NILIOLEWA NA JINI BILA YA KUTARAJIA
SEHEMU YA TATU
Namba ya WhatsApp- 0683 944 333
_______________________________________
Niliendelea kuweka ile simu sikioni bila ya kujua cha kujibu.
Upande wa pili nao ulishangazwa na kimya changu na kuuliza,
"Vipi mpenzi mbona kimya? Hujanielewa au?"
Nikajikaza kumjibu kwa sauti ya upole,
"Ndio sijakuelewa"
"Nimekwambia kuwa uwahi kujiandaa kwaajili ya ile safari yetu ya beach na uvae gauni lako lile la pinki. Bado hujaelewa?"
Nikaishusha ile simu taratibu, sauti ya mama ikanishtua ambapo alifungua mlango bila ya hodi kama kawaida yake na kuanza kuongea.
"Yani mtoto wa kike ndio unaamka saa nne hii, halafu kitu cha kwanza ni kukumbuka hilo pepo lako chafu la simu"
Nikajikuta nikiiachia ile simu kwani nilishangaa kuwa muda ule ni saa nne sema kwa bahati ilikuwa ni kwenye kitanda ndio ikaangukia hapo.
"Mbona umetoa macho tu hata hunijibu wakati simu umeongea nayo?"
"Jamani mama hata salamu? Shikamoo."
"Haina umuhimu saa nne hii, kazi zote umeniachia mamako kama vile sikuzaa jamani!! Haya inuka hapo kitandani uje huku"
Halafu akatoka, nikamshangaa mama kuongea vile wakati si kawaida yangu kulala sana mpaka kupitiliza kiasi kile. Na hata kama nikilala vile basi ni kwamba kuna muda niliamka na kufanya kazi kisha kurudi tena kulala ila siku hiyo nilipitiliza hadi kujishtukia.
Nikajitoa chumbani na kwenda jikoni kumuomba mama msamaha kwa kuchelewa kuamka.
"Unaona kama nakukera mwanangu ila mimi nakufundisha hata utakapoolewa uwahi kuamka, hakuna mwanaume anayependa kuishi na mke mvivu. Yani hadi saa nne mwanamke hajaamka, hajafanya usafi wala kuandaa chai. Nakwambia kwa mtindo huo mwanaume lazima akuache, mwanamke mwingine anamuachia kazi zote msichana wa kazi hadi kazi za mumewe, mwisho wa siku mume anachukua msichana wa kazi badili ya mke. Nakufundisha kazi mwanangu, sijui kama unanielewa!"
"Nakuelewa vizuri sana mama yangu"
"Itabidi nikupe darasa kabisa na kama ukilifata basi kuachika usahau kabisa na kama huyo mume akikuacha basi atakuwa na hila ya kwapa kunuka bila kidonda"
Kwakweli mama yangu alikuwa ni muongeaji sana hadi kipindi wakati baba yupo alikuwa anamuita mama kasuku na tulikuwa tunacheka sana.
"Sasa mama utanipa lini hilo darasa? Nipe leo basi"
"Kwani unataka kuolewa? Hebu nitolee uchuro wako mie nionekane nina uchu sana wa mahari yako."
"Kwani mama mi sifai kuolewa?"
"Nikuoze kwa kale kajamaa kale!! Katanipa nini mimi? Hebu nenda kwanza kaoge huko"
Nikajiinukia kwa unyonge na kwenda kuoga.
Niliporudi chumbani nilikuta simu yangu inaita na mpigaji alikuwa ni Sam, nikaipokea ile simu.
"Mbona unadharau hivyo Sabrina? Kweli wewe wa kutokuijibu simu yangu jamani!!"
"Nisamehe mpenzi wangu"
"Ndio unachoweza kusema hicho, unakumbuka tulichopanga usiku wakati tunaongea kwenye simu?"
