TAHADHARI ⚠️ KATIKA TOVUTI /APP HII HAKUNA SEHEMU YA KULIPIA ONLINE UKIHITAJI MWENDELEZO WA SIMULIZI BONYEZA HIYO BUTTON YA WHATSAPP AMA ANGALIA NAMBA YA MTUNZI WA SIMULIZI HUSIKA KATIKA SIMULIZI HIYO

NISHIKE MKONO 01

NISHIKE MKONO 😥🙌
SEHEMU YA KWANZA.
Kabla sijaolewa nilikuwa naona kuolewa ni jambo moja la fahari sana katika maisha, na pia niliamini kuwa mpaka mtu umeolewa basi ni kwamba unapendwa sana ndiomana mwanaume kaamua kukuweka ndani kwake kabisa, nilikuwa natamani sana kuolewa kuliko kitu chochote katika dunia hii, kuliko hata kusoma yani ndoto yangu kubwa katika maisha ilikuwa ni kuolewa nilijua nikishaolewa basi itakuwa naweza kutimiza kila ninachokitaka katika maisha.
Niliona shule ndio kikwazo kimoja wapo cha kufanya mimi nisiolewe mapema wakati nilipenda niolewe ili niweke heshima nyumbani kwetu na pia kuwa na maisha yangu na mume wangu kama wanandoa wengine wanavyofanya, sikutaka kuwa kama dada zangu wawili waliotangulia ambao wenyewe wamezalia nyumbani bila ya ndoa, kwahiyo nilijichunga sana na kujilinda ili mume wangu aje kufurahia kuwa na mimi.
Nakumbuka  ni vijana wengi sana waliokuwa wananifuata na kutaka kuanzisha mahusiano na mimi ila kwavile naelewa uongo wa vijana, nilijitahidi kuwakwepa sana. Dada yangu Mariam sasa ndio kila leo alikuwa akiniletea habari za vijana wanaonitaka kimapenzi,
“Mdogo wangu, yule Mangi ana hela mkubalie wewe usiwe mjinga”
“Hivi dada unajua kama bado nasoma?”
“Najua ndio, kwani unafikiri mwisho wa kusoma ni nini?”
“Sijui”
“Mwanamke yake ni ndoa, yani mwanamke kawekwa kwaajili ya kuolewa kwahiyo usiseme unasoma na mwisho wa kusoma kwako ni kuolewa, ni heri upate mume mapema uolewe, hao wanaosoma sana ndio ambao wanaishia kulia wakiwa na umri mkubwa na hakuna hata anayejitokeza kwa bahati mbaya kwao akitaka kuwaoa”
“Ila ngoja nimalize shule dada”
“Au unaogopa kubeba mimba kama mimi nikiwa kidato cha pili? Ila si umeona sasa, mwanangu ni mkubwa, ninamtuma chochote nitakacho, huoni raha hiyo?”
“Ni raha ndio ila ni kumsononesha mtoto maana hana baba”
Hapa ndipo ambapo huwa nammaliza nguvu dada yangu Mariam, yani yeye ukimwambia tu mtoto hana baba basi huwa anaishiwa nguvu kabisa ukizingatia ni kweli mtoto wake huyo hana baba sababu mwanaume aliyempa mimba alikataa na kukimbia kabisa, kwahiyo ni sawa tu na mtoto asiyekuwa na baba.
Ila swala la kuolewa hapo nilikuwa nalitamani sana, yani ndio kitu nilichokuwa nakitaka asubuhi, mchana, jioni. Sikutaka kuwaumiza wazazi kwa kuzaa mtoto asiyekuwa na baba, nilitaka niwe mtoto mwema na nizalie ndani ya ndoa, pia nilitaka mume wangu ndio awe mwanaume wa kwanza kuutoa usichana wangu maana nilipata kusikia kuwa hiyo ndio sifa kubwa ya mwanamke anayejiheshimu, yani binti anayejiheshimu basi aolewe akiwa bikra, mume ndiye pekee mwenye haki ya kuutoa usichana na sio kuhangaika hovyo na wanaume wasiofaa.
Alipoondoka Mariam, mama Aliniita na kunituma dukani kwa huyo huyo Mangi, nilifika na kununua mahitaji ila Mangi alikataa kupokea hela kabisa,
“Kwanini hutaki hela yako?”
“Aaaah wewe ni mke wangu”
“Hapana, mimi sio mke wako na kama unanipenda kweli basi subiri nimalize shule”
“Sawa nitasubiri hakuna tatizo, maana mtaka cha uvunguni sharti ainame”
Nilikuwa kama naanza kumuelewa Mangi, kwani kumaliza shule kwenyewe ilikuwa sio miezi mingi sana, basi wakati naondoka kuna rafiki yangu alikuja nyuma yangu na kunishtua, nikasimama na kuanza kumsalimia,
“Nasikia huyu Mangi anakutaka?”
“Mmmh nani kakwambia? Wewe nawe mbea jamani!!”
“Kwani unafikiri unaweza fanya kitu hapa tusijue?”
“Haya, ni kweli ananitaka kasema atasubiri nimalize shule anioe”
Basi huyu rafiki yangu aliyeitwa Tina alianza kwa kucheka yani alicheka sana kisha akaniangalia na kuniambia,
“Hivi unawajua wachaga au unawasikia?”
“Wana nini kwani?”
“Ngoja nikwambie kwa kifupi, kwanza kabisa wachaga wana mtindo wa kuoana wenyewe kwa wenyewe yani wachaga kwa wachaga, halafu ukimkuta mchaga ana duka lake huku mjini jua wazi kuwa ameacha familia yake kijijini huko, lazima awe na mke na watoto huko kwao, yani huku yupo kutafuta maisha tu. Kwahiyo hata ukiwa nae atakuchezea na mwisho wa siku atakuacha kwenye mataa”
“Kheeee, kwahiyo huyu Mangi nae ana mke na watoto?”
“Ndio, tena nasikia ana watoto wanne, usimuone hivyo, wachaga wengine hawazeeki kwa haraka ila ni mtu mzima wa kutosha tu huyo Mangi, anakudanganya shoga yangu”
“Mmmh asante kwa kuniambia hata hivyo sikuwa na nia ya kumkubali maana bado nasoma”
“Si amekudanganya anasubiri umalize shule!! Tena hata usiwe unakuja dukani kwake, yani wewe nenda maduka mengine, kwani hashindwi yule kukuingiza nyumbani kwake na kukubaka”
Nilipumua kiasi, na kumwambia Tina,
“Nashukuru sana kwa hiyo taarifa”
“Haya, mitihani hiyo inakaribia umejiandaa? Au unasubiri kufeli kama sisi wengine?”
“Aaaah kichwa chenyewe kina mambo mengi hiki, itajulikana tu siku hiyo hiyo ya mitihani”
“Hizo ndio dalili za kufeli, unatakiwa kujiandaa, maisha mtaani magumu nakwambia bora hata kwenda shule. Mimi nimemaliza shule mwaka jana ila najiona kama nimemaliza miaka, nimechoka kukaa mtaani basi tu, natamani hata nipate mume niolewe”
“Mmmh inamaana kuolewa ni muhimu kuliko kusoma eti eeeh!!”
“Aaaah usininukuu vibaya, kusoma ni muhimu ila kuolewa kwa mwanamke ni muhimu zaidi, ona kama hivi nipo mtaani nachunguza hata yasiyotakiwa, nimechoka hatari. Mungu anisaidie tu nipate mume niolewe”
Tuliagana na Tina na mimi kuendelea na safari ya kurudi nyumbani ila kichwani kwangu ndio nikazidi kupata hamu ya kuingia kwenye ndoa, nikajua kama  nikiolewa basi nitakuwa nimetimiza jambo kubwa sana katika maisha yangu.

