TAHADHARI ⚠️ KATIKA TOVUTI /APP HII HAKUNA SEHEMU YA KULIPIA ONLINE UKIHITAJI MWENDELEZO WA SIMULIZI BONYEZA HIYO BUTTON YA WHATSAPP AMA ANGALIA NAMBA YA MTUNZI WA SIMULIZI HUSIKA KATIKA SIMULIZI HIYO

TIKTOKER 1-26

1 - 26 KIONJO
1 - 11
TIKTOKER:01
Sijui hata kama mimi ndiye ambaye nilitakiwa kuwa mmoja kati ya watakao hadithia mkasa huu, ila nipo hapa leo, nipo hapa kusema yale ambayo yamenitokea kwenye maisha yangu, yale ambayo nimeweza kuyafanya tena kwa kufurahia bila hata majuto na hata sikuwaza hata mara moja kama yanaweza kunipitisha kote nilipopita na kufanyika shule kwa wengine wanisome ili niweze kuwafundisha ya kuwa hawapaswi kupita kule mimi nimepita.

Wakati mwingine huwa nakaa nafikiria sana, nafikiria hizi lawama zote nimwage juu ya kichwa cha mama yangu, zimtese, zimfanye vibaya mpaka nafsi yangu ifurahie kwasababu alikuwa ni yeye anayechochea kila ambalo mimi nafanya, mama yangu hajawahi kuwa mkali kwangu, hajawahi nionya wala nifokea kwa jambo lolote tena wakati mwingine ni yeye ambaye alikuwa ananitetea nikikosa, yeye alisimama kifua mbele akisema “umkome mwanangu, tena usithubutu kumsemea vibaya wakati mimi mama yake nipo hai. Hawezi kufanya hivyo kamwe, kamwe hawezi.”

Unafamani kuniuliza mimi ni wa pekee nyumbani kwetu, hapana sio wa pekee, nina ndugu zangu kama dada yangu, na kaka yangu. Wote hawa wamesimama imara sana kuhakikisha nakuwa sawa kwenye maisha yangu ila nani atabishana na mama yake, neno la mama kwetu ni sheria. Hata wakinisema mama utasikia anasema “ina maana mna mashaka na malezi yangu, mnanifundisha kulea mimi, huko kote nilipolea hata mmefika hapo mlipo ni ninyi mmenifundisha si ndiyo?”

Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo, mimi nililelewa hivyo na mama yangu. Kuona kosa ni sawa, niliona sihitaji ushauri, sihitaji mawazo ya mtu. Kila ambacho mimi ninakifanya ni sahihi, hakuna cha kupunguza wala kuongezea haijalishi kina madhara gani kwenye maisha yangu basi mimi Cynthia ningefanya bila shaka wala mashaka.

Nakumbuka sana, tangu nilipokuwa kidato cha kwanza, nilianza kujiona mwanamke tayari, ninakumbuka vizuri sana. Wakati huo tayari nilikuwa nina mahusiano tena sio na mwanafunzi mwenzangu, hapana tayari mtu mzima kwangu na alikuwa na familia yake mimi sikuwa najali, zaidi nilikuwa nafurahia matunzo na zawadi ninazopewa.
TIKTOKER:02
Nilianza kupendeza hapo, nilianza kurudi nyumbani na zawadi nzuri, kuna wakati hata nilipita buchani nikanunua na kurudi nayo nyumbani ili kumfurahisha mama yangu. Mama yangu aliponiona na nyama alitabasamu kwa furaha akiniuliza “eemh Cynthia mwanangu umepata wapi pesa?”

Nilitabasamu na kusema “mama yangu mzuri, kuna mtu amenipatia nikaona nyumbani hatuna chakula hivyo nikaamua ninunue nyama tuje kula.”
Mama alinitazama akisema “mimi ndiyo maana nakupenda mwanangu, unajali sana familia yako.”

Dada yangu aliyekuwa pale jirani akamuuliza mama “ina maana mama hutomuuliza huyo mtu ni nani?, na inakuaje mtoto mdogo namna hii akaleta chakula nyumbani na wewe mama unapokea bila hata maswali.”

Nakumbuka nilimtazama mama yangu na kisha mama alimtazama dada na sura ya kukasirika sana akisema “mtoto mpumbavu sana wewe, ningekuwa mpumbavu mngefika hapo nakuuliza, kwahiyo unanufundisha kila kitu. Ndiyo maana mtoto mdogo amewashinda watu wazima akili. Wewe lini umewahi leta hapa hata pipi tu ya 50. Mtu mzima upo tu nyumbani unasubiri mimi niwapeleke chooni maana hamna faida yoyote. Mtazame kwanza.”

Niliona machozi kwenye uso wa dada yangu baada ya maneno ya mama yangu, dada hakuweza hata kusema kitu zaidi alimtazama mama na kunitazama mimi akainuka kuelekea chumbani. Mama alinitazama akavuta pumzi akitabasamu na kusema “mwanangu, njoo tupate kukatakata sisi tutenge nyama yetu tule, tena ilivyo nzuri sijui tuifanye mchemsho.”

Nilicheka tu na mama yangu huku nikisema “mama umemkomesha dada, ananionea sana.”
Mama yangu ananiambia “nani atakuonea mwanangu nikiwa hai, hakuna, hakuna kabisa.”

Haya yalikuwa ni maisha ya nyumbani, tena sio sasa tu hata enzi za uhai wa baba yetu, maisha yalikuwa ni zaidi ya haya. Mama yetu ndiyo sauti yake ilikuwa amri, baba hakuwa na kauli hata kwa baba. Mara zote baba yetu alikuwa ji mnyonge sana, hawezi hata kutukalipia tukikosa, akithubutu ni ugomvi na mama yetu. Baba hakuwa anathubutu kunisema lolote mama akiwepo.

TIKTOKER:03
Mama anamuwakia baba akisema “huyu mtoto mimi ndiye niliyebeba tumboni miezi 9, unajua uchungu wa kuzaa wewe. Muache mwanangu mtazame kule.”
Baba aliishia kuwa mnyonge sana, baba alikuwa ananyamaza tu na kuonekana amekosa furaha muda wote.

Unajua mama kuna wakati hakumpa baba yetu chakula, tulipika mchana, kama baba hayupo tunakula chakula chote. Baba akirudi akiuliza chakula mama anamwambia “leo hujaacha pesa hatujala.”

Baba anabaki na huzuni, au labda dada yangu ambaye hakuwahi penda tabia za mama amfichie baba chakula na mambo kama hayo. Baba yetu mara zote hakuwa na furaha, hata akiniona nimekosea atanitazama tu.

Rafiki yake mkubwa alikuwa ni dada na sio mimi kwasababu mimi ni kipenzi cha mama yangu. Natamani niwaambie watu kwenye familia ya kuwa haya sio malezi, huku sio kumpenda mtoto, huku ni kuharibu maisha ya watoto wetu.

Natamani niseme malezi ni baba na mama, mama hutakiwi kumfanya baba wa watoto wako mnyonge, hata kama sio aliyebeba hiyi mimba ila mmeshiriki pamoja safari yenu na ni mimba yake. Mpe haki yake kama baba, na mfanye ajisikie kichwa cha familia yake, acha kumiliki nafasi isiyokuwa ya kwako.

Niliendelea na tabia ya kubeba baadhi ya majukumu ya familia. Kupitia wanaume kama vile kumlipia mama baadhi ya madeni yake bila yeye kuhoji tena wakati mwingine anasema “Cynthia mwanangu, nimeona kitenge kizuri sana kinakopeshwa. Nikope mwanangu utanilipia?”
Natabasamu nikisema “chukua mama tutalipa tu.”

Dada yangu akisikia hayo anasema “mama hayo sio malezi unamuharibu mtoto, inakuaje mtoto mdogo alipe pesa ambayo mama yake hawezi kulipa.”
Mama atasonya hapo na kusema “kaa mbali na mambo yetu, ndiyo maana huolewi wewe una mdomo sana mtazame vile alivyo.”
Mimi nakuwa nacheka tu. Hapa natamani niseme mimi na mama yangu letu moja ila nashindwa kwasababu sikuwa nimefika kumuelezea mambo yangu.

