ONYO: SIMULIZI INAHUZUNISHA SANA.
Story: SHUJAA
episode: 03
ILIPOISHIA.......
"Nyie ndio wahuni hamtaki kuja shule mnaenda kudanga. Na tunawasaka sana watu kama nyinyi mnaoharibu sifa ya shule yetu, sasa leo utanitambua" alifoka mwalimu David na kumvuta mkono Ester hadi ofisini.
Bakora kali zilianza kusikika zikirindima ndani ya ofisi.
ENDELEA NAYO......
"Mwalimu mimi sina tabia hiyo" alijitetea Ester lakini utetezi wake haukutosha kumshawishi mwalimu David asimpige. Ester alishuhudia kofi zito likitua shavuni kwake.
"Unadhani mimi mtoto mdogo?? Kwahiyo mimi nakusingizia??" alifoka mwalimu na kurusha bakora bila kujali inaenda kutua mahali gani ikishafika kwenye mwili wa Ester. Ile bakora ilitua shingoni, kidogo tu itue usoni.
Ester alilia kwa uchungu wa bakora na kwa kusingiziwa ila angefanyaje. Aliogopa kujitetea kwani kujitetea ilikuwa ni sumu kwake. Mwalimu aliendelea kumpiga utadhani walikuwa na ugomvi hapo awali.
"Hey! Sir David mbona unampiga mwanafunzi kiasi hicho!!?" alishangaa mwalimu Herman baada tu ya kuingia ndani ya ofisi ile.
"Hawa ndio ninaowatafuta siku zote,, wanachafua shule yetu kwa tabia zao za umalaya huko" mwalimu David alitamka pasipo kujali ukali wa neno wala uhalisia wake.
"Lakini mwalimu una uhakika ndio tabia yake hiyo??? Isije kuwa unamuadhibu kwa kosa lisilokuwa lake" alisema mwalimu Herman na kutoka baada ya kuweka vitabu vyake mezani. Hali aliyoikuta iliendelea. Ester alidhani labda itakuwa ahueni ila wapi.
Alitamani kutoka na kukimbia ila huo uwezo alikosa, alilia hadi machozi yaligoma kutoka tena.
Aliona akiendelea kutulia bila kujitetea atapata shida zaidi.
"Mwalimu mimi sina tabia hiyo unanionea" aliongea huku analia. Mwalimu alichukia zaidi.
★
Majira ya jioni alirudi nyumbani akiwa hoi bin taabani kutokana na yote yaliyomkuta siku hiyo. Yote yalimuumiza hakuacha kulia hata kidogo. Aliamini chanzo cha yote hayo ni Janeth. Alitamani ahame hapo nyumbani aende sehemu nyingine ila angeenda wapi??? Ataenda kukaa bure??
Hakuwa na uwezo kwenda kupanga chumba kingine. Hata angewaambia wazazi wangemshangaa na kumhoji sana. Kwanini anataka kuhama??? Angewajibu nini wakati hakuwa tayari kueleza ukweli.
Ester hakujua kwanini alificha ukweli juu ya yote aliyofanyiwa na Janeth
Hakujua kwamba ni kwa sababu anampenda ama ni woga tu katika kusema ukweli. Hata sasa kama ingetokea akaulizwa ni nini kilimkuta bado hakuwa na uwezo wa kuweka bayana.
Ndani ya nyumba walikuwa kama mabubu,, hakuwepo ambaye alijaribu kuzungumza chochote kwa mwenzake. Ester hakutaka kabisa, alimuona Janeth kama ni shetani wake mwenye kutaka kumtoa roho. Muda wote alijiinamia,, machozi yanamtoka hasa alipokumbuka kuwa hana usichana tena. Alilia.
★
Ilikuwa Ijumaa..
Baada ya kujiandaa vizuri alitoka na kuelekea shule. Mawazo mengi yalikisumbua kichwa chake,, akijaribu kuwaza juu ya kitakachotokea leo. Hakutaka kuwa na hofu sana kwani aliamini ya jana ni ya jana tu.
Majira ya saa nne asubuhi alishituka kusikia anaitwa ofisini kwa mwalimu mkuu wa shule. Mapigo ya moyo yalienda kasi,, hakujua anaitiwa nini.
Alitembea haraka huku hofu ikimshika mno. Alifika ofisini pale ila kabla hajaingia, macho yake yalitua juu ya walimu sita kwa idadi waliokuwepo pale ndani. Mwalimu David alikuwa miongoni mwao. Ester aliogopa.
Ester alitoa salamu ambayo ilimfanya ajilaumu tu kwani hakuna mwalimu aliyeitikia. Mkuu hakutaka kupoteza muda.
