TABORA KUNUFAIKA NA PROGRAMU YA BBT MIFUGO
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema Wizara yake ipo mbioni kuanzisha programu ya "BBT" kwa upande wa tasnia ya maziwa na nyama ambapo tayari ameshaielekeza Bodi ya Maziwa chini na kurugenzi ya uzalishaji na masoko kutoka Wizarani kwake kushirikiana na washirika wa mendeleo wa sekta ya Mifugo na Taasisi za fedha ili kuanza utekelezaji wa programu hiyo katika mkoa wa Tabora.
Waziri Ulega alibainisha hayo wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Unywaji Maziwa Duniani yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Chipukizi mkoani Tabora Juni 1, 2023.
Alisema kuwa Wizara yake ipo tayari kuanzisha programu hiyo katika Mkoa wa Tabora kwani mkoa huo una idadi kubwa ya mifugo hivyo anaamini itakuwa rahisi kupata matokeo kwa haraka mara baada ya kuifungamanisha rasilimali hiyo katika mnyororo wa thamani.
"Nina furaha kutumia jukwaa hili kutangaza jambo hilo ambalo tunaamini mbali na kutatua changamoto ya ajira kwa vijana wetu litaenda kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maziwa na nyama kwenye viwanda vyetu nchini na kupata masoko nje ya mipaka ya Tanzania," alisema Mhe. Ulega.
Aidha, alisisitiza kuwa anataka kuona vijana wanapata maeneo katika mashamba yetu ya Serikali na watengenezewe mfumo mzuri wa kuzalisha maziwa wapeleke katika viwanda vyenye uhitaji wa maziwa.
Tags
TaboraYetu