TIKTOKER:04
Nilipokuwa kidato cha pili baba yetu aliugua na kufariki. Hapa tulisikia mengi sana. Msibani watu wa karibu na majirani walikuwa wakimsema mama yetu ya kuwa anajifanya analia wakati ni unafiki tu, baba wa watu amemtesa sana. Mama wa hovyo kabisa huyu. Amemuua mumewe kwa tabia mbaya zake, hakuwa na furaha yule baba muache tu akapumzike.

Nakiri wazi, ni kweki baba alikuwa ni mpole sana kwa mama ila sikuwahi mchukia. Nilimuogopa kama baba, nilimuheshimu kama baba. Kuna ujinga wangu sikutaka kufanya mbele ya baba yangu na kitu nilikuwa sipendi ni kusikia wanazozana na mama akimfokea baba huku baba akiwa mnyonge.

Nilikuwa naumia sana moyoni huku nikiona mama anazidi sasa kumfanya baba mnyonge. Nilikuwa nikijisikia vibaya. Basi maneno ya majirani zetu pale msibani yalinifanya nimkumbuke baba yangu.

Nilikumbuka ile siku nimechelewa kurudi, yaani nilikuwa nimetoroka nyumbani usiku, nilipokuwa nikitoroka naacha mlango wazi ili iwe rahisi kwangu kurudi alfajiri. Unaweza hata kushangaa nawezaje kufanya hivyo nyumbani kwa wazazi wangu ila mimi niliweza na wala haikuwa ngumu kwangu, kitu ambacho sasa hivi ninatamani kurudisha siku nyuma na nisiwe mimi ambaye nimefanya hivyo ila siwezi.

Hiyo siku sasa nilitoka vizuri, nikaenda kwa mpenzi wangu huko kufanya ushetani wangu. Huku familia yangu ikijua nipo sehemu salama nimelala kumbe maskini mpumbavu mimi nipo nahangaika na dunia.

Sasa wakati wa kurudi ni wazi baba wakati natoka aliniona. Nilirudi kwa kunyata sana kuhofia kusikika. Tena namna nilikuwa nimevaa kwa huko wilayani kwetu kuvaa vile ni mtu ambaye ameshindikana sana lakini mimi Cynthia niliweza kuvaa.

TIKTOKER:05
Ile nimenyata, nimenyata nikaingia mpaka ndani. Ndani giza nene, halafu nilikuwa na kisimu kidogo hakuna mtu anakijua pale nyumbani.

Nikawasha tochi. Naanza tu kupiga hatua kuna namna huwa wananiita nikasikia sauti ya baba akiita “Sinti!!!”
Nilishtuka kupita kiasi, nilishtuka sana. Baba yangu aliinuka na kuwasha taa.

Yale mavazi niliyokuwa nimevaa hata aibu kumtazama baba yangu, baba alinitazama kwa muda nikiona namna amefadhaika na aliniambia kwa upole “nenda kavae vizuri mwanangu kisha uje nataka nizungumze kidogo na wewe.”
Kwa aibu niliinamisha kichwa, nikaingia chumbani kwa kuchoka, na nilipofika chumbani nilishusha pumzi ndefu na kisha nilivaa vizuri na kutoka.

Nilipoketi baba alinitazama na kutabasamu akisema “nisamehe nimekusumbua mwanangu.”

Nilitabasamu tu kwa aibu maana najua nililofanya. Kisha baba yangu alinishika mkono akisema “mwanangu wewe ni mzuri sana. Ni msichana mrembo kwelikweli. Mimi baba yako ninaweza kukuambia hilo. Lakini mwanangu mzuri hii dunia uzuri sio kitu kama huna kitu cha ziada.

Unajua mwanangu kwa umri wako sasa hivi hakuna mtu anaweza kukuoa, hakuna mtu ana malengo na wewe kwasababu wewe bado ni mdogo. Haya unayofanya leo hukupaswa kuyafanya sasa hivi binti yangu.

Upo kwenye wakati usio kuwa wako. Kwasasa wewe ulipaswa umelala au umeamka kujisomea. Muda ukifika utafanya hayo tena kwa uhuru. Tazama mwanangu, namna ulivyo mdogo hata inabidi utoroke nyumbani kwetu usiku, na usiku ni hatari sana kwako. Mwanaume anayekupenda kamwe hawezi kukufanyia mambo hatari kama haya tena ukiwa na umri mdogo namna hii. Hakupendi wewe bado mdogo unapaswa kuwa shule tu.

Lolote linaweza kukukuta huko na sisi tusifahamu kwasababu tunaamini upo nyumbani. Sitaki kuzungumza sana usiku huu ila nataka kusema mimi baba yako kitu pekee naweza kukupa ni elimu. Hata kama hutopata kazi ila itakutoa ujinga mwanangu. Soma, soma binti yangu ili kesho na kesho kutwa ujue kutofautisha. Natamani nikuone pazuri binti yangu.

TIKTOKER:06
Dunia hii haina huruma na wasichana wazuri, tena wazuri kama wewe. Wanakutumia vile wanavyotaka, wanakutafuna vile wanavyotaka, wanakugeuza vile watakavyo, watakubinua na kukupiga danadana kisha wanakutupa mbali sana, mbali mno hata huwezi kurudi pale ulikuwa awali, na uzuri wako ukiondoka, kurudisha heshima yako ni kazi sana, na hii itakukuta kwasababu unaacha hisia zikuongoze na kuweka kando akili yako nzuri na hekima za Mungu mwenyezi zikuongoze.

Muda ukipita unapita, wazuri na warembo wanazeeka na kufa, tumia muda wako vizuri sana usiache kufurahia maisha yako kama mtoto, usiruke utoto wako na kukimbilia ambayo hata dada yako hayafanyi. Jitunze, jipambanie, mwanamke ni hekima, mwanamke ni usafi wa mwili na roho yake, mwanamke ni upendo, mwanamke ni furaha na salama.Nakupenda sana mwanangu, nenda kapumzike.”

Maneno ya baba yangu pale msibani yaliniongezea uchungu sana moyoni, kwanza baba alinitunzia siri yangu, hata mama yangu hakumwambia lilibaki kuwa kati yetu. Na sasa baba yangu hayupo. Hayupo na hajawahi kujua hata kama ninampenda sana, na napenda sana mambo ambayo sisi wawili tulikuwa tunazungumza. Nilikuwa naumia sana.

Baada ya baba kufariki mambo hayakuwa mazuri sana. Mama yetu ni kama alikuwa anazidisha sasa, wanaume ambao ni vijana umri wetu mama alikuwa anatembea nao, watu wazima pia mama hajifichi kitu ambacho hata sisi watoto hatukuwa tunapenda.

Nakumbuka siku moja kaka ambaye haishi pale nyumbani alikuja na kutuita mimi na dada yangu na wakati huo mimi nikiwa kidato cha tatu. Nakumbuka kaka aliuliza “dada zangu mnasikia yanayoendelea kumuhusu mama yetu?”

Mimi kipenzi cha mama ndiyo nilisema “kusema kweli ni aibu sana, mimi hata kukaa nyumbani sitaki tena, najisikia vibaya sana.”
Dada naye alisema “kaka nafikiria hata kuondoka hii wilaya niende mbali kabisa na hapa, maana hata kutazama watu ni aibu sana.”

TIKTOKER:07
Kaka alitutazama na kusema “ninyi ndiyo mabinti zake, nawaomba sana dada zangu mkae na mama mzungumze naye pengine anaweza kuwaelewa kuliko mimi mtoto wa kiume.”
Tulitazama na wote tuliona ya kuwa kaka yupo sawa, inatupasa tukae na tuzungumze na mama yetu.

Kweli kaka aliaga na kuondoka akisubiri majibu kutoka kwetu. Na ndivyo ilikuwa sisi jioni tulikaa na mama na tulimwambia kwa upendo haswa mimi ambaye nikiingia chumbani kwake nakuta nguo za mwanaume mwingine mbali na baba.