"Nyie kidato cha sita mnakaribia kufanya mtihani yani mmebakisha miezi minne tu.
Tunawategemea ila mwenendo wenu hautupi matumaini kabisa. Mna tabia mbaya hivyo tunaanza na wewe"
Ester alitetemeka na kugundua kumbe yale mambo hayakuisha, mwalimu David aliyafikisha kwa mkuu.
Kama kawaida Ester alijitetea vya kutosha ila aliambulia kipigo cha mbwa mwizi tu. Alipigwa hadi baadhi ya walimu walimuonea huruma.
"Jamani sina tabia hiyo kama hamuamini basi muulizeni Janeth" alilia
"Janeth ndio nani??" aliuliza mwalimu mkuu.
"Mwenzangu ninayekaa naye, naye ni form six(kidato cha sita)"
Muda si mrefu Janeth aliitwa kuulizwa hayo mambo juu ya mwenzake. Kwanza alishangaa namna mwenzake alivyopigwa hadi amevimba.
"Wewe binti unamfahamu huyu?" lilikuwa swali la mwalimu mkuu.
"Ndio! Ninakaa naye" alijibu Janeth akijifanya ana ujasiri ila alikuwa anatetemeka kwa woga.
"Sawa binti,, hatutaki kuzunguka na ninaomba uwe mkweli. rafiki yako hatulii,, anahangaika na wanaume ni kweli au si kweli?" aliuliza mwalimu David kwa wakati huu.
Janeth alijing'ata ng'ata bila kujua ajibu nini.
"Wewe tunakuuliza" alifoka mwalimu David na kurusha fimbo iliyompiga Janeth.
"Ndio mwalimu ni kweli" alijibu Janeth
Moyo wa Ester ulishikwa na ganzi iliyosababisha ubaridi wa kipekee kama umemwagiwa maji. Alihisi alichokisikia hakikuwa sahihi kwa kuamini labda masikio yamepokea taarifa tofauti na ile iliyotolewa.
Alichokisikia ndicho kilichotamkwa tena kilisisitizwa zaidi.
"Ndio ni kweli Ester hatulii nyumbani, anahangaika na wanaume"
Kama Ester angekuwa na tatizo la presha ama kwa hakika angeanguka na angezimia hapo. Sasa nikuulize swali. Unahisi walimu watamtafsiri vipi Ester?? Ameulizwa mara kibao, amepinga mara kibao. Walimu watamtafsiri vipi??? Ester msumbufu na amewapotezea muda kwa uongo wake.
'Paaaaaaaaaaaaaaaaah!!!!!!!!!' ilisikika kofi iliyotambaa kwenye shavu la kushoto la binti Ester. Akupigaye shavu la kushoto mgeuzie na la kulia. Ester hakugeuza lakini alishituka akipigwa kofi lingine zito kwenye shavu lake la kulia. Kofi hili lilikuwa zito kwani lilisababisha kizunguzungu kilichombwaga chini kama mzigo.
Kilio hakikuisha, kilisikika bila kukoma, Ester alilia sana. Angejiteteaje tena wakati shahidi ameshathibitisha hilo.
Ester ugumu ulikuwa wapi kusema ukweli??? Aaah!
"Huyu Janeth ndio..." aliongea kwa upole akiwa chini palepale ila hakumalizia kusema mkuu alidakia na kwa hasira alifoka.
"Acha kutupigia kelele na uongo wako pumbavu"
"Yani muda wote unatusumbua tu na kutudanganya,,, unatuona sisi wapumbavu sio!?? Unatuchukulia sisi ni bibi zako" alifoka mwalimu David na kurusha fimbo iliyotua mgongoni mwa Ester
"Aaaiiiiiiiiih!!!" aliiishia kutoa mlio wa maumivu. Kuinuka alishindwa kwani kizunguzungu kilimbana chini.
Alipigwa fimbo nyingine mbili za mgongoni. Aliamua ajikaze kusimama la sivyo kifo kitamkuta pale chini. Alivyosimama tu alipepesuka na kushika kichwa kwani bado kizunguzungu kilimshika. Alipepesuka na kuanguka.
Aliangukia mezani kwa mkuu wa shule na kufanya vitu vilivyokuwa vimewekwa katika mpangilio mzuri vitawanyike. Alizawadiwa kofi na kusukumwa Ester. Alianguka chini kidogo tu ajipigize kisogo kwenye sakafu.
