ONYO: SIMULIZI INAHUZUNISHA SANA.
Story: SHUJAA
episode: 04
ILIPOISHIA.......
Ester alitoka huku analia. Alipiga hatua tano baada ya kutoka ofisini ghafla alisikia sauti kali.
"Wewe si nilikwambia unione ukitoka huko" alikuwa mwalimu Herman.
ENDELEA NAYO......
Ulikuwa mshituko wa kipekee uliotambaa ndani ya mwili wa binti Ester mara baada ya kusikia sauti ya mwalimu Herman aliyekuwa anamuita. Huyu mwalimu alijitenga mahali fulani peke yake.
"Fanya haraka" alisema tena mwalimu Herman aliyeonekana kuwa tofauti na kawaida yake. Alikuwa na hasira achilia mbali ule ukali aliokuwa anauonesha. Hakika Ester alishangaa na kuogopa mno leo hii.
Alipiga hatua za haraka kufuatia wito huku mkono wake wa kulia ukienda hadi usoni kufuta machozi yaliyokuwa yametapakaa.
"Twende ofisini huku" aliamuru mwalimu Herman Kisha aliongoza njia wakati huo binti Ester yupo nyuma yake, wasiwasi mkubwa umetanda utadhani ng'ombe anayepelekwa machinjioni.
Walifika ofisini, mwalimu Herman alivuta kiti na kujituliza akiruhusu sekunde kama thelathini kupita pasipo kusema chochote, zaidi ya kujiinamia na kugonga gonga meza mithili ya mtu mwenye mawazo mengi, alikuwa anajaribu kuzichunga hasira zake na kuzipunguza. Ukimya ulitawala,, baadae kidogo mwalimu alinyanyua kinywa.
"Ester!!"
"Abe Sir" aliitika Ester huku anatetemeka.
"Hivi unajua ni kiasi gani nilikuwa nakuamini wewe??" Aliuliza mwalimu Herman lakini Ester alibaki kimya maana aliulizwa swali rahisi lenye jibu gumu. Hakujibu chochote.
"Ester nilikuwa nakuamini sana. Nilikuona wewe ni Binti mwenye maadili ya kiungu,, usiyependa mambo ya dunia. Hata hivyo kila ambaye alikuona sina shaka alipata kuiona hiyo picha nzuri." Alitulia kidogo na kutafakari kisha aliendelea.
"Nimeiona hiyo picha tangu nahamia hapa,, yani kila kitu chako kilidhihirisha mazuri ninayoyasema saa hii na ndio maana yalipokuja masuala ya kwamba wewe unahangaika na wanaume nilipata ujasiri wa kupinga na kukutetea. Ile siku wangeniuliza niwape ushahidi kwanini nakutetea nisingewapa ushahidi zaidi ya maneno ambayo mtu huweza kuhisi nadanganya tu lakini sikujali hilo." aliongea kwa msisitizo.
Ester hakuwa na la kujibu, amebaki tu anasikiliza mambo anayosimuliwa na mwalimu. Mambo ambayo si mageni kwake kwani yalimuhusu yeye mwenyewe.
"Japokuwa walimu wenzangu walinipinga sana na kuona natetea uovu lakini sikujali kwani nilikuwa na uhakika na ninachokisema. Nilikuwa na uhakika na utetezi wangu lakini umefanya nini tena Ester eh" aliongea mwalimu Herman.
"Kumbe yaliyokuwa yanaongelewa ni kweli,, nilidhani najitutumua kukutetea kumbe najitutumua kujipaka matope na hadi sasa ninavyosema sijui naificha wapi sura yangu,, walimu nao wanaanza kuniona muhuni tu,, wananitenga kwanini umefanya hivi Ester?"
Ama hakika uchungu,, maumivu hayachagui. Huweza kukaa popote yanapopenda. Maumivu yalimshika mwalimu Herman hadi akadondosha chozi.
"Wema wangu umeniponza,, nilijitoa kukusaidia lakini kumbe nilikuwa namsaidia mchafu kunichafua. Na nimechafuka hakika" alisema kwa uchungu na kuinamisha uso wake chini. Aliona haya kutoa machozi mbele ya mwanafunzi wake.
Maneno ya mwalimu yalikuwa mithili ya msumari wa moto uliokuwa unachokonoa chokonoa kuta za moyo wa Ester, aliumia zaidi. Aliona ni heri aseme ukweli ili tu ifahamike japo haitasaidia chochote kwa sasa.
"Mwalimu naomba unisamehe kwanza,, pia naomba unisikilize. Haya yote yaliyotokea amesababisha rafiki yangu Janeth..." alieleza Ester, alipotaka kuendelea alikatishwa na sauti ya mwalimu.
"Nenda darasani, nikiwa na shida nawe nitakuita" alisema akiwa amejiinamia vile vile.
