Je Umekuwa Ukikumbwa Na Hofu Maishani Mwako? Hizi hapa Ni Sababu Ambazo Hupelekea Hofu...
___________________________
Kwa mujibu wa kanuni ya kichocheo na matokeo inadai kwamba, "kila kitu hutokea kutokana na sababu"
Hii inamaanisha kwamba, kama hakuna sababu basi hakuna matokeo. Na, hii ni kwa sababu kila matokeo /hali hutokana na kisababishi fulani...
Hii ni sawa na kusema hauhofii tu kwa sababu unatakiwa uhofu, ila unahofia kwa sababu kuna visababishi vilivyopelekea uweze kuhofu...
Ukweli ni kwamba hofu ni kama ugonjwa ambao humfanya mtu awe mahututi, na endapo mtu huyo hatazinduka anaweza akafa katika hali ya unyonge na asifurahie kabisa maisha yake hapa duniani.
Zifuatazo ni sababu ambazo hufanya watu wengi wawe na hofu maishani mwao...
1. Kukosa Maarifa/Taarifa Sahihi…
Hosea 6:4
“…kwa kuwa umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe…"
Kama unakuwa kimwili kutokana na kile unachokula, vilevile utakuwa kiakili kutokana na kile unachoulisha ubongo wako.
Kukosekana kwa mwamko wa kujifunza kumefanya watu wengi wazidi kuwa na hofu kwa sababu ya kukosa, maarifa pamoja na taarifa sahihi.
Na, ifahamike kwamba hakuna kitu chenye nguvu kama taarifa, katika dunia tuliyonayo sasa, kwani zama hizi dunia inaendeshwa kupitia taarifa hivyo ukikosa taarifa hizo hakuna utakachokifanya, na endapo utakosa cha kufanya utajikuta ukibaki na hofu muda wote...
Ukweli ni kwamba watu wengi wanajua wanachokitaka lakini hawajui watakipataje, na kutokujua kunachangiwa na tabia ya kutokujifunza pamoja na kutokutafuta maarifa mbalimbali katika eneo husika...
Moja ya sababu ambayo huwafanya watu wengi wawe na hofu ni ukosefu wa taarifa sahihi, unapokosa taarifa sahihi maana yake hutaweza kufanya jambo hilo kwa usahihi.
Na unapokosa mbinu sahihi za kufanya jambo hilo, maana yake utaanza kuhofia juu ya ugumu utakaopata endapo utaanza kufanya jambo hilo, na ukishaona kuna ugumu utakosa uthubutu, na ukikosa uthubutu utaikaribisha hofu, na ukishaikaribisha hofu hakuna chochote kile cha maana utakachokifanya...
Friend unatakiwa kujua kwamba vile unavyojua zaidi katika jambo Fulani ndivyo na hofu inavyozidi kupungua juu ya ufanyaji wa jambo hilo, ilihali unavyokua haujui juu ya jambo fulani ndivyo na hofu ya kufanya jamboi hilo inavyoongezeka!
Kwa kusema hivyo kuna wakati mwingine unapatwa na hofu ya kufanya jambo Fulani, na si kwamba unatakiwa upatwe na hofu ila ni kwa sababu umekosa taarifa sahihi juu ya ufanyaji wa jambo hilo.
2. Historia Ya Malezi...
Aina ya malezi ambayo watu wengi wamelelewa yamewajengea hofu.
Na, ifahamike kwamba nyumbani ndiyo sehemu ya kwanza ambayo mtoto huanza kuingiza taarifa za awali kwenye ubongo wake.
Hivyo basi endapo taarifa nyingi zitakazorekodiwa kwenye ubongo wake zitakuwa ni taarifa zenye vitisho basi mtoto huyo hukua akiwa na hofu pamoja na kujiona yeye hawezi.
Kwa mfano unapokosolewa, unapodharauliwa, unapoitwa majina ya ajabu pamoja na kufananishwa na viumbe vya ajabu, unapopigwa sana, unapopokea manyanyaso ya hapa na pale, unapozuiwa kuongea, unapoambiwa huwezi kufanya jambo Fulani, unapoambiwa huwezi kuwa mtu Fulani, n.k.
Maana yake unatengenezewa hofu! kwa hiyo maisha yako yote utakuwa ni mtu wa kuhofu tu!
Na, ifahamike kwamba, huwezi ukafanya kitu kitakachokuwa zaidi ya hayo matendo unayofanyiwa pamoja na kauli unazoambiwa.
Kwa mantiki hiyo historia ya matendo ulofanyiwa pamoja na kauli ulizoambiwa wakati wa kukua ndiyo kwa kiasi kikubwa vimechangia katika kukufanya uwe na hofu.
Ili uweze kuachilia hofu hii huna budi kuwasamehe wazazi wako kwanza, kwani wao siyo Mungu.
Unachopaswa kujua ni kwamba, walikulea hivyo kwa sababu na wao walilelewa hivyo.
