TAHADHARI ⚠️ KATIKA TOVUTI /APP HII HAKUNA SEHEMU YA KULIPIA ONLINE UKIHITAJI MWENDELEZO WA SIMULIZI BONYEZA HIYO BUTTON YA WHATSAPP AMA ANGALIA NAMBA YA MTUNZI WA SIMULIZI HUSIKA KATIKA SIMULIZI HIYO

SHUJAA 01

ONYO: SIMULIZI INAHUZUNISHA SANA.

Story: SHUJAA
episode: 01 
"Mmmmh!!! Ester tunafanyaje sasa???" aliuliza mwanadada huku akimtazama mwenzake usoni kwa umakini wenye hitaji la kupata jibu. 
Huyu mwanadada anaitwa Sophia.

"Sophia hakuna cha kufanya" alijibu Ester na kujiweka sawa kwenye kochi alilokalia. Kochi lilikuwa limechanikachanika pengine lilikuwa la zamani sana kwani hata mbao zilianza kuonekana.

Macho ya Ester yalikuwa yanazunguka kwa zamu juu ya vitu vichache sana vilivyokuwa ndani ya nyumba yake ile ambayo wengi wamekuwa wakiita kibanda cha kuku kutokana na muonekano mdogo wa hii nyumba pia uchakavu wake maana hata mlangoni palisitiriwa na bati chakavu.

Ndani palikuwa na ndoo mbili za maji, sufuria tatu na bakuli kadhaa. Kitanda kilichoshikilia godoro lake chakavu sana kilikuwa ni miti kadhaa iliyopangwa vizuri juu ya matofali kadhaa yaliyokuwa chini.

"Ester utaweza??? Acha utani hilo si jambo dogo. Angalia kwanza hali yako ya hapa unapoishi shoga yangu,,, utaweza???" alihoji Sophia jambo ambalo liliupeleka mkono wa Ester shavuni. Alishika tama huku machozi yakianza kutengeneza mifereji usoni pake.

Alitazama pembeni mithili ya mtu mwenye haya usoni pake. Hakutaka kukutanisha macho yake na macho ya Sophia. Hata hivyo kule alikoelekeza macho kulikuwa kama kitunguu kilichochokoza machozi yake kutiririka bila kukoma.

"Sasa usilie Ester. Kwa sasa tunapaswa kujua tunafanyaje?? Tufanye haraka maana mimi si mkaaji sana nahitaji kwenda kumuona Mama Jesca anaumwa"

"Sawa Sophia basi nenda tu" alijibu Ester huku anaendelea kulia.

"Hapana Ester shoga angu,, siwezi kuondoka nikakuacha bila kufikia hata robo ya tamati juu ya hili. Nakuonea huruma sana maana hakuna mwingine wa pembeni yako"

"Ni kweli Sophia,, yani hadi sasa ni wewe tu unayeonesha kunijali katika hili,, zaidi ya hapo sina mwingine" alijibu Ester na kufuta machozi kisha alimgeukia Sophia.

Sophia alimuonea huruma rafiki yake
"Ndio hivyo sasa siwezi kuondoka bila kufikia suluhisho la..." hakumaliza kuongea ulisikika mlio.
'Kweeeee!!!!' ulikuwa mlio uliowafanya wakae kimya kwa sekunde kadhaa wakati huo Sophia alionekana kushitushwa sana na hili jambo.

"Mmmh!! Nini hicho???"

"Usijali ni bati hilo" Ester alimtoa hofu mwenzake. 
Lilikuwa bati lililojisogeza pembeni kidogo kutokana na kuegeshwa tu huko juu ya paa,, mabati hayakugongelewa misumari hivyo upepo ulipopita bati lilisukumwa na kutoa sauti za kelele.

"Aah sawa! Enhe sasa ukiangalia hali ya hapa unapoishi, unadhani utaweza kweli maana hili si jambo la utani, inahitaji kujipanga Ester utaweza???"