Nilisema “mama yetu sisi tunakupenda ila sio tabia nzuri hizi tunaona na kusikia. Ndani kwetu unaleta wanaume tena kwenye chumba cha baba wanaacha na nguo, leo huyu kesho yule, unafikiri baba anajisikiaje huko alipo bora hata ungefanya mambo haya mbali.”

Mama alinitazama machozi yalianza kumwagika. Alilia sana na dada yangu alisema “wewe ni mama yetu, tunajua mwili wako pengine unadai tusamehe kwa kusema haya. Lakini mama huna sababu ya kutuonesha waziwazi. Tena mama vijana wadogo wanataka sisi tuwaite baba.

Bora hata ungechagua mwanaume mmoja wa umri wako mama, tena ni mapema sana baba yetu hata hajaoza vizuri wewe tayari unafanya mambo yakushangaza huoni unatutia aibu mama, acha, acha ni aibu.”

Mama alilia sana tena machozi mengi akisema “ina maana wanangu mnaona mimi sifai leo, mnaona mimi malaya. Kwasababu mume wangu hayupo sasa si ndiyo na ninyi mnaungana na ndugu na majirani kunisimanga kuwa mimi nina tabia mbaya. Sawa tu, si nimewazaa mnitukane. Mmeungana wote mniseme mimi.”

TIKTOKER:08
Mama aliinuka akilia huku anaingia chumbani kwake bila hata kumaliza kikao na kuacha mimi na dada tunatazamana tu. Huyu ndiye mama yetu. Unaweza ukafikiri ni ya kufikirika haya, ila wakina mama kama mama yangu ni wengi sana na mimi Cynthia nilibahatika kuwa na mama wa namna hii. Ni mama yetu, ni mama yangu.

Nakumbuka nilimfuata chumbani na kumkuta bado analia. Mimi nilipiga magoti mbele yake na kusema “naomba tusamehe mama, hatujafanya kwa ubaya. Tunataka mama yetu uwe mama wa heshima kama wakina mama wengine ili na sisi tujisikie raha.”

Nilisema kuna namna huwa wanaharibu jina langu, sasa ndiyo mama yangu aliniita akisema “Sinti, unataka kuniambia mama yako sina heshima, unaniona mama yako ni mjinga sana, ni mama mpunbavu, ungekuwa hivyo leo?”

Nilimtazama usoni mama akiendelea kulia nikisema “mama nisamehe mimi na dada yangu tumekosa.”
Mama yangu alisema kwa kujilaza kitandani “nataka kuwa mwenyewe, nataka kuwa mwenyewe mwanangu naomba niache peke yangu.”

Nikaita kwa upole “mamaa!!!”
Na yeye alisema “Sintia mwanangu, ondoka chumbani kwangu tafadhali.”
Nilishusha pumzi na kumtazama mama kwa unyonge na kuanza kuondoka.

Sio kawaida yangu ila wacha nitoe tangazo fupi katikati ya stori. Hizi hadithi ni za agathadastorywriter napatikana hivyo instagram achaneni na hao wezi wa fb wanawaibia bure.

Basi nilipotoka chumbani nikarudi zangu kwa dada, dada akaniuliza “eeneh vipi?”
Nilimtazama tu dada yangu na kutikisa kichwa kuonesha kuwa mambo bado. Dada alishusha pumzi tu ya kuchoka na tulitiana moyo ya kuwa ametusikia pengine atabadilika tu.

TIKTOKER:09
Haikuwa hivyo kwa mama yetu, hali ndiyo ilizidi kuwa sio hali. Ilifika hatua nyumbani ili tule lazima tujipambanie. Dada alete hiki mwingine alete kile maana bila ya hivyo ni hatari.

Nakumbuka siku moja usiku dada yangu aliniambia “mdogo wangu kipenzi, najua nitakushtua sana ila sina budi kukuelezea. Ni heri wewe unasoma, mimi dada yako nipo tu, hivyo nimewaza sana nimeona ni vyema sasa niondoke hapa nyumbani nikatafute maisha mkoa mwingine.

Hivyo ninaenda Tunduma mdogo wangu na huko nimeongea na watu nishapata kitu cha kufanya. Ubaki vizuri na mama hapa nyumbani mengine tutakuwa tunawasiliana tu na tunapoweza tutasaidiana.”

Sikuwahi kujua ya kuwa ninampenda namna ile dada yangu mpaka hii siku. Roho iliniuma nilijikuta nalia nikisema “dada unaniacha hapa na mama kweli?, tuondoke wote dada.”

Dada alinitazama na kusema “mdogo wangu, unasoma wewe, shule ni muhimu sana kwako. Jikaze umalize baada ya hapo utakuja kwangu.”

Nililia nikisema “dada hata mimi nimechoka sana hapa, nimechoka sana haya maisha mimi usiniache dada, usiniache hapa na mama.”

Dada yangu alinikumbatia kwa nguvu sana, tulikumbatiana na mama alitukuta pale tunalia aliuliza “watoto wangu, kuna tatizo?”

Nilifuta machozi na kuacha dada aongee. Nakumbuka dada alizungumza na mama yangu alimtazama akiuliza “mwanangu ushapata kazi?”
Dada alimtazama na kujibu “ndiyo mama tayari.”

Mama alilaumu “sasa siku zote ndiyo unasema leo binti yangu.”
Dada kwa upole alisema “naomba nisamehe sana mama hata mimi sikujua, taarifa imekuja leo sikujua nitapata, nisamehe mama.”

Mama alimtazama akisema “siwezi kukuzuia mwanangu, mimi ni mama yako nakuombea baraka siku zote. Nenda kapambane mwanangu, ili uje kutusaidia na sisi. Kafanye kazi mwanangu. Sasa na wewe ndiyo unalia badala upambane na shule ukimaliza na wewe utafute cha kufanya.”

Tukacheka tu na huu ukawa mwanzo wa maisha ya wawili tu nyumbani yaani mimi na mama yangu.

TIKTOKER:10
Maisha hayakuwa mazuri sana pale kwa tabia, mama akileta wanaume nyumbani na mimi naleta wangu yeye akilala nje ya nyumba. Maisha kama mashindano mimi na mama. Yeye ana wanaume na mimi ninao na sina hakika kama hatujawahi ingiliana kwa namna ile, sina hakika kabisa.

Ilipita miezi mitatu tangu dada alipo ondoka nyumbani, mimi nilIjigundua ni mjamzito baada ya kukosa hedhi kwa miezi miwili mfululizo. Nilinunua kipima mimba kuthibitisha, ndiyo mimi Cynthia, nikiwa kidato cha tatu nilibeba mimba, mimba ambayo hata sijui baba wa mtoto ni nani kwa wakati huo.

Sikuwa najua hata mimba ni ya mwanaume gani maana ninawachanganya sana, nilichanganyikiwa. Nikiwaza aibu shule naishiwa nguvu, nikiwaza mtaani na nilivyokuwa najiona mimi ndiyo mimi natetemeka. Siku hii iligeuka kuwa ngumu sana kwenye maisha yangu, nililia sana chumbani kwangu, sitasahau kabisa hii siku.

Niliona mbali na matatizo yangu lakini bado nilitamani kuendelea na masomo yangu, bado nilipenda kusoma. Nitamwambia nini mama yangu, jamii yangu, shule nitaiweka wapi sura yangu. Ingawa moyo wangu ulikiri wazi kwamba watu walitegemea haya kutoka kwangu, wengi wanajua mimi ni msichana wa kujisikia, mama yangu hana maadili, mimi pia nimefuata nyayo za mama yangu. Nilikuwa nimejawa na woga ndani ya moyo wangu.

Nikiwa pale kitandani nalia kwa maumivu mama yangu aliingia hata bila ya hodi. Alinitazama usoni, kisha mkononi nikiwa nimeshikilia kile kipimo siwezi hata kuficha. Mama aliniita akisema “Sintia!!, usiniambia una mimba mwanangu, Sintia una mimba?”
Nilijikuta nalia nikiita “mamaa!!, nisamehe mama yangu, nisamehe?”