Endapo utaweza kuachilia msamaha basi huna budi kufuta kauli zote ulizoambiwa pamoja na vitisho vyote ulivyoambiwa, then jisemee kwamba mimi ni mtu mkuu na ninaweza...
3. Athari Za Kimazingira…
Kuna mazingira mengine hata ungekuwa ni mtu mwenye mtizamo mzuri kiasi gani bado yatakutengenezea hofu na kukufanya ujione huwezi.
Hoja inayozungumziwa hapa ni kwamba mazingira hayo yanakuwa hayotoi msukumo wowote ule utakaokusaidia uweze kufanikisha jambo lako.
Na, ifahamike kwamba mazingira ni nguvu isiyoonekana ambayo humtawala mtu kuanzia fikra zake, tabia zake, mwenendo wake, pamoja na mtindo wake wa kuishi.
Katika hali ya kawaida athari za mazingira hazikwepeki, na hii ni kwa sababu mazingira yameweza kukutengenezea hofu kwa namna mbalimbali.
Kwa mfano mazingira uliyosoma yamekuathiri, mazingira unayosali yamekuathiri, mazingira unayoshinda kila siku yamekuatahiri, mazingira unayofanyia kazi yamekuathiri pamoja na mazingira yote yaliyokuzunguka wakati wako wa ukuaji.
Ni, ukweli usio na kipangamizi kwamba kwa chochote kile unachotakiwa kufanya kitahitaji sapoti ya mazingira uliyopo, hivyo basi endapo mazingira yako hayatatoa msukumo wa kuridhisha ni ngumu sana kwako kufanya jambo hilo bali utabaki ukiwa una hofu tu.
4. Ujinga Wa Kutokujua…
Mithali 1:22
“Enyi wajinga, hata lini mtapenda ujinga?…”
Watu wengi ni wajinga kwa maana hatujui hata tunachokihofia ni nini bali tumejikuta tukiogopa tu…
Labda nikuulize kwani wewe huwa unahofia nini? Na hicho unachokihofia kiko wapi? Na, vipi kama hakipo?
Ujinga wa kuhofu pasipo kujua tunachohofia ndiyo umetufanya tuweze kuacha baadhi ya fursa zitupite kwa sababu ya kujiona kwamba hatuwezi kuzikabili fursa hizo.
Unatakiwa kujua kwamba mtu mwenye hofu ni mjinga wa yeye mwenyewe kwani hajui uwezo uliopo ndani yake, hajui anachomiliki ndani yake, hajui anaweza akafanya nini pamoja na kutokujua adhibiti nini maishani mwake.
Mpenzi ujinga ni giza na palipo na giza hapana matumaini, na kama hapana matumaini maana yake hakuna maisha.
Kutokana na hilo mtu huyo hujikuta akiishi katika hofu huku hata anachokihofia chenyewe hakijui vizuri.
My friend unatakiwa kujua kwamba, maisha siyo majaribio bali maisha ni kuishi, hivyo basi usiruhusu ujinga wa kutokujua ukuendeshe kwa maana utapotea kwenye ramani.
5. Aina Ya Marafiki Ulionao…
Mtu mmoja mwenye busara aliwahi kusema kwamba “vile utakuwa miaka mitano ijayo, itategemea na vitu vikuu viwili yaani vitabu unavyosoma pamoja na marafiki ulionao”.
Kwanini marafiki? Ni kwa sababu marafiki hushawishi akili yako, na kwa sababu akili yako inajua jinsi ya kuendana na wengine basi utajikuta ukiitikia kufanya kile ambacho marafiki zako wanakifanya, na huwezi ukafanya kinyume na kile wao wanakifanya kwa maana hutaendana na tamaduni zinazotawala uhusiano wenu.
Kwa mantiki hiyo Endapo marafiki zako watakuwa ni watu wa kuhofu, waoga na wenye wasiwasi nawe utajikuta ukitengenezeka na kuwa kama wao walivyo.
Na, ndiyo maana wahenga walisema kwamba “ndege wanaofanana huruka pamoja”
Unachotakiwa kujua ni kwamba, kuna watu wengine wana hofu si kwa sababu inatakiwa waogope ila ni kwa sababu marafiki walionao wamewafanya wajihisi hivyo.
Zaburi 1:1
“heri mtu yule asiyekwenda katika shauri la wasio haki; wala hakusimama katika njia ya wakosaji; wala hakuketi barazani pa wenye mizaha”
Ahsante sana kwa kuwa mwanafamilia wa masomo haya mazuri!
Mwendelezo Wa Somo Hili Utaendelea Kwa Siku Ya Kesho...
Ndimi Emmanuel Samuel King'ung'e; Mwl. Mwandishi, Muelimishaji Katika Eneo La Maendeleo Binafsi, Life Coach And Consultant!
Unaweza Kuwasiliana Nami Kupitia Whatsapp No +255744284329 au tembelea blog yangu kwa kuandika ekingunge.blogspot.com
Tags
Elimu