"Sasa nitafanyaje Sophia jamani?? Naona hakuna namna"

"Mimi nina wazo"alisema Sophia huku anamtazama Ester aliyekuwa anamtazama kwa matumaini makubwa.

Ester alimtazama Sophia kwa umakini. Alisubiri kwa hamu kusikia wazo hilo.

"Cha kukushauri hapo ni kwenda kutoa hiyo mimba"

Huu ushauri ulikuwa kama sauti ya bomu iliyompeleka Ester katika mshtuko mkubwa. Alishtuka sana.

"Sophia!!!!! nini??? niseme ukweli tu pasipo kuzunguka, huo ushauri wako ni mbovu. Siwezi kutoa mimba hii hata mara moja" alitamka maneno hayo kwa msisitizo uliochagizwa na hasira kali.

Sophia alishangazwa na mabadiliko ya ghafla aliyoyaonesha Ester. Naye aliamua kupanda juu. 

"Nakushauri hivyo kwa ajili ya manufaa yako mwenyewe. Wewe mwenyewe maisha yako yanakutoa jasho sasa huyo mtoto utaweza kumlea? Utawezaa???" Alifoka Sophia. Hakutaka kumpa nafasi ya kuongea ama kujitetea. Aliendelea kufoka.

"Uko peke yako ,,huna mwingine wa kusaidiana naye. Angekuwepo Baba yake labda ingewezekana haya yuko wapi huyo Baba yake? Fanya mambo kwa akili na si kukurupuka shoga. Kama unaogopa gharama mimi nitasimamia hilo kuhakikisha unatoa huo ujauzito"

"Mimi naomba nikwambie ukweli,, shida si gharama wala hofu ya kumlea mtoto akizaliwa. Hata ningekuwa na hizo gharama za kushughulikia huo upuuzi unafikiri ningefanya??? Niko tayari kuvumilia shida hizi na ninaamini nitamzaa salama na nitamlea japo kiugumu ila si kuua kiumbe kisicho na hatia, siwezi fanya dhambi kwa makusudi kabisa" alifoka Ester asitake kabisa kutoa mimba yake ambayo ilikuwa na miezi minne tu lakini ilimsumbua mno.

Halikuwa jambo lenye urahisi kuamini kama hawa ni marafiki wakubwa tu na ambao muda mfupi uliopita walikuwa wanaongea kwa maneno mazuri na laini mithili ya mafuta. Hali ilibadilika ghafla kila mmoja alikuwa mkali kama pilipili.

Hali ya maelekezano na maelewano ilitoweka pale ndani, sasa kila mtu aliongea kwa kadri alivyoweza.

"Mimi yangu macho tu lakini chunga usijeanza kutuletea letea sauti zako za vilio eti oooh!! nahitaji msaada ,,,ooooh!! mtoto kafanyaje, kinyokoko gani" alifoka Sophia huku amebana pua.

Ester alishaona kwamba aliyekuwa naye hapo ndani ni shetani. Aliona ni heri amfukuze.

"Bibi weee, kwanza nakuomba toka nyumbani kwangu shetani ushanitibua. Ondoka nyumbani kwangu" alisema Ester na kumsukuma mwenzake hadi nje.

Sophia alitoka huku akiendelea kuongea kiuchokozi zaidi.

"Halo haloo hata banda la kuku nalo ni nyumba!? Nina shaka hata hao kuku wenyewe wanaweza kugoma kuishi humo" alisema Sophia maneno yaliyojaa kashfa na kejeli,, wapita njia waliyasikia vizuri haya maneno. Walitazama nyumba yenyewe nao wakaangua kicheko.

Ester aliumia.

Alirudi ndani akiwa mnyonge sana huku machozi yakiendelea kumtoka, alikaa chini kabisa pasipo kuhofia vumbi. Angewezaje kuogopa vumbi wakati nguo zenyewe hazikuwa safi kiasi hicho?

Hakujua ni hasira ama ni maumivu moyoni mwake yaliyokuwa yanasababisha uso wake kuchafuliwa na machozi. Alilia Ester na kila mara alipotazama nyumba yake hiyo machozi yaliongezeka maradufu. 