TIKTOKER:11
Mama yangu, alinitazama usoni na kusema “umejua kunitia aibu mwanangu, nilijua wewe utasoma unifute machozi, kumbe na wewe kukupenda kote kazi bure tu. Umenivua nguo mama yako si watu watanicheka mimi kwa kukudekeza na kukuamini wewe. Mimba?, umri huo?”

Nilijikuta ninalia tu hata siwezi kusema lolote jambo zaidi ya kulia. Baba alinisogelea na kuuliza “ina muda gani?”

Nilimtazama mama nikilia na kusema “miezi miwili mama sijaona siku zangu.”
Mama alifoka “unalia nini sasa, unalia nini nakuuliza?, haya niambie hii mimba ni ya nani?”

Nilimtazama, aibu hata kumjibu mama, kamasi zilikuwa zinanishuka nikisema “sijui mama, sijui ya nani, mama mimi sijui mimba hii ni ya nani?”

Mama yangu, alinitazama akisema “ya leo kali, hujui mimba ni ya nani?, kwahiyo unataka kusema huyo mtoto hana baba yake si ndiyo maana yake?”

Badala ya kujibu niliendelea kulia, mama alifoka akisema “ni umalaya gani huu unafanya huna akili kabisa unashindwa vipi kujua mwanaume aliyekupa mimba. Nilijua una akili sana kumbe hakuna kitu, haya sasa hujui baba wa mtoto huyo mtoto akizaliwa itakuaje, hatakuwa na baba si ndiyo?”

Nilizidi kulia tu, mama alinisukuma kichwa changu na kunisonya kwa hasira kisha alitoka chumbani kwangu akiniacha nalia tu.

Usiku ule ulizidi kuwa mchungu kwangu, hata mama aliyenidekeza sana alinikuwa ananisema kuwa sina akili kabisa, mama na yeye alitaka nisome na sio nibebe mimba sasa sijui yeye alijua pesa napata wapi. Ni makosa yake yeye mwenyewe alishindwa kuniongoza katika njia ipasayo ila ni mama sina la kufanya, nilikuwa naumia sana kubeba mimba katika umri ule na sijui ni mimba ya mtu gani.

Asubuhi ilipofika, nilichukua simu yangu nitafute wababa wa mtoto, wakati simh inaita ndiyo mama anaingia tena chumbani kwangu bila hodi, mama alisikia simu ikiita, alisema akinitazama “safi sana binti, kumbe na simu una miliki, sasa tumia hiyo simu kutafuta hao wanaume zako uliolala nao miezi hii miwili na uwaambie una mimba watoe hela tukatoe.”😂😂🙌🙌HAPPY BIRTHDAY TO ME🙏🙏🙏asantenu sana shabiki zangu, nawapendaaaaa haya nasubiri zawadi sasa😂😂

12 - 26

TIKTOKER:12
Nikashtuka na kuuliza nikiwa nimetoa macho “mama nikatoe mimba?”
Mama alinitazama akirudia maneno yangu “mama nikatoe mimba sasa unafikiri mimi nataka wajukuu wasio na baba, nani atalea?, hiyo mimba lazima tutoe.”
Nikaita kwa upole “mamaaaa!!!!”
Mama alisema “amka jiandae.”

Nilijikuta ninashika tumbo langu kwa hofu sana. Hofu ambayo nilikuwa nayo sana ndani ya moyo wangu ni kifo. Nani hajui pale shule kama ukitoa mimba tu unapoteza maisha, tumefundishwa athari nyingi sana na hii ndiyo kubwa, niliogopa sana, niliogopa kupoteza maisha yangu kwa umri ambao nilikuwa nao. Ni kweli nimekosea sana, ila kufa hapana, bado nahitaji kuishi hata kama nakabiliana na aibu mbele yangu, nitapambana niishi.

Mama alirudi tena chumbani na kunikuta bado kwenye hali ya kushika tumbo langu, ninakumbuka mama alishika kiuno chake na kuniambia “ina maana muda wote huo hujafanya kitu chochote kile?”

Nakumbuka kwa upole na huruma nyingi sana niliweza kumwambia mama yangu “mama yangu, najua nimekuumiza sana, natambua hili na najutia. Lakini mama, siwezi kutoa hii mimba nitakufa mimi, nitakufa mama, utanipoteza mimi.”

Mama alishusha pumzi yake na niliona uso wake ukiwa kwenye maumivu, alinitazama na kisha alinisogelea na aliniambia “Sinti, unajua wewe ni mwanangu kipenzi. Kamwe siwezi kukupeleka sehemu mbaya mimi.

Kiukweli suala hili limeniuma sana kama mzazi, ila mwanangu wewe bado ni mdogo, tutachekwa sana, tutachekwa sisi na isitoshe mwanangu, unatakiwa bado kusoma, unafikiri nikikuacha na hii mimba kwa umri huo itakuaje?. Mimi siwezi kukupeleka sehemu mbaya mwanangu, tukishindwa tutaacha, nimeelekezwa ni dokta mzuri sana.”

TIKTOKER:13
Nilimtazama mama yangu nikitokwa na machozi, mama yangu alijikaza sana ila bado niliweza kumuona mama anaumia. Nimemuumiza sana mama yangu kipenzi.Hapa bado dada yangu hajapata habari, anavyojua kuzungumza yule dada atanimeza, naogopa sana.

Nilijiandaa, sasa hata simu mama kaona siwezi kuficha zaidi, kichwani nahangaika kutafuta nililala na nani na nani lini tena kwa mpangilio, utasema mimi nimewahi sana, ndiyo nimewahi kuwapanga ila sio mimi tu wapo wengi hata mimi nilikuwa na wenzangu wengi tu ambao waligeuka marafiki zangu na ndiyo maana nipo hapa ili wazazi huko majumbani wajifunze kitu kutoka kwa familia yangu.

Mnapoona panapwaya, ziba usiwe kama mama yangu. Mtoto mpende sana lakini usimnyime mafundisho yako ya hekima hata kama inawezekana kutumia ukali akuelewe tumia kwa maana kuna siku huyo mtoto atakulaumu kwa kumlea vibaya.

Mimi na mama tulienda mpaka hospitali ambayo mama alikuwa ameelekezwa, tulipofika pale mama alifanya maelekezo na kukutana na yule daktari. Alitukaribisha kwa upole na kisha aliniuliza umri wangu na mimi nilimjibu. Dokta alisikitika akisema “wewe ni mdogo sana kubeba mimba, sio kama nakuhukumu sana mwanangu kwasababu kuna wengine wanakuja hapa ni wadogo zaidi yako na wanakuwa wana mimba.

Nawahurumia sana kwasababu mnaharibu kesho yenu nzuri sana. Unajua hawa vijana mnaofanya nao haya wanajua wazi wanaharibu maisha yenu na kamwe hawafikirii kuwaoa ninyi kwasababu bado ni wadogo sana. Mtoto mzuri unapaswa kuzingatia elimu, elimu ndiyo ufunguo wa maisha yako.”

Maneno haya yalinikumbusha enzi za uhai wa baba yangu, nilijisikia uchungu sana ila nitafanya nini na ndiyo nimeharibu tayari. Huyu baba alinitazama na kusema “pole sana, haya sasa panda kitandani pale na uvue ngup yako ya ndani.”

TIKTOKER:14
Nilimtazama mama na mama alinisisitiza hivyohivyo. Mama yangu mzazi anashuhudia haya yote ili tu kunilinda na kujilinda yeye mwenyewe na dunia ya nje. Hataki kuwa mama aliyeshindwa malezi yangu, hataki kuchekwa na mimi nikawa ndiyo sababu mama yangu amekataa.

Nilipanda kitandani na dokta alinifuata pale, alifanya alichotaka kunifanyia. Vyuma nasikia mpaka ndani ya tumbo langu, damu zinatoka ila huyu dokta alikuwa anashangaa kila kitu. Alipomaliza alishusha pumzi na kusema na mama yangu “haiwezekani hii, mimba imegoma kutoka kabisa. Nimetumia kila namna ila imeshindikana.”
Mama yangu alishtuka na kuuliza “kivipi tena dokta?”
Dokta aliniacha pale kitandani mimi nikiwa nimechoka huku naona kabisa naenda kuwa mama mdogo mdogo mtoto kazaa mtoto ndiyo hii.