"Nimesahau Sam"
"Nakata simu halafu nakupa dakika kumi uwe umekumbuka, nitakupigia tena kunipa jibu"
Halafu Sam akaikata ile simu, nikajikuta nikianza kurudisha mawazo ya nyuma kichwani mwangu.
Nikakumbuka kuwa niliongea na Sam hadi usiku sana ila sikukumbuka tumeongelea kitu gani, mara kumbu kumbu za ndoto zikanijia hadi pale ambapo Sam aliponipigia simu ni hapo nilipojituliza akili na kujiuliza kuwa kuna mahusiano gani ya yule mwanaume wa kwenye ndoto zangu na Sam? Na kwanini Sam aniambie nivae gauni la pinki ambalo limetokea kwenye ndoto zangu?
Wakati natafakari hayo simu yangu ikaanza kuita, nilipoona kuwa ni Sam nikajua tu kuwa anayataka majibu yake. Nikapokea ile simu,
"Haya niambie ulichokumbuka"
"Kwakweli tuliyoyaongea usiku sikumbuki kabisa ila ninachokumbuka ni tulichoongea asubuhi"
"Ok, hiyo asubuhi nilisemaje?"
"Ulisema kuwa niwahi kujiandaa ili twende beach na nivae gauni langu la pinki"
"Sawa sawa, kumbe kumbe kumbukumbu unayo. Sasa kwanini hukumbuki vya usiku? Na je ushajiandaa kwa safari?"
"Bado sijajiandaa"
"Kwanini unanifanyia hivyo Sabrina jamani? Unajua mambo mangapi nimeacha kwaajili yako? Mbona unadharau kiasi hicho?"
"Hapana Sam"
"Kwanini Hapana?"
"Kwanini uchague gauni la pinki? Na mbona umenishtukiza na hiyo safari wakati siku zote huwa nakwambia kwamba uniambie mapema? Unanionea tu Sam na yote sababu unapenda ubabe"
"Naomba uelewe Sabrina, kwanza kabisa hii safari si ya kushtukiza. Jana usiku tumejadili wote kwenye simu kuwa leo twende beach, halafu kuhusu swala la nguo ulilianzisha mwenyewe jana na ukasema kuwa mimi nivae shati nyeupe na ukaniuliza kuwa mimi ningependelea wewe uvae nguo ipi, wakati nakujibu ulikuwa umepitiwa na usingizi ndiomana nikakupigia muda ule kukuambia kuwa nimependelea uvae gauni la pinki. Haya kosa langu ni nini hapo?? Je tutaenda huko beach?" Nilibaki kimya nikijishangaa kuwa usiku nilikuwa nikijadili na Sam kitu cha namna ile, Sam alingoja jibu hadi akaamua kukata simu.
Nilitafakari mara mbili mbili na kujiuliza sana kuwa au sikuota chochote sema ni maruweruwe tu, ila kumbukumbu zinaniambia kuwa mambo yale nimeyaona kwenye ndoto kwahiyo sikuwa na jinsi zaidi ya kukataa ile safari.
Sam aliponipigia tena nikamwambia kuwa sitaenda basi aliongea maneno mengi ya hasira. Kwakweli Sam alichukizwa sana na maamuzi yangu ila nilifanya vile ili kuepusha kutokea kama kilichotokea kwenye ndoto.
Mama akaja kunifata tena chumbani na kunikuta nikiongea na simu huku nikimbembeleza Sam aweze kunielewa.
"Simu hizo simu mwanangu, sijui hata zinakusaidia nini? Toka useme unaenda kuoga hadi sasa jamani? Hujala wala hujafanya chochote cha maana. Kwakweli nakuhurumia mwanangu, haya njoo tule chakula tayari mamako nishapika na kukuandalia malkia wa nyumba hii"
Mama akatoka, kwakweli nilijisikia vibaya ila ikabidi nitoke kumfata mama pale mezani ili asiseme tena.
Wakati tunakula, sauti ya Sam ikawa inajirudia kichwani mwangu kuwa kwanini nimemkatalia ile safari.