Ester alidhani amepata nafasi kuelezea ukweli wake aliouficha siku zote lakini nafasi nayo ikakimbia. Aliganda hajui aondoke au ajaribu kumuomba aongee naye ili amueleze.
"Mwal,, mwalimu!!" Aliita
"Nimesema nenda darasani" alisema na kuinua uso wake uliojaa hasira macho yalikuwa mekundu mno hadi Ester aliogopa. Alitoka haraka na kwenda darasani.
Minong'ono ya hapa na pale ilisikika mle darasani alipoingia tu minong'ono yote ilipotea. Alitambua hiyo minong'ono ilimuhusu yeye, hakujali sana alielekea hadi kwenye meza yake na kujiinamia huku kizunguzungu kikipigana vita vikali na ubongo wake.
Hata hakupata dakika za kupumzika ghafla alisikia kengele ikigongwa. Ilikuwa kengele ya dharura. Maneno ya wanafunzi wenzake yalisikika waziwazi. Maneno ambayo mwanzo yalikuwa minong'ono.
"Ohoooo mambo tayari hukoo, hatunaye tenaa. Shule ilimpenda lakini dunia imempenda zaidi" alitamka hayo mwanafunzi mmoja wa kiume, alipita haraka karibu na Ester na kumpiga kikumbo, Ester alipepesuka kidogo aanguke.
Wanafunzi wote walikuwa katika mistari iliyonyooka.
Walimu walianza kutoka ofisini na kujaa pale kwenye uwanja wa kukusanyikia.
Walikuwepo walimu wote ndani ya eneo hilo isipokuwa mwalimu Herman ambaye alijitenga mbali.
Mkuu hakutaka kuzungumza sana wala kuzunguka sana.
"Wanafunzi tumewaita hapa kwa lengo moja tu. Tunataka mjifunze kuwa hata ukibakisha wiki moja tu kufanya mtihani tutakutimua ukileta ujinga, kuna mpumbavu mmoja amekutwa na kesi ya kinidhamu. Sasa hili halihitaji kuita wazazi wala kuhojiana chochote na mtu yeyote yule. Huyu Ester Valency tunamfukuza shule moja kwa moja maana hata ushahidi wa ujauzito anao hivyo kuanzia leo si mwanafunzi wetu" alisema mkuu.
Ester nguvu zilimuisha hakuamini alichosikia, hakukaa sawa aliitwa akachukue barua kwenda kuwapa wazazi ili wafahamu.
"Haya funga virago vyako nenda, wasalimie Iringa" alikuwa Mwalimu David.
Ester alirudi pale wanapoishi na Janeth,, muda wote analia tu haamini kama yaliyomkuta ni ya kweli. Alifikiria safari ya Morogoro kwenda Iringa, aondoke lini??? Hata jibu alikosa kabisa na kila alipojiuliza swali kuwa ataenda kuwaambia nini wazazi wake?? Nguvu zilimuishia.
Atawaambia nini wazazi wake waliojitoa kwa hali na mali kuhakikisha wanampa mtoto wao wa pekee kila alichohitaji ili tu asome kwa bidii?? Ataenda kumwambia nini Mama yake ambaye kila mara amekuwa akimsisitiza kujitunza???
"MUNGU kwanini umeruhusu hili litokee kwangu???" Ester alilia sana.
Hadi kufikia hapo Ester aliona dunia ni nzito na imemuelemea mno. Hakujua kwanini haya yanamtokea ilhali hana kosa lolote. Aliona dunia haiko sawa kwani yule mwenye kufanya mabaya siku zote yuko salama na hajakutwa na maswahibu kama hayo lakini yeye ambaye daima huenda katika njia za kumpendeza MUNGU amekutana na mabaya hayo ya kuvunja moyo. Aliumia sana.
Muda wote alikuwa analia, alilia hadi ilifika wakati hata mwili wake ulikataa kutoa machozi tena nayo sauti haikutoka, alibaki tu anajikakamua kutoa machozi na sauti ya kilio pengine angeweza kuutua mzigo wa uchungu uliong'ang'ania moyo wake lakini haikuwezekana, zaidi tu aliumia koo kwa kujikakamua kulia.
Uchovu kutokana na kulia uliingia mwilini mwake. Alichoka haswaa hivyo aliamua kutulia ili apumzike kwanza.
Haikuwa kazi rahisi kujituliza kutoka kwenye hali hiyo lakini kwa jitihada zake za kujisahaulisha hatimaye kilio kilikata kabisa. Alikuwa amekaa chini huku mgongo wake ukiwa umeegamia kwenye kitanda.
Alitembeza macho huku na huku lengo tu kuepusha macho yake kuganda sehemu moja hatimaye akaanza kupata mawazo tena. Akili ya kuimba nyimbo fulani fulani ilimjia, alihitaji kuimba ili ajichangamshe lakini kiukweli huo uwezo wa kuimba hakuwa nao.