Pembeni alikuwepo mwalimu fulani wa kiume, alionekana akiupeleka mkono wake ulioshika leso na kufuta chozi. Huyu ni mwalimu Herman. Alimtazama Ester aliyekuwa ameanguka na kubaki palepale chini kisha alisema.
"Jamani hata kama ana makosa lakini sio kwa adhabu ya namna hii,, naye ni binadamu anasikia maumivu" alisema huku walimu wote wametulia wakisikiliza wakati huo Janeth aliruhusiwa kuondoka.
"Kwahiyo unatetea uovu???" alikuwa mkuu. Aliuliza kwa hasira hadi mwalimu Herman akanyong'onyea ila alijiwekea ahadi ya kumsaidia Ester.
Majadiliano yalifanyika, walimu wengi walikuwa wanahitaji Ester afukuzwe shule kabisa. Mwalimu Herman alijitahidi kwa uwezo wake kuwashawishi walimu hata kuomba msamaha kwa ajili ya Ester ili tu asamehewe.
"Mimi ni mlezi wa chama cha TYCS , mimi namfahamu Ester tabia hizo hana, Ester anamtumikia Mungu kwa uwezo wake wote hivyo hilo jambo hawezi kufanya"
Mungu si athumani, ile mipango ya kumfukuza shule ilifutwa. Ester alifurahi japo alikuwa anaugulia maumivu makali sana ya fimbo.
★
Majira ya saa moja usiku Ester na mwenzake walikuwa nyumbani. Kama kawaida hakukuwa na mazungumzo yoyote yale.
Ester alivumilia na kushindwa hivyo aliamua kumvaa Janeth kwa maswali.
"Hivi Janeth nimekukosea nini?? Umefanya nimeharibiwa usichana wangu mimi, bado hujaridhika, umeamua kunizushia uongo shuleni,, nimekukosea nini mimi???" aliuliza huku analia. Janeth hakujibu chochote.
"Nijibu ubaya wangu uko wapi kwako???"
"Ester wewe ulitaka nipigwe,, ulitaka nikatae ili nipigwe na walimu???"
Walizozana ilibaki kidogo kupigana.
★
Miezi miwili ilipita huku amani ikitoweka kati ya Ester na Janeth pale wanapokaa.
Kila mmoja alijua lake ikiwemo kujiandaa alivyojua mwenyewe dhidi ya mtihani wa kidato cha sita, maana ni miezi miwili imebaki.
Siku moja wakiwa shuleni ghafla kengele iligongwa. Ilikuwa saa 5 asubuhi. Wanafunzi wote walikusanyika hata hivyo wavulana waliambiwa waendelee na majukumu mengine, kidato cha tano na wenyewe waliambiwa vivyo hivyo wakati wasichana wa kidato cha sita walitakiwa kuingia kwenye chumba fulani.
Hii ni siku ambayo hatokaa aisahau.
Kule ndani ya chumba walikuwa wanapimwa ujauzito. Ester alikutwa na ujauzito wa miezi miwili.
Wale walimu waliokuwa wanataka Ester afukuzwe walipata cha kusema. Minong'ono ilitambaa chini kwa chini mwisho shule nzima ikafahamu hizi taarifa kwamba Ester ni mjamzito.
Licha ya Ester kufahamu kwamba kuna siku alifanyiwa ukatili lakini hakutegemea kama itakuwa hivyo,, alidhani ujauzito hauwezi kuingia ndani ya siku moja tu tena siku ya kwanza kushiriki tendo.
Ester alipata mshituko mkubwa mno siku hii, pale alipokaa alihisi anakuwa mwepesi kiasi cha kuweza kuruka. Alijiona anaelea hewani, mara kadhaa alijishtukia na kujitikisa ili akili ikae sawa. Masikini Ester akili ilivurugika kabisa. Hakuwa na uhakika juu ya uhalisia wa haya aliyoambiwa, alihisi ni ndoto na pengine baada ya muda ataamka kutoka usingizini.
"Ester Valency anahitajika ofisini kwa mkuu wa shule" alisema kijana mmoja wa kidato cha tatu. Ester alikuwa darasani kwani baada ya kupimwa waliingia darasani. Alisimama akiwa na hofu, Miguu ilitetemeka kidogo amuangukie Juma aliyekuwa amekaa meza ya mbele yake.
"Kuwa makini bwege wewe"
Ester hata hakusikia,, alizama katika mawazo yaliyompeleka mbali sana.
Alihisi kuchanganyikiwa maana hata ofisi yenyewe aliisahau, aliingia kwenye 'staff office' ofisi ya walimu wote. Aliwakuta baadhi ya walimu. Aliwasalimia lakini hawakumjibu chochote. Alitulia kwa sekunde kadhaa kisha alisema.
