzuri sana kushinda Sam wangu ni nani?
Hapo ndio nikakumbuka kuwa natakiwa kumpigia Sam simu.
Nikaangalia simu yangu na kuichukua kisha nikaibonyeza, nikakuta simu ambazo hazijapokelewa kumi (10 missed call), kuangalia zote ni kutoka kwa Sam na ujumbe mfupi tano (5 messages).
Kila ujumbe ulikuwa ni wa lawama tu kutoka kwa Sam, nikaona haya majanga sasa.
Nikabonyeza simu na kuanza kupiga nikasikia,
"Salio lako halitoshi kupiga simu, tafadhari ongeza........."
Nikaishusha ile simu na kuikata, kuangalia kweli nimebakiwa na sifuri nikaanza kujiuliza kuwa nimeitumiaje ndipo nikakumbuka kuwa nilinunua salio na kusahau kujiunga na huduma za bure na wakati narudi nyumbani nilimpigia Suzy na kuongea nae sana tu nikijua nimejiunga kumbe sikujiunga, vocha yangu yote ya elfu mbili imekwenda bure bure bila hata ya faida sikujua cha kufanya kwa wakati huo.
Nikatamani niende chumbani kwa mama nikachukue simu yake na kuhamishia salio lake kwangu kama ana salio.
Nikainuka pale kitandani na kusogelea mlango kisha nikafungua, wazo la stori za majini likanijia tena kichwani na kujikuta nikiubamiza ule mlango kwa kuufunga na kurudi tena kitandani, nikajiuliza kuwa kwanini ile stori ya majini imenikaa sana kichwani mwangu? Nikaanza tena kufikiria ile ndoto kuwa ilikuwa na maana gani kwangu.
Sikuweza kulala tena kwa uoga na pia bado nilikuwa na mawazo juu ya Sam.
Asubuhi yake, mimi ndio nilikuwa wa kwanza tena kuamka, nikafanya usafi na kazi za hapa na pale nyumbani huku nikingoja pakuche vizuri nikanunue vocha ya kuweza kumpigia Sam.
Nilipomaliza usafi nilirudi tena chumbani, nikajilaza kitandani na usingizi ukanichukua hapohapo.
Yule mkaka mtanashati akaanza kunionyesha mali zake, zilikuwa nyingi sana. Kumbe yule mkaka alikuwa tajiri, akanionyesha magari ya aina nne halafu akaniambia kuwa nichague moja liwe langu naye atanipa lotelote, nikawa natabasamu kwani magari yalikuwa mazuri sana na ndoto zangu siku zote ni kuwa na gari ila gafla nikakumbuka kuwa nina Sam wangu ambaye hawezi kunipa vyote vile ila anaweza kunipa mapenzi ya dhati, nikajikuta nikishtuka na kupiga kelele.
"Saaaaaaaaaammmmmm....."
Mama akaja chumbani na kusema.
"Wee Sabrina wewe, usiniletee uchuro nyumbani kwangu. Yani wewe kuamka tu na kumtaja Sam! Amekuwa Mungu huyo Sam?"
"Hapana mama, ila nimeota vibaya"
Jasho nalo lilikuwa lanitoka.
"Umeota vibaya kivipi? Umeota Sam anachinjwa au?"
"Hapana mama."
"Haya inuka hapo, kuna mboga ya kukata kata huku"
Nikainuka tena pale kitandani na kumfata mama jikoni, kisha kukiendea kisu na kukata kata ile mboga.
Mawazo yalikuwa ni juu ya ile ndoto na yale magari, kisha nikakumbuka tena kuwa nilitakiwa kununua vocha na kumpigia Sam.
Nilikata mboga haraka haraka na kuibandika jikoni kisha nikajitanda vizuri ili niende dukani kwanza.
Kabla sijatoka mama akauliza,
"Unaenda wapi Sabrina?"
"Naenda dukani mama."
"Kufanya nini?"
"Kununua vocha mama"
"Ili umpigie Sam eeh!! Sijui huyo mwanaume amekupa nini mwanangu unakuwa kama chizi"
Sikutaka kumsikiliza zaidi kwani nilijua kuwa lazima atanizuia tu.