Nakumbuka nilisikia akisema “mimba yake imeshindikana kabisa kutolewa.Nimetumia mbinu zote imeshindikana na siwezi kulazimsha zaidi.”
Mama yangu alisema kwa huruma “dokta nakutegemea ujue.”
Dokta alimtazama mama akisema “siwezi kukudanganya, nakushauri pia usiende lazimisha kutoa hiyo mimba, atakufa, muache azae pengine kuna maana yeye kuwa na mimba hiyo leo hii usitoe mimba hii imegoma.”
Mama alichoka, na kuuliza “ina maana haiwezekani kabisa dokta?”

Dokta alinitazama akisema “sio mimi tu dada, hakuna mtu anaweza kuitoa labda awe na shida sana na pesa ndiyo atafanya hivyo na utarudi nyumbani na maiti ya binti yako kwasababu atafanya ambacho si stahili.”

Mama yangu alichoka sana, alinitazama tu na mimi pale kitandani nikiwa nimepoteza matumaini kabisa ya kuendelea kuishi kwa furaha.

Mama yangu kwa kujikaza sana, aliniweka sawa na safari ya kurudi nyumbani ilianza. Nakumbuka mama njia nzima hakuwa anazungumza labisa, hakuongea hata neno moja. Mpaka tumefika nyumbani mimi ndiye niliuliza “mama sasa itakuaje?”
Mama alinitazama na huku anaingia chumbani kwake “zaa.”

TIKTOKER:15
Nilijisikia vibaya sana, mama ana hasira sana na mimi kwasababu ya hii mimba ambayo sijui baba wa mtoto ni nani.Nilimsikia mama akizungumza na simu sasa sikuwa naelewa maana nasikia upande mmoja tu ambao ni upande wa mama akijibu.

Nakumbuka nilisikia mama akisema “ndiyo imekuwa hivyo, nina maumimivu sana. Amesema tukilazimisha atakufa.”

Kisha nilisoge tena nikamsikia akisema “acha tu ndugu yangu, mwanao amejua kunivua nguo, ninaumia ila nitafanya nini acha azae tu, atakabiliana na haya.”

Nilijisikia uchungu haraka nikarudi chumbani kwangu na nikakaa kitandani, niliamua kuchukua kalamu na karatasi na hapo ndiyo nilianza kuwapanga wanaume namna nimekutana nao, alitoka huyu alifuata huyu.

Nilifanikiwa kuwapanga, ninatamani hata nitaje orodha hii lakini siwezi maana utaniona sifai mapema sana wakati ninayo mengi ya kusimulia na ya kufanya wengi wajifunze kutoka kwangu mimi ambaye nimetumika kama darasa.

Ndiyo, kuna watatu ambao mimi moyoni nilikuwa nawaza kama sio ya huyu lazima itakuwa ya huyu au huyu.Niliahidi kuwaambia hawa wanaume kila mmoja kwa wakati wake na nitaona wao wanataka nini, mimi Cynthia shule ndiyo imeishia hapa, kidato cha tatu nayaacha masomo yangu na kuendelea kulea mimba.

Nilianza kuwaambia hawa wakina baba watatu ambao mmoja kati yao ni mwanafunzi na wawili ni wafanya kazi na mwingine kati ya hao wafanya kazi ni mume wa mtu.

Huyu ndiyo hakutaka hata kusikia hizi habari. Aliniambia “toa hiyo mimba, kama huwezi kamwe mtoto asinijue, sitaki kuharibu nyumba yangu kwasababu yako.”

TIKTOKER:16
Roho iliniuma sana, nilijikuta ninalia baada ya lile jibu. Kweli kabisa baba yangu alikuwa sahihi. Kwa umri wangu kupendwa ni uongo, zaidi baada ya kutolewa bikra yangu tena na mwanaume asomaana ni kutumika mpaka niombe poo.

Hawa wengine walikubaliana na mimi ingawa na wao pia hawakuwa tayari kuwa wazazi tena na mwanafunzi walihofia maisha yao na mimi sikuwa tayari kuharibu maisha ya yeyote kati yao. Niliamua kutunza mimba, ndoto zangu, maisha yangu mimi Cynthia, hapa nyumbani ndiyo kitovu cha yote.

Niliacha kwenda shule, wanafunzi wenzangu mpaka nyumbani walinifuata kuniuliza juu ya kwanini siendi shule, nilikuwa najibaraguza tu huku naumia moyoni. Niliacha kutoka nje nikiwa huru, nilikuwa tu mtu wa kujifungia ndani kuificha aibu yangu.

Nakumbuka namna uongozi wa shule ulipoagiza watu mpaka nyumbani na bado sikukosa cha kusema ingawa walilazimisha nirudi shule na baadaye mama aliitwa kuulizwa maswali kunihusu na kuhojiwa kwanini siendi shule.

Ninakumbuka sana siku hii, mama yangu kwa kulia na kushindwa hata kuinua uso wake alisema “mnisamehe sana waalimu, mwanangu ana mimba, mwanangu amekatisha yeye mwenyewe ndoto zake za msingi.”

Waalimu walishtuka na kusikitika sana, roho yangu ilikuwa inapasuka kwa maumivu na sasa hii sio siri tena. Baada ya wale waalimu kuondoka wakiwa hoi, wamechoka kwa walichosikia, najua tu kwa walivyokuwa wananikanya lazima watakuwa wanakumbushia namna sifai.

Niimuuliza mama yangu nikilia “sasa mama kwanini umewaambia mama, kwanini?, kila mtu atajua mama nitaficha wapi sura yangu.”
Mama akanitazama na kuniuliza “unawaza kuhusu sura yako tu Sinti, na vipi kuhusu mimi sura yangu. Hii ni serikali, siwezi ongopa na huendi shule siku wakijua unafikiri itakuaje. Hiki nimefanya ni sahihi sana. Mwanangu muhimu sasa wewe kulea tu, hii ni mimba mwanangu, sio jipu. Mtoto anakua kila siku ndiyo maana tumbo nalo halidanganyi. Kubali umeshindwa binti.”


TIKTOKER:17
Ni kweli mama alivyokuwa amefanya, mimi rasmi siku iliyofuata nilipokea barua nikiwa nyumbani na mama. Na baada kupokea, aliyeileta alipoondoka tu tulifungua ile barua, rasmi mimi Cynthia nimefukuzwa shule kwa kukiuka sheria za nchi na shule yangu. Napaswa kuacha shule haraka sana.

Pamoja na yote hili sikuwahi kuliwaza kabisa na sasa ndiyo limenitokea mimi. Nilikuwa nasoma ile barua huku machozi yakinimwagika, hata mama yangu aliniuliza “mwanangu kuna nini?”

Nikalia kwa uchungu nikisema “mama nimefukuzwa shule rasmi sasa, nitakuwa mgeni wa nani mimi?”

Mama alinihurumia sana, alikuja pembeni yangu na kunikumbatia akisema “umefanya makosa binti yangu, ila hatuna budi kukubali acha kulia bado mapema sana. Jambo la heri mama yako nipo hai, umeniumiza sana ila nipo hapo kuhakikisha safari yako inaenda vizuri.”

Kwa nguvu nilikumbatiana na mama yangu nikilia sana huku nasema “nimekosa mama, nimekosa nisamehe sana mama yangu. Najua unaumia sana, nakuahidi sitakuwa mzigo kwako wala mwanangu nitapambana mama, nitapambana.”
Mama yangu alizidi kunikumbatia na kunitia moyo.

Habari zangu zilisafiri kila pande za wilaya na vile wilaya ni ndogo basi mzuri wa wilaya nimeyavaa, mtoto mrembo ana mimba, mzuri wa kijiji ameharibu mambo. Nikawa mfano mbaya mtaani, wenye watoto wao hawataki watoto wao wawe karibu na mimi, hawataki niende kwao, mimi ndiyo yule usiwe kama Cynthia si mmeona mwisho wake, usiishi kama fulani.Nilinyooshewa vidole na kuchekwa sana ilinibidi niwe nashinda tu nyumbani. Habari zangu mpaka ndugu ziliwafikia haswa dada yangu ambaye alienda Tunduma.