Sauti ile ikarudia mara kwa mara hadi nikajikuta nagonga meza na kusema,
"Aaaaaaaarggghhhhhhh........"
Kumbe nilipiga kelele mi nilijua kuwa nimejisemea chini chini, mama akashtuka na kuniangalia kwa jicho kali,
"Wee mwana wee umeanza kuwehuka?"
Nilibaki kumkodolea tu macho mama bila ya kusema chochote.
"Mamako nimepika chakula kizuri na kitamu ili malkia wa humu ndani ule ufurahi sasa unaniletea uchizi mezani. Unatatizo gani jamani mwanangu mzuri Sabrina?"
Nilitamani kumueleza mama ila nikajua kuwa kwa vyovyote vile lazima atazidi kumchukia Sam, ikabidi nimwambie kuwa sina tatizo. Ila kile chakula nilikuwa nakitazama tu na kuchezesha kijiko, mama alimaliza kula na kuniacha mwenyewe pale mezani. Badae nikaenda kukifunika jikoni, kisha nikarudi sebleni na kuweka picha za ngumi kwenye video na kuanza kuangalia.
Nikasikia simu yangu inaita, nikaenda kuichukua nikakuta ni Lucy ananipigia nikaenda kuongea nayo sebleni.
"Jamani Sabrina! Yani shem anakuomba mtoke out unamkatalia jamani! Kwani unafanya nini hapo kwenu?"
"Kwani wewe nani kakwambia?"
"Nimewasiliana na shem kaniambia, kwakweli ulichofanya sio kizuri shoga yangu."
"Fanya yako mengine hayakuhusu"
Halafu nikaikata ile simu hata nikajishangaa kwa kumchukia hadi Lucy.
Niliangalia Video ile ila bado haikunoga, moyo wangu ulikuwa unavutika kuwa ufukweni tu mambo mengine yote kwangu niliona kama ni kujisumbua tu.
Mama alikaa na mimi na tukaangalia wote ila bado haikunoga, hadi dada anarudi alinikuta palepale sebleni na sielewi chochote.
Mara gafla kichwa kikaanza kuniuma, nikamwambia mama akaenda kuniletea dawa nikanywa kisha akaniambia kuwa nikapumzike kwanza ilikuwa kama mida ya saa kumi na mbili jioni.
Nilipofika tu kitandani usingizi ukanichukua hapohapo na kama kawaida ndoto za maruweruwe zikanianza tena.
Nilikuwa mahali nimesimama na mbele yangu amesimama Sam huku akinilalamikia kuwa kwanini nimekaa kwenda nae.
"Najua Sabrina hunipendi ndiomana umekataa kutoka na mimi."
Na mimi nikamjibu,
"Hapana Sam nakupenda tena sana tu"
"Sabrina hunipendi, ila kuna mvulana mzuri na mtanashati wa kwenye ndoto zako ndio unayempenda. Najua yeye anaweza kukupa gari, nyumba na chochote cha gharama utakacho ila mimi sina uwezo huo Sabrina ndiomana hunipendi"
"Si kweli Sam nakupenda wewe"
"Ungenipenda mimi usingekataa kwenda beach na mimi Sabrina, usingekataa kutoka na mimi"
pembezoni mwa mazungumzo yetu akatokea yule kaka wa kwenye ndoto huku akitabasamu.
Nikashtuka gafla na kusema,
"Nakupenda sana Sam"
Kisha nikainuka pale kitandani, nikatoa gauni langu la pinki tena bila hata ya kufikiria mara mbili, nikavaa na viatu navyo nikavaa.
Kisha Nikatoka chumbani na kupita sebleni hakukuwa na mtu yeyote yule, wote walikuwa wameshalala kumbe ilikuwa ni usiku sana ila sikujali, nikaenda kufungua milango ili nitoke nje niende huko ufukweni.
Itaendelea….!!!
Tags
simulizi