Niliporudi nyumbani, nilianza kumtania mama kuhusu swala la kuolewa,
“Hivi mama katika maisha yako ulitamani kuolewa?”
“Mwanangu ni mwanamke gani yupo yupo tu halafu asitamani kuolewa? Kila mwanamke anatamani kuolewa, ila cha msingi tu ni kukutana na mwanaume sahihi mwenye uhitaji wa ndoa, nyie watoto wetu wa siku hizi mnadanganyika sana, dada zako hao unawaona wameniletea watoto nyumbani”
“Ila mama utamjuaje mwanaume mwenye uhitaji wa ndoa?”
“Wanaume wamejua wazi kuwa wanawake wengi wanapenda kuolewa, basi na wao hutongoza mwanamke kwa gia moja ya kutaka kuwaoa kumbe ni uongo, mwanaume anayetaka kukuoa kweli, hatotaka kukifunua mpaka mtakapoingia kwenye ndoa, hao wanaume wa kuomba tunda kabla ya ndoa sio waoaji hao, wengi ni waharibifu na wadanganyifu”
“Kumbe mama!!”
“Ndio hivyo, utuletee heshima mwanangu. Hawa dada zako wamenitia aibu sana, ila wakithubutu kuleta tena mimba zingine hapa tutawatimulia mbali, siwezi kulea ujinga mimi. Nilijitunza na kujiheshimu ndiomana nikaolewa na baba yenu, nimewazaa ndani ya ndoa nyie, kwanini msifate njia zangu? Mnahangaika hangaika na wanaume wasio na mbele wala nyuma, wanaume waongo ndio mnahangaika nao, mnaacha kufikiria wanaume wa kweli mnakazana na wauongo. Unamuuliza mtu una lengo gani na huyo mwanaume anakujibu sijui, bado hatujapanga, sasa si ujuha huo jamani! Sipendi mwanamke asiyejielewa kabisa, mwanamke yake ni ndoa, na ili uheshimike kwenye jamii ni lazima uolewe na uiheshimu ndoa yako na kuitunza, usikubali ndoa ivunjike kwa ujinga na uzembe wako. Nadhani umenielewa mwanangu na wala hutotutia aibu”
“Sitawatia aibu mama, nipo kujitunza hadi leo sitaki mwanaume yoyote, nataka mwanaume wa kwanza kulala nae basi awe mume wangu wa ndoa”
“Oooh hapa kweli mtoto nimelea, namshukuru Mungu kwa kupata mtoto anayejisoma kama wewe. Usijali mwanangu hivyo ndio inavyotakiwa. Cha muhimu uolewe halafu vingine vitafuatia”
“Sawa mama”
Nilipenda ushauri wa mama pia, maneno ya mama yalinifanya nizidi kujiweka mbali na wale wanaume wakware wanaopenda kuchezea wanawake na kuwaacha kwenye mataa.