Dada yangu alinipigia simu ni wazi namba amepata kwa mama maana nipo huru sasa na simu. Nilizungumza na dada kwa woga namjua sana dada yangu yeye amenyooka hakwepeshi. Nakumbuka aliniuliza “mdogo wangu ninayosikia kukuhusu ni kweli?”

Nilijibu kwa upole “naomba nisamehe dada, mnisamehe wote nimekosa.”
Dafa yangu kwa huruma alisema “mdogo wangu kwanini lakini!!, haya ndiyo nilikuwa nakuonya mimi.”


TIKTOKER:18
Nitajibu nini zaidi ya kuomba msamaha nikisema “tafadhali sana dada, usiniseme tena nakuomba. Nimesemwa sana na watu, nimenyooshewa vidole na kuchekwa. Dada najutia kila kitu na nimejifunza sana kwenye hili. Nimekosa.”

Dada yangu alishindwa kufanya lingine zaidi alinitakia safari njema kuelekea kuwa mama na alinisisitiza kufuata ushauri wa wataalamu.

Namshukuru sana Mungu, familia yangu kwa pamoja ingawa niliwaumiza ila walihakikisha safari yangu inakuwa salama. Walihakikisha nakula vizuri na napata mahitaji yote. Ni dada yangu na kaka yangu walipambana sana kuhakikisha mama hazidiwi na mzigo.

Miezi 9 ikawa, familia yangu iliungana, dada yangu kwaajili yangu alirudi kunitazama. Mimi nilijifungua, mtoto wa kike mrembo kama mimi mama yake. Mgeni aliingia nyumbani kwetu.

Familia hii ambayo mimi nilikuwa naona haina maana awali kwasababu tu napendwa sana na mama. Kwasasa ninazo nguvu za kusema hakuna kitu cha maana duniani kama familia.

Upo muda wote watakuacha ila wale wa nyumbani kwako wataelewa machozi yako, huzuni yako na kila pito lako. Nashukuru sana familia yangu kwa kuona magumu yangu hayabaki kuwa kwangu pekee bali sote kama familia haijalishi watu wanaongea nini juu yetu ila ikifika usiku watalala kama ambavyo sisi tunalala na asubuhi wataamka na usiku tena watalala mpaka watakapo choka. Sijali tena najali mambo yangu tu.

Huyu mtoto alifanana sana na yule mwanaume ambaye alimkataa. Sikutaka kumlazimisha zaidi nilimuelezea ukweli tu ya kuwa mtoto amezaliwa na ni wake hata kama hakujibu ila ujumbe amepata nafsi iliniuma mwanangu kukosa baba mbali na yote ambayo mama yake nimeyapitia. Ila machozi hayakuwa na maana kama mimi nikiendelea tu kulia bila ya kupambana kwaajili ya binti yangu.

Mimi ni mama sasa natakiwa kushughulika. Nashukuru Mungu niliendelea kupambana pale nyumbani nikilea mtoto wangu huku uwezo wangu wa kusuka watu nywele ukijionesha dhahiri. Nilianza kuwa sikosi chochote kitu kwaajili ya binti yangu.

TIKTOKER:19
Nilinyonyesha na hata nilipomaliza nilimuomba mama yangu, nilimuomba nikisema “mama nakuomba sana, kubali niondoke hapa nikatafute kwaajili yetu. Ninakuahidi mama kila kitu kitakuwa sawa.”
Mama alinitazama na kuniuliza “unataka kwenda wapi lakini Sintia, mtoto mdogo huyu anakuhitaji sana.”

Nilimtazama mama na kusema “nakuelewa mama, ila hii sio kwaajili yangu peke yangu. Ni kwaajili yetu mama, mjini fursa ni nyingi sana nitakuwa ninawahudumia kwa kila kitu tafadhali mama nikubalie. Nimekuwa mtu mzima sasa najua nini nifanye na wapi nipite, nakuomba mama.”

Mama alivuta pumzi akisema “umewaza vizuri mwanangu, ila wacha nishauriane kwanza na ndugu zako kisha tutajua kitu gani kifanyike.”
Nilitabasamu nikisema “nashukuru sana mama yangu, Mungu wa Mbinguni akubariki sana.”

Wakati nasema hayo ungesikia sauti ya binti yangu ikisema “mamaaa!!, mama!!! Mamaa bebe, bebe mamaa!!”
Bibi yake alicheka akisema “huyu naye kwa kudeka haya njoo hapa mjukuu wangu mama amechoka sana.”
Alienda kwa bibi yake wakabebana na kutoka huku mimi nikiwatazama kwa tabasamu.

Nimekua sasa, ukinitazama ni tofauti na awali. Nimekua na muonekano mzuri zaidi, ninapendeza japo kwa gharama za kawaida. Siku zote kizuri cha jiuza ila sikutaka tena kutumia uzuri wangu kuwa sababu ya kuharibu mipango yangu. Sasa ninayo mipaka, mipaka ya kuniongoza kwenye maisha yangu.

Nina mwili wa kutosha na nyamanyama rundo. Kiuno kinaonekana kilipo, hips za kutosha na mengine mengi sana. Mungu ameniumba kwa uzuri, hata naweza kumsifu yeye dabali dabali(mara 2, 2). Ndiyo anastahili sifa tele, sikia ni kama vile nilimuandikia barua ya maelekezo ya kumtaka aniumbe nitakavyo kumbe ni kujitukuza yeye tu. Hakika kwangu Mungu amefanya kazi iliyo njema sana.

Baada ya wiki kupita mama yangu aliniita chumbani kwake. Mama yangu aliniambia “mwanangu Sintia, unamkumbuka yule dada yangu, rafiki yangu kipenzi mama Faraja?”
Nilitabasamu tu na kusema “nisimkumbuke tena tajiri.”

TIKTOKER:20
Mama alicheka akisema “kwakweli ndugu yangu maisha ameyapatia japo sio tajiri kama unavyosema ila kwao pesa ipo. Eenh sasa nimeongea naye, na nimemuelezea kuhusu wewe. Kashangaa sana nilipomwambia una mtoto.”
Nilitabasamu nikisema “weee kumbe hukumwambia mama?”
Mama alitabasamu akisema “nawezaje sasa mwanangu, nilikuwa na aibu sana unajua. Sasa sikia nimemuomba aongee na mume wake akusaidie kutafuta kazi kwenye maduka maduka yao huko mjini. Mama Faraja amefurahi sana na amesema ukiwa tayari tu wewe nenda atakupokea ukikaa sawa utatafuta chumba chako na watakutafutia kazi.”
Nilifurahi nikimuuliza “unasema kweli mama yangu?”
Mama alitabasamu akisema “ongea na watu uvae viatu mwanangu, ila sasa chondechonde binti, ukifika huko kumbuka una mtoto jitahidi sana kutuma visenti maana mama yako unanijua sina mume mimi ni kupambana tu.”
Nilitabasamu nikisema “mama yangu unanifahamu vizuri kwako, siwezi kukuacha unateseka niombee tu mama yangu. Na sasa tunafanyaje kuhusu nauli sasa?”
Mama alinitazama akisema “mimi tena?, ongea na ndugu zako wakuchangie sina pesa ya nauli mimi.”
Nilicheka tu, huku mama akicheka akisema “unaenda mjini mwanangu huko hakuna huruma, jipambanie, jilinde na ujitunze nafikiri unaelewa.”
Nilitabasamu tu.

Hekaheka za mimi kutafuta nauli zilianza. Ndugu zangu walinichangia nauli kwa upendo huku dada yangu akiniambia “mdogo wangu nakutakia kila lenye heri, nenda kajitume, nenda kafanye kazi. Unaenda kwenye nyumba za watu mdogo wangu. Usitutie aibu huko nenda kasaidie kazi na uwe na heshima huko.”