Nilinunua vocha na kurudi nyumbani. Nikamkuta mama sebleni,
"Huna adabu mwanangu Sabrina, yani umeona vocha ya maana kuliko maneno yangu? Vocha ambayo pesa nakupa mimi!!"
Nilibaki kumuangalia tu mama na maneno yake kwani nilijua yote sababu hataki niwasiliane na Sam.
"Haya lete hiyo vocha haraka"
Nilimpa ile vocha mama kwa shingo upande kwani moyo uliniuma sana, nikatamani hata kuwa na maisha ya kwangu. Nikatamani kutoa machozi mbele yake ila nikajizuia kwa kufumba macho ili mama asinione mzembe, ingawa na kujizuia kule bado machozi yalipenya na kudondoka mashavuni mwangu.
"Kaone kalivyo kajinga, eti kanamlilia mwanaume. Hebu niondolee uchizi wako mbele yangu haraka"
Nikaondoka na kukimbilia chumbani, huko nililia nitakavyo katika kupooza uchungu wangu.
Nilipotazama tena simu nikaona ujumbe wa Sam tena wa kutosha, sikuweza kujibu hata jumbe moja kwa kukosa vocha. Nikajikuta nikiulaumu mtandao ninaotumia pia kwa kushindwa kutuma tafadhari nipigie.
Nilizidi kutokwa na machozi tu mule ndani.
Wakati nalia nikasikia mtu akigonga mlango wa chumba changu, nikashtuka na kujiuliza ni nani maana dada na mama hawanaga hodi, huwa wanaingia tu chumbani.
Nikamuitikia kuwa aingie ndani, huku nikimaliza kujikausha machozi yangu. Kumbe alikuwa ni rafiki yangu mpenzi Lucy, nilifurahi kumuona nikainuka pale kitandani na kumkumbatia, nikamkaribisha vizuri sana.
Kumbe Lucy naye alishangazwa na hali aliyonikuta nayo,
"Nimekungoja sana hapo sebleni kwenu ndipo mama yako aliposema nikufate chumbani eti umechukia sababu ya mwanaume. Mmh! Mwanaume gani tena huyo Sabrina?"
Nikamueleza kwa kifupi kuhusu Sam kwani Lucy alikuwa hajui chochote kuhusu Sam.
"Inamaana kushindwa kuwasiliana nae ndio kunakuliza jamani shoga yangu? Chukua basi simu yangu uwasiliane nae maana ina muda wa kutosha"
Nikachukua simu ya Lucy na kumpigia simu ambapo alishangaa kuona namba ngeni.
"Mbona namba mpya hii, ni ya nani?"
"Ni ya rafiki yangu mmoja anaitwa Lucy ila wewe humjui, ipo siku utamjua"
Wakati nazungumza na Sam, Lucy nae akaniomba simu ili amsalimie shemeji yake huyo, nami nikamkabidhi.
Baada ya salamu tukazungumza na Sam kisha tukapatana tena na kusameheana kwa yote yaliyopita halafu Sam akanitumia vocha ili niache kumpigia kwa namba mpya.
Kilichobaki ilikuwa ni stori na vicheko baina yangu na Lucy.
"Mmh shemeji ana sauti ya kuvutia huyo, yaonyesha atakuwa handsome sana"
"Mmh Lucy ushaanza maneno yako, hukui wewe?"
"Kwani nikimsifia shem wangu kuna ubaya Sabrina?"
"Hakuna ubaya"
"Ila ningependa kumfahamu zaidi, natumaini ipo siku utanikutanisha nae"
Niliongea mengi sana na Lucy ila alikazana sana kumsifia Sam hadi akawa ananipa mashaka ila sikuyatilia maanani sana.
Lucy alipoaga, nilimsindikiza akaondoka.
Jioni ilipoingia kama kawaida ya siku hizi za karibuni, wakaanza tena stori zao za majini na aliyeanzisha alikuwa ni dada yangu Penina.
"Jamani Posta kuna mambo, yani mtu niliyepishana nae ni dhahiri kabisa alikuwa jini maana nywele zote zilinisimama"
Mama nae akadakia,
"Ulikuwa hujui mwanangu? Yani Posta na Kariakoo hakuwezi kukosa majini kule, unadhani unaopishana nao huko wote ni watu basi! Nusu yao ni majini"
Nikaanza kuogopa tena kwa yale maneno na hata sikujua kwanini mimi yaliniogopesha wakati wao walioyaongea hawakuogopa.