Pia kila alipotembeza macho kwenye tumbo lake uso ulichafuka zaidi huku moyo ukijaribu kuyashika maneno ya Sophia lakini hakuwa tayari kufuata ule ushauri.

"Najua hii ni kama vita lakini naamini nitashinda" alisema na kuinuka kwenda kuchota maji kwenye ndoo moja kuukuu iliyokuwa imehifadhi maji ya kunywa.

Alichota maji na kuyabugia mdomoni. Alipiga funda tatu na kumaliza kikombe cha kwanza. Kutokana na kiu na njaa aliamua kuongeza kikombe kingine cha maji.

Baada ya hapo alijipweteka tena chini huku akiruhusu akili yake kutafakari hili na lile. Matukio ya nyuma yalirudi haraka kichwani mwake. Hakutaka kuyakumbuka sana kwani mara kadhaa akiyakumbuka huwa yanampeleka katika kilio cha kwikwi.

Muda nao uliendelea kusonga na sasa ilikuwa saa 9 alasiri. Tumbo lilihitaji kupata kitu ila ni kitu gani angeweka tumboni mwake?? Angepata wapi hicho kitu?? Alimkumbuka mume wake. Aliamini kwamba angekuwepo basi si haba angeweza kutafuna hata kipande cha muhogo muda huu.

Hakuwa na namna, aliona ni heri aende kwa Mama yake.

"Anikatae asinikatae, mimi naenda naweza kupata chochote cha kula kuliko kubaki hapa, namtesa mwanangu aliyepo tumboni"

Taratibu alijivuta hadi kwa Mama yake, hapakuwa mbali sana ndio maana ndani ya dakika kumi alifika. 

"Wewe mwanaharamu umefuata nini hapa?? Ondoka sitaki nikuoneee ondokaa" alikaribishwa kwa namna hii. 

"Ah lakini Mama.."

"Hakuna cha lakini hapa, ondoka la sivyo nitakuitia polisi" alifoka Mama yake.

Ester aliona dunia yote imemkataa maana hata mzazi wake anamfukuza kama mbwa mwizi. Aligeuka na kuondoka huku analia njia nzima, wakati huo kumbukumbu ya mambo yote yaliyotokea nyuma iliendelea kukitesa kichwa chake.

Alitembea huku analia. 
"Kwanini Mama hataki kunisamehe?? Bado ananihesabia kosa wakati sina kosa kwanini??" Ester alililalamika kwa uchungu wakati huo huku nyuma Mama yake naye aliendelea kupaza sauti ya hasira.

"Na sitaki nikuone hapa ibilisi wewe. sitaki uje kwangu tena, muuaji mkubwa" kila neno lililotamkwa na Mama yake halikuwa tofauti sana na msumari wa moto uliokuwa unapekecha moyo wake.

Maneno yalikuwa makali.

"Ndivyo ilivyo mitoto ya siku hizi,, inajiona imekua hata kwa Mama zao. Acha likome" yalikuwa maneno ya wapita njia.

Ester aliumia zaidi. Yote haya yaliamuru macho yake kutoa machozi yaliyokuwa na kazi moja ya kuchafua uso.

Alirudi hadi nyumbani kwake na kufungua mlango wake ambao ulikuwa bati tupu lililoziba pale mlangoni. Aliingia ndani na kujitupa kwenye kitanda chake ambacho kama watu wangekiona basi wangekiita mbavu za mbwa.

Kwake ilikuwa ni sawa na mtu aliyekuwa ndani ya jengo la ikulu japo aliumia kila alipoitazama nyumba yake hii na vitu kadhaa vilivyokuwepo humo. Angefanyaje sasa??? Alikubaliana na hali yake.

"Haya yote yasingetokea kama isingekuwa wewe Janeth,,, nakuchukiaaa Janeth" alisema Ester huku anafuta machozi.