Niliguna na kusema “unataka kusema mimi mvivu na sina adabu dada?”
Dada yangu alicheka kidogo akisema “hapana mrembo wetu wala sina maana hiyo ila tu lazima kama dada nikukumbushe kuhusu maisha kwa ujumla.”

Nilitabasamu nikisema “nashukuru sana dada, Mungu akubariki sana na asanteni kwa kuwa nami kwenye kila hali hamjaniacha.”

Hakika nilikuwa na bahati mbali na yote haya nilikuwa na familia, familia ambayo imejua kusimama na mimi na kunijali mbali ya kuachwa na mimba na bado mtoto wangu wanamtazama

TIKTOKER:21
Nilijiandaa vizuri na safari na muda ulifika wa kwenda huko Mjini Dar kwa mama Faraja ambaye ndiye mwenyeji wangu. Nilifurahia kila kitu kusema kweli, na niliondoka kwenye wilaya yangu mpaka mjini. Nilipokelewa na huyu mama kwa furaha sana. Alinichukua kwa upendo mpaka nyumbani kwake. Mama huyu ni mama mwenye upendo sana, ni mama mwenye huruma na utu sana. Hakika nilifarijika kuwa mgeni wake.

Nyumba yake kubwa na nzuri, sio uzuri ule kwamba utashangaa hapana ila ni nzuri tofauti na nyumba zingine pale mtaani. Nyumba ina rangi safi na geti lake ndani vitu vizuri na gari yao ndogo hakika anao uwezo wa kumtosha yeye na familia yake. Na wakati ule alikuwa yeye tu kwani binti yake Faraja sikumkuta alinielezea kuwa ameenda China kusoma. Mimi nilikuwa natabasamu tu.

Usiku huu baada ya chakula mama huyu alinionesha chumba changu na nilipata nafasi nikaoga na kuingia chumbani, niliwasiliana na ndugu zangu na kisha nililala kwasababu nilikuwa nimechoka sana. Nilikuwa nimechoka.

Asubuhi niliweza kuamka, nilipotoka tu nilikuta baba na mke wake wanapata chai. Mama alinikaribisha na kunitambulisha kwa mumewe akisema “mume wangu, huyu ndiyo binti niliyekuambia.Anaitwa Cynthia.”
Nilitabasamu nikisalimia “shikamoo baba.”
Baba huyu alijibu “nashukuru sana, karibu binti jisikie upo nyumbani.”
Nilitabasamu tu. Kisha mama aliendelea kunywa chai akinikaribisha na mimi.

Huyu baba alipomaliza kunywa chai aliaga na kuniambia “Cynthia mama yako hapa alinielezea kuhusu wewe, ila unatakiwa kuwa mvumilivu kidogo ndiyo nashughulikia suala lako. Nakuahidi hivi karibuni tu kila kitu kitakuwa sawa natumai umeelewa.”
Nilimtazama nikisema “nashukuru sana baba, Mungu akubariki.”
Aliondoka na mimi nikabaki na mama tukiwa na furaha sana.

TIKTOKER:22
Siku hii tulipika na mama, tulishinda pamoja tukiwa na furaha sana, ikawa usiku mpaka tumekula tumeingia kulala baba bado hakuwa amerudi. Na mimi hapa ni mgeni siwezi ingilia maisha ya watu, hivyo nilikwenda kulala.

Na sikukawia kupata usingizi kabisa nililala usingizi fofofo. Nilipokuwa usingizini nilianza kusikia kelele. Nilishtuka usingizini na kusogea mlangoni. Alikuwa ni yule baba anamtukana mke wake matusi, matusi ya nguoni tena akimpiga.

Nilisikia akisema “huna faida wewe mwanamke, mwanamke gani wewe kwanza unaning’ang’ania kitu gani, kitu gani kinakufanya unang’ang’ana hapa, huna kwenu wewe, huna kwenuuu eeenh, hata hivyo nakuuliza kama sijui kwenu kumekujaa shida, ndiyo maana hutoki hapa, kwenu njaa kali, maskini mkubwa wewe, malaya tu huna lolote na nitakuua siku moja wewe mwanamke nitakuua.”

Niliziba mdomo wangu nisiamini kile kinachoendelea. Huyu baba alivyo mpole, mkarimu huwezi kujua ni mlevi wa kutupwa na hata anamwambia mwanamke wake maneno mabaya namna ile. Anamtukania mpaka kwao, hakika dunia imejaa vioja, kwangu mama alikuwa ana mdomo huku tena mama anaonewa. Kazi kwelikweli.

Nikiwa katika hali ile nilisikia huyu mama akilia kwa maumivu akisema “mume wangu kwanini unakuwa hivi, unaniabisha mbele ya mgeni, pombe zitakupa nini mume wangu, wewe na pombe pombe na wewe usinipige nakuomba mume wangu, usifanye hivyo.”

Alipokuwa anaambiwa hivyo ndiyo anazidi kupigwa hata nikawa naogopa, hekaheka zikawa nyingi ndiposa nikatoka chumbani kwangu nikamsaidie mama. Huyu mwanaume aliponiona alisema kilevi “umekuja saidia mjinga mwenzako maskini wakubwa ninyi, watazame kwanza sura mbaaayaaaaaaa.”

Mimi nilimkumbatia tu yule mama aliyekuwa analia, huyu baba alifunga mlango wa chumbani na kumuacha mke wake nje ya chumba chao.

Huyu mama nakumbuka alikuwa analia sana, alikuwa analia akisema “nimekukosea nini Mungu, baada ya uvumilivu wangu, ibada zangu, utulivu wangu na upendo wote haya ndiyo majibu yangu nakosea wapi mimi, wapi nakosea?”
Kama mwanamke nilimuhurumia ingawa bado nilikuwa binti ila nilielewa na kitambua maumivu yake, kabisa.

TIKTOKER:23
Nilimwambia kwa upendo “inuka mama, inuka.”
Huyu mama aliinuka kwa taabu sana, kisha tuliingia chumbani kwangu alinitazama na kusema “nisamehe sana mwanangu, nisamehe umefika kwangu unakutana na mambo kama haya. Msamehe baba yako, ni nyakati tu maana sijui nini anapitia.

Ndoa yangu imekuwa chungu sana wakati huu, ndoa yangu inaniumiza sana wakati huu. Naumia kuona haya yanaendelea, naumia kuona maisha ya ndoa yanazidi kuwa changamoto kwetu.

Ila ni mume wangu, nitaomba kwaajili yake naimani atarudi kuwa kama mwanzo. Alikuwa ni baba mwenye upendo sana, alikuwa anajali sana kuhusu familia, sijui yule mwanamke amemfanya nini mume wangu, naumia sana binti yangu, naumia!!”

Aliendelea kulia kwa uchungu sana, hali aliyokuwa nayo sikutaka kuuliza zaidi, nilijikuta namkumbatia tu kwa nguvu na upendo sana.

Nikimsihi mama huyu aache kulia ili apumzike.Ilikuwa hivyo, mama huyu alilala, nami nikalala ila usiku niliposhtuka nilimuona mama huyu akiwa amepiga maombi akilia mbele za Mungu.

Ndani ya moyo wangu nilikiri wazi mimi Cynthia, siwezi ndoa kama mambo yenyewe ndiyo haya yaani mtu na upumbavu wake kisha mimi nikeshe nikiomba kwaajili yake na matusi yote yale ilihali yeye amelala. Hapana mimi siwezi, nilimtazama na kusikitika nikalala.

Asubuhi nilipoamka, tena nilikuta kama jana hapakuwa na ugomvi, wawili hawa walikuwa pamoja jikoni wakisaidiana na kutaniana. Huyu baba aliponiona nilisalimia na kisha aliniambia “mwanangu, naona aibu sana kwako ila naomba nisamehe sana. Nisamehe kwa nilichokifanya jana sikuwa nimedhamiria nawaahidi hapa na mama yako, sitarudia.”
Mama akawa anasema “mume wangu inatosha, inatosha mume wangu naimani Cynthia ni muelewa sana.”
Nilitabasamu tu na kusaidia kuandaa chakula.