Hata alipojaribu kukumbuka nyimbo za kuimba, zilimjia zile nyimbo zilizobeba huzuni isiyo kifani. Aliamua kuacha na kusimama labda akatembee tembee nje kupoteza mawazo.
Aliposimama alihisi maumivu makali mwilini nalo tumbo lilifanya kuvuta hivi. Alilishika na kulitazama, alipolitazama tu akili ilimwambia.
"Hili ndilo tumbo lililobeba mimba"
Ester alishituka utadhani ilikuwa sauti ya mtu iliyomwambia haya. Masikini Ester alirudi katika huzuni na kilio ambacho kilitulia kwa muda. Alilia tena, haamini kama amebeba ujauzito,, ujauzito uliomuondoa katika maisha ya shule.
"Ina maana mimi sio mwanafunzi tena!!! Aaaah!" alilia Ester. Hakuamini kama yupo katika maandalizi ya kuitwa Mama wa mtoto. Vipi kuhusu Baba wa mtoto???
Hamjui labda sura tu kwa mbali.
Hii siku ya Ijumaa ilipita akiwa hajui anaanzia wapi kutoka na kwenda nyumbani Iringa, Jumamosi nayo ilipita. kiukweli pale ndani walikuwa wanaishi kama maadui, chuki ilitawala kati ya Ester na Janeth. Jambo Kidogo tu walizozana mno.
"Kwanza si uondoke tu, unanijazia nyumba hapa. Unachosubiri nini?" Hii ilikuwa kauli ya kila mara kutoka kwa Janeth.
"Huwezi kuniamuru hivyo shetani wewe"
"Mimi shetani???" Alifoka Janeth na kumrarua mwenzake kofi zito.
"Na bado,, hautaamini nitakachokufanyia! wewe ngoja uone" alisema Janeth.
Ester alikuwa anaumia kila sekunde kila dakika ,, raha aliikosa kabisa.
siku ya Jumapili ilifika na ilipita hata kanisani hakuenda maana alihisi nguvu ya kwenda huko haipo kabisa. Kila alipokumbuka yaliyomtokea aliona kama MUNGU amemuonea, hakwenda kanisani.
Kuhusu kula alikuwa anakula kidogo sana hata afya yake ilidhoofu mno ndani ya hizo siku tatu tu.
Ilikuwa Jumatatu sasa, aliamka hajui afanye nini na aende wapi.
Pa kwenda ni Iringa ila angeanzaje???
Majira ya saa 5 asubuhi akiwa hapo nyumbani ghafla alisikia mlango unagongwa. Hakujua ni nani ndio maana basi hakutaka kujibu haraka.
'ngo ngo ngo' yule mtu aligonga kwa mara nyingine tena, hakutaka kutoa sauti yake, alikuwa anagonga tu.
Ester aliamua kunyanyuka na kwenda kufungua mlango. Alikutana uso kwa uso na Janeth aliyekuwa pamoja na walimu wawili.
"Yani wewe binti tumekufukuza uondoke uende kwenu huko lakini bado umeng'ang'ana hapa. Unamsumbua mwenzako hapati raha ya kujisomea maana anasema muda wote wewe ni kuingiza tu wanaume."
"Ndio ukweli huo mwalimu nashindwa hata kusoma maana mwenzangu hajali wala haogopi kuleta watu wake. Mbaya zaidi anataka na mimi nifanye upuuzi anaofanya" alisema huku anatoa chozi Janeth. Walimu waliamini.
"Kweli mtu aliyezoea mambo yake huwezi kumbadilisha, yani licha ya ujauzito bado huachi wanaume. Ama kweli umeshindikana wewe" huyu alikuwa yule yule mwalimu David.
"Tena usitake kumuharibu mwanafunzi wetu, andaa virago vyako uende"
Sasa Janeth alihitajika kuingia ndani kuchukua kila kilicho cha Ester akitoe nje.
Janeth alifanya hivyo kisha mlango ulifungwa.
"Kwa usalama wako ondoka tu" alisema mwalimu David kisha wao waliondoka na kumuacha Ester peke yake pale.
Hata nauli hakuwa nayo hivyo hakujua anaondokaje. Akiwa hapo ghafla alikumbuka kitu. Alikumbuka ile siku alipewa elfu hamsini na Janeth.
Aliitafuta sana kwenye begi lake mwisho aliipata, alisimama na kuanza kutembea taratibu.
"Nyumbani siendi bora nipotee. Naenda kokote ninakokujua mimi" alijisemea Ester huku analia wakati huo begi lake lipo kichwani.
ITAENDELEA.......
Tukutane kesho asubuhi ili kujua sehemu atakayoenda Ester.
Tags
simulizi