                          ★★★

Mzee Valency ni moja kati ya watu maarufu waliosifika kuwa na mali nyingi sana ndani ya kijiji cha Malangali Iringa. Mifugo alikuwa nayo wakati huo mashamba yalikuwa ya kutosha. 
Huyu mzee hakuwa tajiri kiasi hicho lakini kwa wale watu wa hali ya chini kabisa ilikuwa ni sahihi na lazima kumuita tajiri.

Licha ya mali zake hizi ila bado furaha yake haikutimia kwani wakati wote wazo na tamaa juu ya mtoto vilimtesa sana na kumnyima raha. Hakuwa na mtoto hata mmoja ambaye pengine atarithi hata shamba moja, alikuwa na umri wa miaka 20 ndani ya ndoa bila mtoto.

Alihangaika hapa na pale pasipo mafanikio yoyote yale, hela iliendelea kwenda bila kupata hitaji lake. Bado alipata shida akilini mwake. Mawazo yalimtesa, hakujua lini ataitwa Baba.

Wahenga walisema anayetafuta jambo siku zote hachoki. Mzee Valency hakuchoka wala kukata tamaa. Mungu si athumani baada ya mahangaiko ya muda fulani, alimjaalia mtoto wa kike baada ya kuhangaika kwa kiwango cha juu. Ilikuwa vyema kwao kumuita mtoto wao jina la Ester.

Ester alilelewa vizuri sana, kila alichohitaji alikipata tena kwa wakati. 
Kadri alivyoendelea kukua ndivyo mafundisho ya maadili mema yalivyoongezeka kwake. Wazazi wake walihakikisha wanampa maadili yaliyo bora zaidi.

Upekee wake ulichochea huduma nyingi na nzuri kwake. Pia kwa kuwaza kwamba urithi bora ni elimu basi alipelekwa shule. Miaka iliendelea kusonga hadi wakati alipokuwa kidato cha tatu.

Ester alitesa watu kwa juhudi zake darasani pamoja na uzuri na urembo wake. Wale wanafunzi waliokuwa wanapenda mambo ya kikubwa walimsumbua sana, hata hivyo hakuwasikiliza. Alisoma kwa bidii.

Alikuwa makini sana hasa katika uchaguzi wa marafiki kwani kila mara wazazi wake walimsisitiza juu ya hili.
Wakati huu ndio wakati alipounga urafiki na Janeth,, msichana ambaye walikuwa darasa moja. Ester na Janeth walikuwa marafiki walioshibana sana.

Ester na Janeth walikuwa marafiki wakubwa sana. Kwa namna inayoeleweka ni kwamba walikuwa chanda na pete, walitembea pamoja,, walisoma pamoja. 
Pengine kutowaona pamoja hawa wasichana wawili warembo lilikuwa jambo gumu kuliko ugumu wa jambo lolote gumu.

Urafiki ulizidi, wahusika huwa kama ndugu wa kuzaliwa tena wale mapacha kwa maana tabia na mambo mengine mengi huwa sawa kabisa. 

Tembea yao hata ongea yao walishaathiriana. 
Tabia zao zilifanana mno,, nazo juhudi zilikuwa sawa, Ester akishika nafasi ya kwanza na mwenzake nafasi ya pili darasani. Wavulana walipata tabu sana.

Maisha yaliendelea hadi kidato cha nne huku kila mmoja akiomba kwa dhati ya moyo wake ili waweze kupangwa shule moja katika elimu ngazi ya 'Advance' (kidato cha tano na sita).  

Hivi utake nini tena kwa muumba wako kipindi umepata majibu ya maombi yako. Ulie?? Au utake gunia la misumari!! La hasha! Furaha ndio hitaji na hutawala kila jambo.

Ndivyo ilivyokuwa kwa Ester na Janeth,, Mungu alijibu maombi yao kwa kuwapatia nafasi ya kuendelea kuuenzi urafiki wao wa dhati. 
Wote walifaulu na Walipangwa shule moja ambayo ilikuwa ya mchanganyiko yaani ina wavulana na wasichana. Hii shule ipo mkoani Morogoro nayo ni kigurunyembe.