Nilipomaliza kidato cha nne, sasa nilikuwa nipo tu nyumbani nikingoja majibu, basi nikaamua kwenda kumtembelea dada binamu ambaye naye alikuwa ameolewa kama miaka miwili iliyopita, mara nyingi huwa naongea nae kuhusu maisha ya ndoa na alinieleza uzuri wa ndoa na kufanya nitamani sana huku nikimuomba Mungu mimi niweze kumpata mume.
Siku hiyo pale kwa dada binamu, kuna mkaka alifika mahali pale na alitusalimia tu na kuondoka na shemeji kufanya mazungumzo, basi dada binamu akaanza kunitania,
“Latifa, unajua yule kijana bado hajaoa”
“Mmmmh dada! Kwanini sasa bado hajaoa?”
“Huwa anasema hajampata bado wa kumuoa, halafu ni kijana anayejishughulisha sana, kama akipata mke mwenye akili kwa hakika atafika nae mbali, kwani ni kijana mwenye bahati sana ya kupata pesa”
“Ooooh basi mke atakayemuoa atakuwa na bahati sana”
“Kwanini unasema hivyo? Kwanini usiwe wewe?”
“Kheee dada!! Mimi tena?”
“Ndio, mbona una sifa za kuolewa nae, maana wewe ni mwanamke mwenye akili sana, ukimpata kwa hakika utafurahia maisha kuwa naye”
Nilitabasamu tu na kumuangalia dada binamu, ambaye alitambulika kwa jina la mama Waziri, sababu ndio jina la mtoto wake wa kwanza.
Niliongea kiasi pale na dada binamu halafu jioni yake nilimuaga na kuondoka zangu.