"Nimeambiwa mkuu ameniita" walimu walimshangaa.
"Umeanza kuchanganyikiwa wewe si bure, kwahiyo ofisi ya mkuu ni hii???" Alisema Mwalimu fulani wa kike. Jambo hili lilifanya wote wacheke.
Ester alipatwa na aibu isiyoelezeka, kugeuka aondoke alishindwa, kusimama hapohapo alishindwa alibaki tu anahisi kama mahali alipokanyaga ardhi inanyanyuka, inashuka kisha kama inazama hivi.
"Hebu toka pumbavu unachafua hali ya hewa"
Ilikuwa ni kauli ya kuumiza lakini kwa Ester ilimsaidia maana bila hiyo asingeweza kutoka pale.
Ester alikutana na Mwalimu Herman pale mlangoni.
"Ester!!!!!" Aliita mwalimu Herman kwa namna ya kushtuka hivi.
"Abe Sir" alijibu Ester akiwa kama hajiamini. Aibu ilitawala uso wake, aliinamia chini.
"Unaelekea darasani???"
"Hapana mwalimu naenda kwa mkuu"
"Hebu ukitoka huko njoo unione" alisema mwalimu Herman na kuingia ofisini. Ester Alihisi kuchanganyikiwa zaidi. Aliona mambo yanaanza kumuelemea na kumzonga.
Alijaribu kutuliza akili kidogo, ilipotulia alielekea ofisini kwa mkuu. Kufika tu alianza kushambuliwa kwa maneno kutoka kwa mkuu.
"Binti mjinga wewe!!! mnafanya tabia chafu huko, mambo ya kikubwa basi mnajiona mmekuwa kupita hata sisi walimu wenu. Nimekuita muda mrefu ila unaanza kujivuta vuta kama mzee" alifoka mkuu.
"Mkuu hata usiumize kichwa sana, ngoja kwanza tumfundishe heshima kidogo." alisema mwalimu Frank na kuchukua fimbo mbili zilizokuwa kwenye kona ya jengo la ofisi.
"Lala hapo!!, lala chini hapo" alitoa amri mwalimu Frank. Ester alishangaa kusikia alichoambiwa maana kwa kawaida wasichana huwa wanapigwa mikononi na sio kwenye makalio kama wavulana.
"Usinipotezee muda lala hapo" alisema kwa hasira, alimshika kisogo na kumpiga Ngwala. Ester alianguka chini na bahati mbaya mdomo uligonga sakafu. Damu zilitoka lakini hakuna mwalimu aliyeonesha kujali.
Bakora sita za nguvu zilipigwa kiunoni kwa Ester.
Ester alilia sana. Alilia mno alitamani hata angekuwepo wa kumtetea lakini. Hakuwepo.
"Ndio muache kiburi wapumbavu nyie. Mnaifanya shule ionekane danguro la makahaba na watu wasio na nidhamu. Mnatudhalilisha. Haya inuka hapo" alisema mkuu aliyekuwa amechukia sana.
"Miezi miwili iliyopita tulikuuliza sana na uligoma kweli kweli, haya huo ujauzito umeshushiwa?" aliuliza mwalimu David,, Ester alikuwa analia tu hata kusema hakuweza sababu ya kilio.
"Unaulizwa huo ujauzito umeshushiwa??
Haya mmeona walimu niliwaambia huyu amekomaa katika mambo haya, tunamuuliza hajibu chochote ametulia na tumbo lake" alisema madam aliyeitwa Marry.
Walipoona Ester hajibu chochote walimpiga sana kwa madai ana kiburi.
"Mimi siona hata haja ya kuendelea kuongea kuhusu yeye, huyu ni wa kufukuzwa shule tu. Unafikiri atasoma shule ya nani na hiyo mimba yake. Hapo hakuna namna nyingine hata wakimtetea tena maana walimu wengine ni kama wapuuzi tu wanatetea ujinga na ushenzi" alifoka mwalimu David.
Mkuu alirudi mezani na kuanza kuandika barua.
"Nenda darasani tutakuita sio muda mrefu"
Ester alitoka huku analia. Alipiga hatua tano baada ya kutoka ofisini ghafla alisikia sauti kali.
"Wewe si nilikwambia unione ukitoka huko" alikuwa mwalimu Herman.
ITAENDELEA.......
Mara unaweza kuona ni fupi wakati wa kuisoma lkn ni refu sana wakati wa kuandika, tuonane usiku katika muendelezo wake. 😂😂🏃🏻♂️
Tags
simulizi