Kwanini wasifurahi wakati wataendelea kuwa pamoja,, tena wamepata nafasi ya kubadilisha mazingira. Walitamani waende haraka ili wakaonje joto la Morogoro kidogo.

Wakati ulifika,, walifanikiwa kujiunga na masomo ya kidato cha tano. Maisha yaliendelea huku urafiki wao ukiendelea kupamba moto na kustawi zaidi ya mara ya kwanza.

Miezi mitatu baadaye tayari walishazoea maisha ya kidato cha tano ndani ya Morogoro,, haya mazoea yalikuwa bora sana kwa mwanafunzi yeyote yule. Ni vyema kuzoea mazingira japo huchukua muda.

Sijui ni wahenga ama ni sisi tu tuliosema kwamba hakuna jambo lenye faida tu. Kila jambo lina faida na hasara zake.
Licha ya faida kibao za ile hali ya kuzoea mazingira na maisha kiujumla pia kulikuwa na hasara zake hasa kwa upande wa Janeth.

Morogoro ilimkaa vizuri binti Janeth, ukimuona utadhani ni mzaliwa wa mkoa huo. Ule upole wake na tabia njema vikaanza kuyeyuka kama barafu kwenye jua kali la umjini mjini wa Morogoro.

"Janeth siku hizi Sikuelewi" alisema Ester siku moja wakiwa chumbani kwao.

"Hunielewi kivipi tena??" alisema huku anamalizia kupaka poda uso wake uliokuwa ushapodoka vilivyo.

"Mmh!! Unaweza niambia unajiandaa kwenda wapi??" aliuliza Ester.

"Oooh!!! Natoka mara moja,, si unajua jana sikufanikiwa kukutana na Japhet kama nilivyomuahidi maana Kelvin alinishikilia kweli kweli hapo jana" alisema huku macho yakiwa kwenye kioo. Fahamu kwamba Walikuwa wanaishi kwenye chumba cha kupanga.

"Mwanzo haukuwa hivyo ujue. Imefikia wakati hurudi kabisa nyumbani siku nzima" alilalamika Ester aliyekuwa bado amejilaza. Ilikuwa jumamosi siku hii hivyo hawakuwa na kipindi.

"Changamka Ester. Uko Morogoro dada" alisema Janeth kisha alipomaliza kuupodoa uso wake, alitazama mavazi yake, alijizungusha hapa na pale na kumtazama Ester.

"Nimependeza eh??" 
Ester hakujibu chochote zaidi alinyanyuka pale kitandani na kusali kidogo pamoja na kumshukuru Mungu wake kumlinda salama usiku.

"Haya bibi mi naondoka" alisema Janeth baada ya kuchukua kibegi chake. Huyo alitoka.
Ester alisikitika sana kumuona rafiki yake amekuwa tofauti na mwanzo wakati huo walisisitizwa sana juu ya suala hili.

Wazazi waliwaambia wasisahau gharama zinazotolewa kwa ajili yao katika kuhakikisha wanasoma tena katika shule nzuri. Walishauriwa wasome kwa bidii na kuyapa kisogo mambo mengine yasiyo ya lazima.

Ester alishangaa kuona mwenzake akienda kinyume na hayo. Alisahau yote aliyoambiwa, yeye anakula raha ya joto la mji kasoro bahari.

Janeth alikuwa hana muda na wasichana wenzake. Marafiki zake kwa sasa ni wanaume pengine isingekuwa kuishi pamoja na Ester hata urafiki wao ungekuwa ushakufa maana tayari ulianza kudidimia.

Janeth alimfanyia nini Ester???

Inawezekana unafahamu ila si kwa namna unayoifahamu.

USIKOSE KUFUATILIA NA ZAIDI ILI KUJUA YOTE YALIYOKUWA YAMEJIRI KATIKA MAISHA YAKE KIPINDI CHA NYUMA HADI HAPO ALIPO SASA.

kslprojects

kslprojectstz@gmail.com Entrepreneurship Power

Post a Comment

Previous Post Next Post