Nilifika nyumbani, nikajikuta nikijiwa sana na mawazo kuhusu yule kijana nikajikuta nikitamani hata awe mume wangu, ila bado nikasema usikute wakati wangu bado kwahiyo sikutaka kufikiria sana ingawa wazo la yule kijana lilinijia mara kwa mara.
Baada ya siku mbili, niliitwa na dada binamu, basi nikaenda kumsikiliza ili nijue ni kitu gani alichoniitia.
Nilipofika nyumbani kwa dada binamu aliniambia kuwa,
“Latifa, yule kijana wa siku ile ana maongezi na wewe”
Moyo wangu ulilipuka ila nikajituliza kidogo, na moja kwa moja dada binamu aliacha nafasi ya mimi kuweza kuzungumza na yule kijana ambaye alianza kwanza kujitambulisha kwangu,
“Mimi naitwa Mussa, nimeambiwa unaitwa Latifa si ndio!”
Nilitabasamu kiasi na kujibu,
“Ndio, Latifa ndio jina langu”
“Sawa Latifa, nimekupenda kweli. Nahitaji uwe mke wangu”
Nilitabasamu tu na kumwambia,
“Njoo kwa wazazi ufate taratibu za ndoa”
“Ila je, upo tayari kuolewa na mimi?”
Yani hapo sikuwa na jibu lingine ila ndio, kwani niliona kama bahati kwa kijana kukubali haraka haraka vile kufata taratibu za nyumbani wakati huwa wengi wanaanza na porojo zao ila huyu kijana alikuwa na lengo kweli la kuoa.
Basi nilirudi kwa dada binamu naye alikuwa akicheka tu na kuniambia,
“Latifa, huyu kijana toka amekuona siku ile ni amekupenda kweli anasema hata ingewezekana leo angeenda kwa wazazi kwaajili ya kufata taratibu za ndoa”
Nilifurahi kwakweli kwani ile ilikuwa ni bahati kubwa sana kwangu, nilijiona ni binti mwenye bahati mno, wakati huo hata sikufikiria kama kuna jambo linaitwa matokeo ya kidato cha nne kwani nilichokuwa nafikiria ni kuhusu mimi kuolewa na Mussa tu.

Na kweli Mussa alifata taratibu zote za nyumbani kwetu, alikuja kujitambulisha, alilipa mahali hadi siku ya ndoa ikapangwa, kisha mimi na Mussa tulifunga ndoa na ikawa ni furaha kubwa sana.
Baada ya ndoa, ndipo nilipoenda fungate na Mussa, ilikuwa ndio mara yangu ya kwanza kulala na mwanaume maana sijawahi hata mara moja, siku zote nilikuwa nikijitunza ili nimtunzie usichana wangu mume wangu.
Kwahiyo niliumia kiasi wakati akiniingilia kimwili, ila alipomaliza nilimuona kama kachukia hivi, ila mimi nilikuwa bado na aibu maana kwangu kile kilikuwa ni kitendo cha aibu, ila nilimuuliza,
“Mume wangu mbona kama huna furaha?”
Alinijibu kwa ukali,
“Nilijua wewe ni kigori kumbe hakuna kitu”
Nikamuuliza,
“Unamaanisha nini?”
Akaniangalia na kusema,
“Hivi si ndio umetoka kumaliza shule wewe? Sasa ulikuwa ukihangaika na wanaume kwa muda gani hadi mimi nikukose ukiwa na usichana wako?”
Nikamjibu kwa kusononekana kiasi,
“Ila mimi sijawahi kulala na mwanaume”
Akacheka sana na kusema,
“Kamdanganye mtoto mdogo, si ungeona hata damu hapo kitandani! Wewe umekubuhu, usijifanye hujawahi”
Kwakweli nilishangaa kwani kuna vitu nilikuwa sivijui, na nilikuwa nazungumza ukweli kabisa wa roho yangu kuwa mimi sijawahi kulala na mwanaume hata nashangaa ni kwanini mume wangu alipaniki kiasi kile. Ila sikutaka kubishana nae sana kwa kufuata mafundisho ya ndoa niliyofundwa kuwa natakiwa kuwa mnyenyekevu kwa mume wangu na kumsikiliza kwa kila anachoniambia ukizingatia bado nilikuwa mtoto, kwahiyo hata kujitetea tu sikuweza wala nini.
Tulikaa kwenye fungate kama wiki moja hivi, ila wala haikuwa na furaha kama ambavyo nilitegemea kuwa ingekuwa ni furaha.