TIKTOKER:24
Baada ya hapo tulipata chai kisha baba aliaga na kuondoka zake. Nilibaki na mama, mama alinitazama tu ni wazi alikuwa anajua ninachojiuliza kichwani. Nilishindwa nikajikuta namuuliza “mama unawezaje?”

Alitabasamu akisema “ni mume wangu mwanangu, alikuwa mume wangu tangu hapo na atabaki kuwa mume wangu. Upo wakati mambo yanakuwa sio mambo bila mazuri aliyowahi nifanyia pengine nisingekuwa naye hapa. Wa kufa na kuzikana, kiapo chetu kanisani.

Watoto wasasa hamuwezi elewa kwasababu mnataka uhuru wa kila kitu. Nimeishi na kulala naye kitanda kimoja zaidi ya miaka ishirini na mitano. Amenikosea mengi, mimi pia sio malaika nakosea ingawa yake ni ya kuumiza ila haifuti ni wangu.

Maisha awali yalikuwa mazuri sana, tulikuwa tunaishi jumba zuri sana, alipata dogodogo, alipewa madawa yakutosha, mpaka anakumbuka nyumbani alikuwa hajitambui kabisa, ni Mungu tu na sasa huyu hapa.

Sasa ningemuacha mwenyewe unafikiri ingekuaje, amekuwa mume wangu, ni wangu haitabadilika ni ana mapungufu sawa, ila ni mwanaume mzuri sana kwangu, ni mzuri ana moyo mzuri naupenda sana moyo wake.”

Mimi hapo moyoni natamani hata kucheka, mimi siwezi vumilia hata kidogo upumbavu wa mtu mzima. Siwezi kabisa tena ninavyomfahamu mama yangu na alivyokuwa amemuonea baba yangu ndiyo kabisa, asingeweza kuvumilia tena mwanaume ambaye amewahi kuacha familia kisa mchepuko, kuna wanawake wanamoyo mzuri sana na mmoja wao ni huyu mama Faraja, ana roho nzuri sana.

Nakumbuka wiki ilipita nikishuhudia huyu baba anavyochelewa kurudi, mara agombane na mama na kuondoka ndiyo maisha yao nami niliamua nisiingilie tu maana kilichonileta ni kazi mengine hayanihusu.

Mama huyu tuliendelea kuzungumza mengi kuhusu maisha huku mimi nikiwa ndiyo mfuta machozi wake kuna wakati hata alikuwa akichelewa kurudi mama huyu utasikia anasema sijui kapata dogodogo nyingine basi nacheka huku nikisema mama usisieme hivyo pengine hana wazo hilo, mama anacheka tu.

TIKTOKER:25
Nakumbuka nilianza kuona dalili za kazi kwani kuna mahali baba alikuwa anapiga simu anamwambia mama nikaangalie kisha tutalinganisha hizo sehemu tuchague moja nzuri.

Nakumbuka siku moja hivi, nilitoka kuangalia duka la kuuza hii mitungi ya gas. Sasa niliporudi nyumbani palikuwa kimya sana. Na tayari ilikuwa ni mida ya saa mbili hivi usiku. Niliita “mama, mama upo wapi?”

Sikuwa nasikia sauti yoyote, ilinibidi nisogee mpaka chumbani kwake, ndipo nikawa nasikia sauti ya mama akilalamika kama vile yupo kwenye maumivu makali sana.

Sikuchelewa ilinibidi nisukume mlango, ile kuingia naona mama yupo chini analia kwa maumivu akisema “Mwanangu mpigie simu baba yako, mwambie naumwa sana nahitaji msaada.”

Haraka nikachukua simu ya mama na kutafuta jina la mumewe sikuona, akasema “mume wangu.”

Nilielewa, nikatafuta jina mume wangu, na nilipoona tu nikapiga kwa bahati mbaya simu haikuwa na dakika. Ilinibidi nichukue ile namba niweke kwa simu yangu na nipige, simu ilipokelewa na baba alikuwa sehemu yenye kelele sana. Kwa kiwewe nilisema “baba, baba mama anaumwa sana hapa nyumbani anahitaji msaada.”

Baba alisema kwa kushtuka sana “Mungu wangu!!, Mungu wangu!!, Binti toka hapo nje haraka ita usafiri mwambie dereva awapeleke hospitali kisha mimi nakukuta hospitali wewe tu utaniambia mmepelekwa wapi.”

Sikuwa na muda wa kujibu. Nilifanya kama alivyosema nikiwa na hofu sana. Nilisaidiana na Dereva mpaka kwenye gari, nikamuuliza hospitali alipojibu nikamuelezea baba. Sisi hao mpaka hospitali mama akiwa na hali ya maumivu sana. Mama alipokelewa pale hospitali haukupita muda baba alifika.

Yeye ndiye alikuwa anashughulikia kila kitu mimi nikiwa na mama. Mpaka mida ya saa tano kuelekea saa 6 ndiyo baba aliniambia “Jina lako linanisumbua sana.”
Nilitabasamu tu nikisema “niite Sinti hata nyumbani huniita hivyo.”

TIKTOKER:26
Akasema akinitazama “sasa Sintia inabidi turudi nyumbani, hali ya mama yako bado si nzuri. Ukapumzike ili asubuhi uwahi kumuandalia chochote kitu. Yeye atabaki hapa tutamuona tena asubuhi.”

Nilivuta pumzi na kuuliza “ina maana hali ni mbaya sana?”
Alinijibu “hapana sio mbaya sana, si unajua umri tu kila kitu kitakuwa sawa.”

Nilimtazama mama na kushikashika nywele zake kwani alikuwa amelala kisha mimi na baba tuliondoka.

Tulipokuwa njiani tulikuwa kimya wala hakuna kuzungumza, ndivyo alivyo baba huyu ni mpole sana. Kisha tulifika nyumbani, alinitakia usiku mwema akaingia chumbani kwake nami nikaingia chumbani kwangu. Kwakuwa nilikuwa nimechoka sana, ilinibidi nivue nguo zangu nikaoge.

Tabia yangu mbaya au ndiyo niseme mazoea yangu ni kwasababu choo kipo ndani ya chumba changu basi huwa naacha kanga kitandani kisha mimi naingia bafuni natoka navuta kanga ndiyo najifuta, kwenda bafuni na kanga au taulo na choo kipo hapahapa chumbani sio mambo yangu.

Basi nikavua nguo zangu, nikawa naoga huku naimba. Napenda sana kuimba nikiwa sina kitu nafanya, sio kwamba mimi ni msanii, hapana ni vitu tu napenda sana, napenda kupita kiasi. Na siku hii nilikuwa naimba bafuni ili kuweka akili yangu sawa.

Nilipomaliza sasa natoka ili nivute kanga nijifute maji, ndiyo naimba imba nimetoka sijatazama popote nikageuka kufunga mlango wa chooni ile narudi kutazama upande wa kitanda, nakutana macho kwa macho na baba, baba mwenye nyumba akiwa amevalia kaushi na boksa, mume wa mama Faraja, mama ambaye amekuwa akilia juu ya tabia za mumewe, mama ambaye ananipenda sana.

Mimi nipo utupu tena mikono yangu nikiwa nafuta maji yaliyokuwa yanatiririka usoni, nilishtuka na kushangaa sana, nikawa nataka kuvuta ile kanga, baba huyu aliiwahi kaka.

Akaivuta kwake, mimi nikabaki sijui nizibe matiti yangu au bustani yangu, mwili wangu ukiwa umeisha nguvu kwa kilichotokea, na namtazama baba usoni hana shaka wala mashaka. Ananitazama kwa uchu na kutabasamu, kisha alinoa koo lake na alizungumza kwa sauti tulivu sana…😂tunavyomjua Sintia maskini mama Faraja huyu atapita naye huyu simuamini mimi😂🙌

SOMA MPAKA MWISHO WA SEASON KWA SH 1000
NJOO WHATSAPP +255743433005

kslprojects

kslprojectstz@gmail.com Entrepreneurship Power

Post a Comment

Previous Post Next Post