"Hivi jamani, kwanini ikifika usiku ndio mnaanza hizo stori za majini? Hakuna stori zingine?"
Dada akaanza kunicheka kuwa kwanini naogopa wakati ni kitu cha kawaida tu.
"Sasa wewe Sabrina unaogopa nini? Unadhani yatakutokea?"
"Naogopa tu jamani"
Mara mama akanitisha,
"Haya, huyo nyuma yako"
Nilipiga kelele na kurukaruka, huku wote wakiwa wananicheka.
"Hutakiwi kuogopa mwanangu, haya ni mambo ya kawaida na wengi yanawapata ndiomana tunayaongelea. Na ukitaka kutokuogopa kitu basi wewe kizoee"
"Ndio kuzoea majini mama?"
"Hapana si kuzoea majini, ila stori hizi uzione kama kawaida na hautapata shida tena"
Wakaendelea kusimuliana mambo ya watu wanaofufuka na majini.
Ikabidi nimuulize dada kuhusu ile picha aliyoniomba niifute jana yake.
"Dada, nakumbuka uliniambia kuwa majini ni mabaya na sura zao zina tisha. Mbona yule mkaka mzuri ulisema tufute picha yake kuwa huenda akawa jini?"
"Nilikuwa najisemea tu ila hata hivyo majini yanamtindo wa kubadilika kama kinyonga"
Mama akaingilia mazungumzo yetu.
"Kumbe na wewe Sabrina unawajua wakaka wazuri? Mbona ukampenda Sam basi?"
Dada akanisaidia kujibu,
"Ila Sam sio mbaya jamani mama, humpendi tu sababu ya kipato ila usisingizie uzuri"
Nikawaacha na kwenda chumbani kwangu. Nikaenda kuoga kisha kujiandaa kulala.
Usiku wa leo ulikuwa na uoga kiasi kwangu na furaha pia kwani vocha nilikuwa nayo na Sam nilishapatana naye.
Nilipokuwa tu kitandani nikampigia Sam simu ili kupotezea yale mawazo ya stori ambazo mama na dada walikuwa wakisimuliana.
Niliongea sana na Sam kwenye simu hadi saa saba usiku kisha nikapitiwa na usingizi huku simu ikiwa sikioni.
Nilikuwa ufukweni (beach) na Sam tukifurahia upepo na kuchezea maji. Sam alivaa nguo nyeupe na mimi nilivaa gauni la pinki, tulifanya mambo mengi sana ambayo wapendanao huwa wanafanya.
Tukaanza mchezo wa kufunikana macho kwa nyuma na wakati huo Sam alikuwa nyuma yangu na mikono yake imepita juu ya mabega yangu kisha viganja vyake vilifunika macho yangu, akaanza kunitembeza na kunipeleka nisipopajua.
Kufika mbele akaniuliza,
"Nikufumbue macho nisikufumbue?"
Nami nikamjibu kwa sauti ya taratibu tena ile ya kudeka,
"Nifumbue bwana"
Basi Sam akaachia vile viganja vya mikono yake nami nikapata kuona kilichopo mbele yangu, nikamuona yule mkaka wa kwenye ndoto akiwa mbele yangu na alivaa nguo nyeupe tupu kuanzia kiatu, suruali hadi shati.
Nikajikuta nikitetemeka ila yeye alikuwa akitabasamu, nikaangalia nyuma yangu kama yupo Sam ila hakuwepo na sikujua ameelekea wapi, nikaanza kukimbia huku yule mkaka akinifata nyuma alipokaribia kunishika nikashtuka kumbe nilikuwa naota.
Jasho jingi lilinitoka, kutazama nje kulikuwa kumekucha kabisa yani kama sio saa mbili basi ni saa tatu.
Kabla sijafanya chochote, simu yangu ikawa inaita kuangalia ni Sam anapiga basi nikaipokea, baada ya salamu nikamsikia.
"Uwahi kujiandaa mpenzi ili badae twende beach, sawa Sabrina. Halafu uvae lile gauni lako la pinki"
Niliendelea kuweka ile simu sikioni bila ya kujua cha kujibu.
Itaendelea….!!!
Tags
simulizi