Baada ya fungate tulirudi kukaa kwenye chumba alichokuwa amepanga, sasa hapa ndio maisha ya ndoa kwangu yalianza rasmi, nilianza kufanya vile nilivyofundwa, kuwa mume akirudi nimliwaze, nimuimbie nyimbo, nimpikie, nimkandekande, kwahiyo nilikuwa najitahidi kwa kila hali.
Siku moja nilikuwa natoa nguo zake kabatini ili nizipange vizuri, kuna picha kama tatu zilianguka zilikuwa ni picha za mwanamke, nikashtuka sana na kujiuliza kuwa picha za mwanamke yule zinafanya nini kwenye kabati la nguo za mume wangu? Nikaziweka pembeni na kuendelea na usafi, wakati mume wangu amerudi ndipo nilipoamua kumuuliza kwa kumuonyesha zile picha,
“Mume wangu samahani, hizi picha ni za nani?”
Mume wangu alichukua zile picha huku akiwa na tabasamu la bashasha usoni mwake halafu akaniambia,
“Huyu kwenye picha ni Zawadi wangu”
Nikashtuka na kumuuliza,
“Zawadi wako?”
“Ndio ni Zawadi wangu, unashtuka nini?”
“Hamna kitu mume wangu”
Sikutaka kuongea sana wala nini kwahiyo niliacha tu lile jambo lipite kama lilivyokuwa maana niliona kama nikihoji zaidi basi naweza nikawa kinyume na mafundisho ya ndoa.

Siku hiyo usiku tukiwa tumelala, mume wangu alipigiwa simu na aliipokea na kuanza kuongea nayo, kwakweli aliongea kwa muda mrefu sana na ile simu hadi nikakereka kwakweli, alipomaliza kuongea nilimuuliza,
“Mume wangu, ni nani ulikuwa unaongea nae usiku huu?”
Alitabasamu na kunijibu,
“Aaaah nilikuwa naongea na Zawadi wangu”
“Zawadi wako!!”
“Ndio, zawadi wangu”
Sikutaka kuongea zaidi ila swala la Zawadi wangu lilikuwa likinikosesha raha kabisa, kwa kipindi kifupi nilianza kusumbuliwa kichwani na hili jina la Zawadi wangu yani sikuona kama ni jambo sahihi kwa mume wangu kuniambiwa vile.

Siku hiyo, matokeo ya kidato cha nne yalitoka hata sikufatilia kuhusu mimi ni mpaka rafiki yangu aliponipigia simu na kusema kuwa sijafaulu, ila hata sikuumia kichwa kwani mimi tayari ni mke wa mtu, kwahiyo kwangu kufaulu na kufeli ni sawa kabisa na sikutaka hata kufatilia hayo matokeo yenyewe.
Mume wangu alitoka kwenye mihangaiko yake na kuniambia,
“Latifa, jitahidi kesho upike chakula kizuri kuna mgeni anakuja”
“Sawa mume wangu”
Sikujua ni mgeni gani anakuja ila nilimuitikia vizuri kabisa.
Kesho yake, mume wangu alinipa hela nikanunue nyama kilo nzima nipike ndizi nyama huku akidai kuwa huyo mgeni anapenda nyama sana kwahiyo nikimpakulia nimpakulie nyama za kutosha, nilikubali na kwenda kununua ndizi na ile nyama kisha nilianza kupika. Sikutaka mume wangu aambiwe kaoa mwanamke mzembe asiyejua kupika, kwani siku hiyo nilihakikisha nafanya ufundi wote kwenye zile ndizi, niliziweka hadi nazi na zilipoiva nilipakua kwenye hotpot na kuweka mezani kabisa ili mgeni akija apate kula.
Mume wangu alikuwa yupo ndani tu, mara kidogo akaniambia kuwa anaenda stendi kumpokea huyo mgeni wetu, basi nilitulia nyumbani nikimngoja huyo mgeni kwa hamu zote.
Baada ya muda, mume wangu alirudi akiwa ameongozana na mwanamke, nilishangaa sana kuwa mgeni mwenyewe ni mwanamke, ila nilimkaribisha vizuri sana, mume wangu alianza kunitambulisha pale,
“Huyu ni mke wangu anaitwa Latifa”
“Oooh nafurahi kumfahamu”
Alisema yule mgeni, kisha mume wangu aliniangalia mimi na kuniambia,
“Latifa, huyu mgeni ndio yule ninayekwambiaga kuwa ni Zawadi wangu, huyu ni mwanamke wa maisha yangu, nampenda sana mwanamke huyu”
yani nilihisi mwili kupatwa na ganzi gafla, nilijikuta nikikosa nguvu kabisa.

Itaendelea….!!!

Full shilingi 1000

kslprojects

kslprojectstz@gmail.com Entrepreneurship Power

Post a Comment

Previous Post Next Post